https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, February 09, 2013

Shida ya maji Handeni yatikisa Jeshi la Kujenga Taifa

Mkuu wa Mkoa Tanga, Chiku Gallawa

Na Mashaka Mhando, Handeni.
SHIDA ya maji Wilayani Handeni imeingia sura mpya baada ya jeshi la kujenga Taifa kutangaza hali ya hatari baina yake na wananchi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni jeshi hilo kuchoshwa na mvutano wa mara kwa mara uliyopo wa kugombea upatikanaji wa huduma hiyo.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkuu wa kikosi cha 835 KJ- Mgambo JKT kilichopo wilayani hapa, Meja Mohamed Mketto wakati akisoma taarifa ya kikosi hicho kwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi yaliyopewa jina la “Vijana op Sensa 2012” yaliyofanyika jana katika uwanja wa kikosi hicho uliyopo kijiji cha Mgambo Wilayani Handeni.

Meja Mketto ambaye alikuwa akieleza miongoni mwa changamoto za kikosi hicho alidai kuwa ni pamoja na tatizo la maji ambalo linakiingiza kikosi hicho kwenye mgogoro baina yake na wananchi na kufikia hatua ya malumbano yanayohatarisha usalama na amani iliyokuwepo.

Alimueleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba yamekuwepo malumbano ya muda mrefu kati ya kikosi na jamii inayokizunguuka kuhusu matumizi ya bomba la maji linalotumiwa na kikosi hicho ambapo wakati mwingine wananchi hulihujumu kwa kulitoboa na hivyo kusababisha huduma hiyo kukosekana kabisa.

Alidai kuwa kikosi hicho kinapata huduma hiyo kutoka mradi wa HTM ambayo pia si ya uhakika na hivyo wakati mwingine wanalazimika kutembea hadi kijiji cha Hale umbali wa kilometa 54 kutoka kikosini hapo.

Hata hivyo kutokana na hali hiyo uongozi wa kikosi hicho ulitahadharisha kuwa endapo hali hiyo itaachwa iendelee bila kushughulikiwa na mamlaka zinazohusika kuna hatari ya kuzuka mgogoro mkubwa usiyo wa lazima unaoweza kuathiri amani na maelewano.

Alieleza jitihada zinazofanywa katika kuondokana na kero hiyo kuwa ni pamoja na kuchimba visima virefu kikosini hapo hata hivyo alisema kuwa jitihada hizo zinagonga mwamba kwa kuwa havitoi maji hasa wakati wa kiangazi.

Kwa upande wa mafunzo hayo yaliyoanza agosti 6 mwaka jana, Mkuu huyo wa kikosi hciho alisema kuwa vijana 851 kati ya 885 waliyojiunga wanahitimu na kwamba wengine 34 hawakuweza kumaliza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, utoro, utovu wa nidhamu na kuacha kwa ridhaa.

Awali akisoma taarifa ya wahitimu hao Bw. Iman Habu licha ya kupongeza ufufuaji wa jeshi hilo, lakini pia walitoa pendekezo kwa serikali, makampuni na sekta binafsi kuelekeza mkono wa ajira kwa vijana waliyopo ndani ya jeshi hilo ambao tayari wamejifunza mambo mengi ya uvumilivu, uzalendo na nidhamu kwa ujumla.

Hata hivyo mbali na tatizo la maji walilalamikia pia ukosefu wa miundombinu ya barabara, gari ya wagonjwa na huduma za matibabu kwa ujumla na kudai kuwa inapolazimika mgonjwa kupelekwa hospitali ya Wilaya inawawia vigumu na hivyo kudhoofisha juhudi za uimalishaji wa afya zinazofanywa na uongozi huo.

Katika majibu yake kuhusu kero hiyo ya maji Mkuu wa mkoa alisema viongozi wa wilaya ya Handeni ambako alimaliza ziara ya siku tano ya kutembelea shughuli za maendeleo, wameeleza kwamba wana mpango wa kuchimba visima virefu na vifupi kwa ajili ya upunguza tatizo hilo la maji ili uondoa kero ikiwemo kikosi hicho.



No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...