https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, February 25, 2013

Soka la Tanzania ni ubabaishaji tu



SIWEZI KUVUMILIA

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WANAFURAHIA na jinsi mdau wa Simba, Rahma Al Kharous kujitolea kulipa fedha zinazodaiwa na kocha wao wa zamani, Mserbia, Milovan Cirkovic,  Dola 35,000 zinazofikia Shilingi milioni 51 za Tanzania, lakini hawajaumizwa na ubabaishaji mkubwa uliokuwa ndani ya klabu yao, kiasi cha kuleta balaa na mkanganyiko kwa wadau wa michezo.

Kwa mfano, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alinukuliwa hivi karibuni, eti akimtaka Milovan arudi kwao, huku wao wakifanya utaratibu wa kumtumia fedha zake anazodai, kama atawaachia akaunti yake ya benki.

Huu ni uzandiki wa aina yake. Kwani kabla ya hapo, Simba walikuwa wanalipana kwa mtindo gani na kocha huyu wa Kimataifa? Au walikuwa wanapeana fedha dirishani kama dukani?


Hili ni swali ninalojiuliza, huku nikitangaza kuwa mimi ni miongoni mwa watu waliochefuliwa kwa kiasi kikubwa na mwendo wa ubabaishaji wa soka la Tanzania.

Ubabaishaji huu haupo Simba, Yanga bali upo pia kwenye mhimili wa soka letu, ambaye ni Shirikisho la Soka nchini (TFF), chini ya Rais wake, Leodgar Tenga, akiwa na kamati zake nyingi ambazo baadaye zinasigana zenyewe.

Hili ni tatizo kubwa. Hivi, kama klabu haina utaratibu wa ulipaji mishahara au madeni yake kwa watu unafikiri kuna maendeleo hapo? Nimekuwa nikiumizwa na suala hili kila wakati. Simba, imekuwa ikifanya kazi zake midomoni zaidi.

Haina jipya, ndio maana hata suala hili la deni la Milovan, lingekuwa aibu kubwa kwake, kwakuwa mipango ya kulipwa haikuwapo. Najua hili ni jambo ambalo wenyewe Simba, akiwamo Rage asingependa kuona linasemwa, ila huo ndio ukweli.

Na ukweli hauwezi kufichwa hata siku moja. Rage aliyekuwa anasema kuwa Simba haiwezi kulipa bila akaunti ya kocha huyu, akalazimisha arudi kwanza kwao, haoni huu ni ubabaishaji? Je, huyo wanayemuita Malkia wa Nyuki amelipana naye kwa mtindo gani?

Hii sio njia nzuri ya kuleta maendeleo ya soka kwa Tanzania. Lazima wadau wote tufahamu kasoro zetu, kama kweli tuna lengo la kukuza mpira wa miguu. Kama kila sehemu kutakuwa na porojo, hadithi hatuwezi kufika mbali.

Miaka nenda rudi, soka la Tanzania limekuwa likichezwa zaidi katika midomo, jambo ambalo hakika haliwezi kufurahisha wenye mtazamo wa kimaendeleo. Hivyo basi, viongozi wetu wa soka lazima wajuwe na kujifanyia marekebisho.

Huwa nakerwa sana na hadithi kama wanasiasa. Na yoyote anayefanya kazi kwa mtindo huo, lazima tumseme na kumkosoa, maana hawezi kutuletea maendeleo hata kidogo. Huo ndio ukweli, ndio maana siwezi kuvumilia.

Klabu za Tanzania, ikiwamo Simba lazima iweke utaratibu wa kulipana mishahara vizuri, bila ubabaishaji kwa kuzingatia mikataba ya Kimataifa. 

Simba inapaswa ijuwe kuwa haifanyi kazi na Watanzania pekee kama vile Jamhuri Kihwelo Julio, kocha wao msaidizi, Juma Kaseja, kipa wao au wachezaji wengine wanaoweza kulipwa hata dilishani.

Lakini kuchanganya watu wa nchi mbalimbali, kunatakiwa kutumika vyema kwa kuwekwa utaratibu mzuri kwa ajili ya kuleta ushirikiano kwa wadau wote. Kama kila mtu ataona ubabaishaji huo, hata nidhamu, moyo wa kujituma hupungua kama sio kwisha kabisa.

Hili wakati mwingine linazua kinyongo, hivyo kuondoa kabisa moyo wa kujituma uwanjani, ingawa baadaye huzushwa kuwa wachezaji wameuza mechi. Haya ni mambo ya ajabu. Katika michezo, hasa mpira wa miguu ni matokeo mabaya mno.

Ndio maana nilishindwa kuvumilia, nilipoona ahadi, kuzunguushana kwa kupitia majibizano kwenye vyombo vya habari kama waimbaji wa taarabu. 

Mara linasemwa hili, kesho yule anajibu, ingawa ukweli unajulikana.
Kama asingelipa fedha hizo Rahma, ina maana Milovan fedha zake asingezipata leo, japo alikuwa anapewa ahadi na kauli za kila aina. Kwa Simba inayoijua sasa, kulipa kiasi cha Sh Milioni 51 kwa wakati mmoja ni jambo gumu.

Fedha za milangoni zinazogawiwa kwa timu zote mbili inazocheza nazo ni ngumu kupunguza Milioni 51 kwa ajili ya kumpa Milovan. Hata hivyo haitoshi, fedha zote zinazopatikana kwenye mchezo mmoja, huwa na mgawo mkubwa kwa kila upande.

Utakuja kushuhudia mchezo mmoja klabu hiyo inaambulia Milioni 10 au 20 kwa mechi iliyoangiza kiasi kisichozidi Milioni 60. Huu ni ukweli, hivyo walau sasa wadau wa soka, wakiwamo viongozi wetu waache ubabaishaji kwa ajili ya kunusuru soka letu.

Kama tunataka kupiga porojo, hadithi tufanye wenyewe na sio kuwasumbua watu kutoka Mataifa mengine, maana kuna siku tutalia na kusaga meno. Kama kila mtu anasumbuliwa na mashtaka kupeleka CAF au FIFA, sumu hiyo inazidi kusambaa.

Yanga hadi sasa inasumbuana vibaya na mchezaji wake, raia wa Ghana, Kenneth Asamouh, nako kukiwa na ubabaishaji wa aina yake. Ukiacha huyo Milovan, bado Simba ilikuwa inadaiwa na kocha wake , Mganda, Moses Basena, lakini ilishangaza alipofuata fedha zake Tanzania, akapewa tena kibarua, kama njia ya kumziba mdomo.

Huu nao ni ubabaishaji wa kutupwa. Mtu afuate fedha zake, nyie mnampa kazi ya usaidizi, huku mnajua uwezo hamna wa kuwalipa kwa wakati. Kwa mfano, wakati Basena amekuja kuchukua fedha zake, Simba inanolewa na Patrick Liewing, akiwa na msaidizi wake, Jamhuri Julio.

Kwa matokeo hayo, Simba ikawa na makocha watatu, akiwa na Basena, aliyezibwa mdomo, mara baada ya kutua Dar es Salaam. Haya ni matokeo gani kama sio ubabaishaji? Hatuwezi kwenda hivi. Lazima tubadilike kwa ajili ya soka letu.

Tutafanya kila tuwezalo, lakini kama utaratibu wetu mbovu, uongozi wetu mbovu ushirikiano wetu hausemeki, hakika tusitafute mchawi, maana kumpata mtu makini, anayejitambua, eti aache kucheza soka kunakoeleweka na kuja kwa Simba, Yanga, itakuwa ndoto.

Hakika hii siwezi kuvumilia na tujiangalie upya na ubabaishaji wetu huu unaokera watu walioendelea kwenye Mataifa yao.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949, 0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...