https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 19, 2013

Mohammed Dida ndie mgombea Urais mdogo kuliko wote katika uchaguzi wa Kenya Imeandikwa na Hafidh Kidomwaka huu.


Imeandikwa na Hafidh Kido, Dar es Salaam

IMEBAKIA wiki moja kufanyika Uchaguzi Mkuu nchini Kenya ambapo, tayari wagombea wanane wameshapitishwa na  Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mohamedi Abduba Dida
Miongoni mwa wagombea urais ni pamoja na Mohamedi Abduba Dida alizaliwa mwaka 1975 katika Wilaya ya Wajir. Dida, aliyekuwa mwalimu, anagombea urais kupitia Muungano wa  Mabadiliko Halisi (Alliance for Real Change). Mgombea mweza wake ni Joshua Odongo Onono, ambaye pia alikuwa mwalimu.


Dida, Alisema elimu inapaswa kuwa bure kwa Wakenya wote, na siyo kwa kutegemea mfumo wa ruzuku. Ana digrii ya elimu kutoka chuo kikuu cha Kenyatta na kwa sasa anafanya shahada ya uzamili katika masomo ya dini kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Dida amefundisha katika shule kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufundisha fasihi ya Kiingereza na dini katika Shule ya Sekondari ya Daadab katika kambi mchanganyiko ya wakimbizi na baadaye katika Shule ya Lenana.

Martha Wangari Karua
Mgombea pekee mwanamke, Martha Karua katika kinyang’anyiro cha urais, alizaliwa Septemba 1957 huko Kirinyaga, Jimbo la Kati.

Karua, mbunge wa Gichugu, anagombea kupitia National Rainbow Coalition pamoja na aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Bunge la Afrika Mashariki Augustine Lotodo.

Karua ameapa kuwakilisha Muungano wa Kenya pamoja na jukwaa la mabadiliko ya uchumi na jamii, ikiwa ni pamoja na huduma za afya kila mahali na kuifanya Kenya kuwa kitovu cha uchumi katika kanda.

Alisema atatoa asilimia 10 ya bajeti ya Kenya kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuongeza vyanzo vya nishati rejezi na kufanya kazi kuwa ili kuwezesha upatikananji wa intaneti kwa asilimia 50 kwa Wakenya katika miaka mitano.  Karua ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani, Nairobi.

Kuanzia mwaka 1981 hadi 1987, Karua alifanya kazi mahakamani, alipanda kutoka hakimu wa wilaya hadi hakimu mkuu mkazi. Baada ya hapo amekuwa na shirika la uwakili binafsi hadi 2002. Mwaka 1992, Karua alichaguliwa kuwa mbunge wa Gichugu, kiti ambacho anakishikilia hadi sasa.

Peter Kenneth
Peter Kenneth alizaliwa Novemba 1965 huko Bahati, Nairobi. Yeye ni mbunge mwenye taaluma ya masuala ya benki. Anagombea urais chini ya chama cha Kenya National Congress, pamoja na mgombea mwenza Ronald Osumba.

Kenneth Pia alidhamiria kuipa polisi vifaa na kuwalipa vizuri maofisa ili kuwahamasisha kufanya kazi nzuri, na anaamini kwamba maendeleo na elimu katika maeneo yanayokumbwa na uhalifu yatazuia vitendo haramu. Anapanga kulipia programu zake kwa kupunguza matumizi makubwa ya Serikali.

Kenneth ana shahada ya kwanza na ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, pamoja na kozi ya shahada ya juu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Programu ya Utendaji kwa ajili ya Maendeleo ya Usimamizi huko Lausanne, Uswizi.

Kama mkurugenzi wa benki, Kenneth alianza kufanya kazi na Kampuni ya Fedha ya Nationwide mwaka 1985, kisha akafanya kazi na Prudential Finance na Benki tangu 1986 hadi 1997, ambako alikuwa meneja.

Uhuru Muigai Kenyatta
Uhuru Muigai Kenyatta alizaliwa Oktoba 1961. Baba yake ni rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, ambaye aliongoza tangu 1964 hadi 1978. Ni mgombea wa urais wa mungano wa  Jubilee Alliance. Muungano huo unaundwa na Chama cha The National Alliance cha Kenyata na Chama cha United Republican cha William Ruto.

Katika ilani ya muungano wake, Kenyatta ana msimamo wa Kenya iliyoungana “Chini ya ndoto moja ya kujenga Kenya bora”. Alisema atajikita katika suala la umiliki wa ardhi, na anadhamiria kuibadili Kenya kuwa kitovu cha uchumi, akijenga uchumi wa usafirishaji bidhaa nchi za nje.
 
Kenyatta ana shahada ya kwanza katika siasa na uchumi kutoka Chuo cha Amherst huko Marekani.

Baada ya kipindi kifupi cha kufanya biashara, Kenyatta aligombea kiti cha ubunge cha Gatundu Kusini mwaka 1997, lakini alishindwa. Miaka miwili baadaye, Rais Daniel arap Moi alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Kenya.
 
Alihamishiwa katika Wizara ya Fedha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, wakati akiendelea kuwa naibu waziri mkuu.

Aliacha kazi ya uwaziri wa fedha mwezi Januari 2012 baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kumtuhumu kwa kufanya uhalifu kinyume cha ubinadamu kwa wajibu wake katika vurugu za uchaguzi wa 2007-08.

Wote Kenyatta na Ruto walikabiliwa na upinzani wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusiana na kesi zao zilizosimamishwa na ICC na Kenyatta alijibu maswali kuhusiana na suala hili wakati wa mdahalo wa urais.

Profesa James ole Kiyiapi
James ole Kiyiapi alizaliwa mwezi Mei 1961 huko Osupuko, Jimbo la Bonde la Ufa. Katibu Mkuu wa zamani katika wizara mbalimbali, aliacha kazi mwaka 2012 ili kugombea pamoja na mwanamke mfanyabiashara Winnie Kaburu chini ya urejeshaji na kukijenga Chama cha Kenya Party.

Kiyiapi anasimamia ilani ya uchaguzi inayokana siasa za kikabila.  Alisema kipaumbele chake cha awali kitakuwa kuzingatia ukosefu wa ajira kwa vijana, ambalo aliita janga la taifa. Serikali yake, alisema, itashinikiza kazi ya kumaliza migogoro ya ardhi kwa uangalifu wa hali ya juu na uwazi, na itaboresha uzalishaji wa kilimo nchini.

Kiyiapi ana shahada ya uzamili kutoka katika Chuo Kikuu cha Moi na shahada ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Kanada, zote ni kuhusu misitu.

Musalia Mudavadi
Naibu Wairi Mkuu Wycliffe Musalia Mudavadi alizaliwa mwezi Septemba 1960 huko Sabatia, Jimbo la Magharibi. Anagombea kupitia chama cha United Democratic Forum katika Amani Alliance, pamoja na Jeremiah Kioni, mbunge kutoka Jimbo la Uchaguzi la Ndaragwa.
 
Mudavadi ameahidi kukuza uchumi wa uhakika nchini Kenya kwa kuzingatia utawala bora na kupunguza umaskini. Alisema atakabiliana na rushwa nchini kwa kupanga upya mfumo wa mahakama, na kuajiri maofisa polisi wengine zaidi ili kuboresha usalama.
 
Mudavadi ana shahada ya uchumi wa ardhi kutoka katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Baada ya kuhitimu, alifanya kazi katika Shirika la Nyumba la Taifa kabla ya kufanya kazi katika kampuni ya Tysons Limited inayohusika na ujenzi na upangishaji wa nyumba.
 
Mudavadi alikuwa mbunge mwaka 1989, wakati alipochaguliwa bila kupingwa kuchukua kiti cha ubunge wa Sabatia kilichoachwa wazi baada ya kifo cha baba yake, Moses Mudavadi.
 
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, Mudavadi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitano. Mwaka 1998, aliteuliwa kuwa waziri wa kilimo, kisha waziri wa habari, uchukuzi na mawasiliano mwaka 1999, na Waziri wa Uchukuzi na Mawasilino mwaka 2001.
 
Mwaka 2002, Mudavadi alipoteza kiti chake cha ubunge, lakini aliteuliwa na Rais Daniel Arap Moi kuwa makamu wa rais na alishikilia nafasi hiyo kwa miezi miwili. Kisha aligombea bila mafanikio nafasi ya makamu wa rais na mgombea mwenza Uhuru Kenyatta mwaka 2002.

Baada ya hapo, Mudavadi alisaidia kuanzisha Chama cha Orange Democratic Movement na aligombea kwa nafasi ya rais wa chama mwaka 2007, lakini Raila Odinga alimshinda.

Paul Kibugi Muite
Paul Kibugi Muite alizaliwa mwezi wa Aprili 1945. Ni mbunge wa zamani kutoka Kabete ambaye ni mwanachama mwanzilishi na kiongozi wa Chama cha Safina. Anagombea pamoja na Shem Ochuodho, Waziri wa zamani wa Nishati na mbunge kutoka Rangwe.

Muite alisema, yeye kama rais atashughulikia ukosefu wa ajira na kuboresha hali za kazi, sehemu moja kwa kupandisha mishahara na kuimarisha sheria za kazi ambazo zinaweka kikomo cha saa siku ya kazi kuwa masaa manane.

Anasema anaamini kwa umoja wa Wakenya wote, bila ya kujali makabila yao, na atafanyia kazi uboreshaji jamii na uchumi kwa watu wote. Muite anasema Kenya pia inaumizwa na sifa hasi kimataifa kwa ufisadi na rekodi mbaya ya haki za binadamu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia kupitia elimu na masoko.

Raila Amollo Odinga
Waziri Mkuu, Raila Amollo Odinga alizaliwa tarehe 7, Januari mwaka 1945 huko Maseno Jimbo la Nyanza, mtoto wa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga. Anagombea katika Chama cha Orange Democratic Movement pamoja na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kama mgombea wake mwenza.

Odinga amejikita katika vijana kwenye kampeni zake, akiwaahidi kupata ajira na elimu. Alisema kuwa atatoa pesa taslimu kwa maskini na wazee, na kuanzisha mpango kwa vijana wanaosubiri kuingia chuo kikuu au wanaotafuta kazi kwa kufundisha kwenye shule za msingi.

Odinga ana shahada ya uzamili ya uhandisi wa mitambo kutoka Chuo cha Magdeburg cha Tekonolojia ya Juu. Pia ametunukiwa digrii za heshima za uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida huko Tallahassee, Marekani.

Pia 1970, alianza kufanya kazi kama mhadhiri kwenye Idara Uhandisi wa mitambo katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Mwaka 1974, aliondoka wakati alipoteuliwa kama meneja wa viwango katika kikundi kwenye Ofisi mpya ya Viwango ya Kenya, ambako alikuwa naibu mkurugenzi mwaka 1978.

Mwaka 1982, Oginga Odinga alihusishwa kama mtoa fedha wa jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali ya Rais Daniel Arap Moi, ambaye alikuwa amezuwia jaribio la Oginga Odinga la kusajili chama cha upinzani. Raila Odinga alishtakiwa kwa uhaini na kuwekwa kuzuizini kwa muda wa miaka sita bila kesi.

Odinga aliachiwa huru mwaka 1988, lakini na kutiwa mbaroni tena mwaka mmoja baadaye kwa kuhusika na harakati za mapinduzi Kenya, kikundi kilichokuwa kkinashinikiza kuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya.

Odinga alikamatwa tena mwaka 1990 na alipoachiwa huru mwaka 1991 aliomba hifadhi huko Norway, kwa madai kwamba serikali ilikuwa inapanga kumuua.

Baada ya mwisho wa mfumo wa chama kimoja, Odinga alirejea mwaka 1992 na kujiunga na Jukwaa la Demokrasia (FORD), chama cha siasa kilichokuwa kinaongozwa na baba yake, na kushinda kiti cha ubunge katika eneo la ubunge la Langata. Mwaka wa 1997, Odinga alishindwa alipogombania urais.

Mwaka 2005, Odinga aliondoka FORD na kuasisi chama cha Democratic Movement, ambako aligombea bila mafanikio mwaka 2007. Baada vurugu iliyofuatia, Odinga akawa Waziri Mkuu katika Serikali ya umoja wa kitaifa.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...