https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 19, 2013

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO:YAH:KULAANI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI, WANAWAKE NA WATOTO

KATIKA siku za hivi karibuni, kumetokea matukio ya ukatilii  dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo yaliriripotiwa na vyombo vya habari likiwemo tukio lililotokea katika kitongoji cha Kivifuti, Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo gazeti la Habari LEO la tarehe 13 Februari, 2013, liliripoti kuwa, Bi. Maria Chambanege (39) mwenye ulemavu wa ngozi  alikatwa mkono. Halikadhalika, katika magazeti ya JAMBO LEO na MTANZANIA ya tarehe 17 /2/2013, yameripoti tukio kama hilo kutokea mjini  Sumbawanga ambapo mtoto Mwigula Magessa (7) mwenye ulemavu wa ngozi nae  alikatwa mkono na watu wasiojulikana na kutokomea nao.

 
 Kutokana na ukatili waliofanyiwa wakazi hao wenye ulemavu wa ngozi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inakemea na kulaani vikali matukio hayo ya ukatili ambayo yanawanyima watu wenye ulemavu wa ngozi haki yao ya kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo kwa wananchi wengine. Wizara inamtaka kila mwanajamii kulinda na kuthamini uhai wa mtu mwingine  ikiwemo kuheshimu  sheria na haki za binadamu. 

Ikumbukwe kuwa, vitendo hivyo vya kikatili siyo tu vinaathiri aliyefanyiwa ukatili, bali pia vinagusa na kuathiri maisha ya watu wengine katika jamii; na kuchafua sifa ya nchi yetu.

 Aidha, Wizara inaitaka jamii kubadilika na kuachana na imani potofu ambazo zinahatarisha maisha na usalama wa watu wengine na ambazo zinarudisha nyuma jitihada za Serikali za  kupiga vita ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na watoto. Wizara inawataka wananchi wote, kuwafichua wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa walinzi wa amani katika maeneo yao ili Serikali iweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

 Kwa matukio hayo, na mengine ambayo yameripotiwa  na vyombo mbalimbali  likiwemo la utupaji wa watoto wachanga matukio ambayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda na kuripotiwa na gazeti la MTANZANIA la tarehe 13 Februari, 2013. Tukio lingine ni la mtoto Kaselemako Mpale (14) aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kasumulu Wilayani Kyela Mkoani Mbeya ambaye alichinjwa na baba yake mzazi Mpale Mbisa (35) kutokana na imani za kishirikina. Aidha, kijana  Malba Hamisi(19) wa Wilaya ya Kishapu anayetuhumia kumuua bibi yake Mindi Dotto (70) kwa imani za kishirikina.

 Kutokana na taarifa hizo za ukatili ambazo zimeripotiwa na vyombo vya habari, Wizara inapenda kupongeza jitihada zilizofanywa na vyombo vya habari vyote ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili unaofanyika katika jamii jambo ambalo limeisaidia Serikali kubaini na kufuatilia taarifa za ukatili mara vitendo hivyo vinapotokea. Aidha, ripoti hizo zimesaidia  kuamsha ari kwa wananchi kuripoti matukio ya ukatili mara zinapotokea, jambo ambalo limesaidia kuwachukuliwa hatua za kisheria wale wote wanaobainika kuhusika na matukio hayo. Wizara inahimiza wananchi kuendelea kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na kupuuza imani za ushirikina katika kujiletea maendeleo yao.

Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...