https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, February 20, 2013

Serikali Zanzibar yaahidi kuwasaka hadi kuwatia mbaroni waliohusika na mauaji ya Padri Evaristus Mushi


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea kwa mshtuko mauaji ya Padri Evaristus Mushi na kutoa pole kwa  waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia kifo hicho.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud ameeleza hayo jana, Jumatatu, Februari 18, 2013 na kusisitiza kwamba   Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi itawasaka hadi kuwatia mikononi na hatimaye kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo.


Waziri Aboud ameyaeleza hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia mauaji ya  Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki  Zanzibar Parokia ya Mtakatifu ST.Joseph, Shangani.

Hapo jana Dkt. Shein alikutana na Askofu Augustino Shao wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, huko katika Ikulu Ndogo Migombani, Zanzibar  na kueleza masikitiko yake kutokana na mauaji hayo ya Padri Mushi wa Kanisa Katoliki la Zanzibar, na kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari,  Waziri Aboud alisema kuwa Serikali imejipanga vizuri  kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa mara moja .

“Kutokana na jiografia ya Zanzibar,Tunaelewa kwamba zipo sehemu katika kisiwa cha Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili kupambana na uhalifu “, alisema Aboud.


Alisema matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya usiri mkubwa kwa hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa mashirikiano  kwa Jeshi la Polisi pale wanapohitajika.

Akijibu suali la Mwandishi, Mhe.Aboud alikanusha taarifa zilizozagaa mitaani za kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na kuwataka wananchi kuondoa hofu. 

Sambamba na hayo, Mhe. Aboud amewataka viongozi wa dini mbali mbali  pamoja na waumini wa dini zote  hapa Zanzibar kuwa wastamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.

Aidha, Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa waumini wa dini zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa na migongano ya kidini.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...