https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, February 11, 2013

Wachezaji Coastal Union wanataka nini?



 SIWEZI KUVUMILIA
Msemaji wa Coastal Union, Edo Kumwembe

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA vitu kwenye mpira wa miguu vikikutokea, hasa kwa wale wanaowekeza au kudhamini timu mbalimbali, matumbo yao huuma. 
Wadhamini wa Coastal Union wanavyoonekana pichani.

Hata hivyo haitoshi, huchanganyikiwa na kutembea wakisema peke yao, wakikumbuka fedha zao zinamwagika na hakuna ushindi unaopatikana.

Bila kuficha, suala hili lilimsababisha mmiliki wa zamani wa African Lyon, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji ‘Mo’ aipige bei timu hiyo.


Hakuona maslahi zaidi ya kumpa presha na hasara ya fedha za kuihudumia, kuanzia kambi, safari na mishahara ya wachezaji, bila kusahau viongozi wao, kama vile Mwenyekiti, Katibu Mkuu na benchi la ufundi.

Kwanini nasema hivyo; hakika najikuta siwezi kuvumilia kuona mwenendo mbaya wa timu Wagosi wa Kaya, Coastal Union inavyopata matokeo mabaya licha ya wadau kutoa misaada mingi, bila kusahau ufadhili wa Nassoro Binslum.

Kwa miaka kadhaa sasa, nashangazwa na taarifa za Coastal Union kupanda ndege kuelekea kwenye mchezo wao na Toto African ya Mwanza. Katika mchezo huo uliochezwa Jumamosi iliyopita,. Timu hizo zilizotoka sare ya bila kufungana.

Kwanini? Ingawa kufungwa, kushinda au sare ni matokeo ya kawaida kwenye mchezo wa soka, lakini kwa jinsi Coastal inavyohudumiwa, nilijidanganya kwamba sasa itakuwa tishio walau kushika nafasi ya kwanza kama sio ya pili.

Timu hiyo ya jijini Tanga, ndani ya ngome ya Mkuu wa Mkoa Tanga, mama Chiku Gallawa, sasa inaishi kama zinavyoishi nyingine, hasa Simba, Yanga, Azam, maana nayo inajiweza.  Huwezi kuona Coastal ya leo inalalama kushindwa kwenda mikoani kwa kukosa nauli.

Wakati ikienda Mwanza kwa ndege, tayari uwezekano wa kuwafikisha kwa basi wachezaji na viongozi wao hadi Bukoba kwa basi ulishaandaliwa, hasa kwasababu ni karibu na  vijana hawawezi kuchoka, kuelekea mchezo wao na Kagera Sugar.

Hakika siwezi kuvumilia. Inauma, maana kama Coastal haifanyi vizuri leo, ni lini tena itafanikiwa kuonyesha soka la uhakika, ishinde na kuwa tishio zaidi. Hata kama ishindwe kunyakua ubingwa, lakini nafasi ya pili au ya tatu ni muhimu.

Uwezo huo wanao, maana wapo vijana wenye uwezo mzuri wa kucheza soka, kama vile Shaban Kado, Ismail Suma, Othman Tamimu, Phillip Mugenzi, Mbwana Khamis, Jrrry Santo, Joseph Mahundi, Razak Khalfan, Daniel Lyanga, Mohamed Sudi, Selemani Kassim, Rajabu Kaumbu, Gerald Lukindo, Ibrahim Twaha, Gabriel Barbosa, Hamad Juma, Khamis Shengo na wengineo wanaopigania namba katika kikosi hicho cha Coastal Union.

Hii ni aibu kubwa, maana wachezaji wameshindwa kabisa kucheza jihadi uwanjani ili kuleta matumaini kwa wadau na mashabiki wao. Coastal Union huwezi kuifananisha na timu ndogo ndogo kwa sasa, ikiwapo Toto African pamoja na timu za Polisi.

Inapofikia kuendelea kukaa nafasi ya nne, tena kwa matokeo yasiyokuwa na mashiko, ni wazi kupanda juu zaidi itakuwa ndoto. Nasema hivyo kwasababu ligi inazidi kuwa ngumu, hivyo hakuna timu itakayotaka kufungwa kirahisi.

Huu ndio wakati wa vijana kuonyesha kwanini wao wanaitwa wachezaji wa mpira wa miguu. Wafie uwanjani ili wenye kutoa fedha zao, wenye kulipa viingilio vyao kuendelea kupata moyo huo na sio kufanya mambo yasiyoeleweka.

Hali ikiendelea kuwa hivi, ni wazi wenye moyo wao watashindwa. Tatizo kubwa la ligi yetu ipo kwenye safari, hasa za mikoa ya Mwanza na Bukoba. Kwa mfano Coastal kutoka Tanga hadi Mwanza na Bukoba, hakika fedha za uongozi tu hazitoshi kamwe.

Ndio hapo wadau, akiwapo BinSlum anapoonyesha umahiri wake kwa vijana, ndio maana anamwaga fedha zake, ingawa tunaamini anashirikiana na wanaopenda maendeleo ya Coastal Union.

Labda niulize swali, hawa vijana wa Coastal Union wanataka nini tena? Kama wanaishi maisha mazuri, kama wanavyoishi Simba, Yanga, Azam nini tena zaidi? Wachezaji hawa lazima wajuwe wana deni kubwa na timu hiyo.

Mashabiki wa soka wa Tanga nzima hawataki kuona visingizio visivyokuwa na mashiko, ukizingatia kuwa kila kitu vijana hawa wanapata. Mikoa ya karibu yote, ikiwamo Dar es Salaam, Morogoro na Arusha basi zuri tu wanalo.

Kwa timu kama Coastal, hakika inahitaji kufanya bidii, kujituma kwa nguvu zao zote, ili washike walau nafasi ya pili na kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho katika hali ya kuonyesha makali yao na kuuza majina yao.

Wachezaji wanaangalia Simba na Yanga, kwasababu wanapata nafasi ya kuoanda ndege mara kwa mara wanapokwenda nje ya nchi, lakini zamu hiyo sasa ipo kwa Azam FC. 

Kama timu nyingine ndogo, ikiwamo Coastal ikishika namba mbili, walau sasa tunaweza kubadilisha fikra zetu kuwa mazuri yote yapo kwa wakongwe, wakati si kweli.

Ndio maana nasema, wachezaji wa Coastal Union wanahitaji nini zaidi? Au wanataka roho za wadau na mashabiki wao? Hii presha wataiacha lini? Ni lini watacheza soka la jihadi kwa timu zote? 

Katika kulisema hilo, naamini uongozi utakaa chini na wachezaji wao kuliangalia tatizo liliopo, huku nikiomba Mungu iendelee kubaki kwenye ligi kwa kutimua mizigo ndani ya timu.

Uongozi ndani ya timu hiyo upo chini ya Hemed Hilal (Aurora) kama mwenyekiti, huku nikiamini kuwa mwendo huu mbovu unamuumiza kichwa kama wanavyoumia mashabiki na wadau wao wanaoisaidia visenti vyao ili kuiwezesha Coastal Union.

Hakika siwezi kuvumilia, maana kama kila kitu timu inapata, wanataka nini tena?
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...