Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA wale wanaonufaika na wizi wa tiketi au kuuza tiketi za
bandia katika viwanja kadhaa vya michezo, hususan katika Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam, kamwe hawezi kufurahia ujio wa tiketi za kieletroniki.
Hii ni kwa sababu tiketi hizo zitawaua njaa. Watashindwa
kuishi vizuri mjini wao na familia zao. Ndio maana tumeendelea kushuhudia
malalamiko au maoni ya wadau wakielezea uuzwaji wa tiketi hizo kwa jinsi
walivyojua wenyewe. Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia.
Katika mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa hivi karibuni,
wapo watu waliokamatwa kwa kununua tiketi za bandia. Tiketi hizi zinauzwa kama
njugu na wanaokamatwa ni wachache kati ya wengi wanaofanikiwa kuingia uwanjani
kwa tiketi za bandia.
Hawa wanasababisha mapato yawe kiduchu. Wanadhulumu jasho la
wachezaji na maandalizi yao yanayotumia gharama kubwa. Hii si haki. Ni vyema
serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakaweka juhudi katika uuzwaji wa
tiketi hizo ili wachache wasiendelee kufanikiwa kwa wizi huo.
Wakati nasema haya, nakiri kabisa mtu asiyekuwa na mtandao wa
wizi huo wa tiketi za bandia, kamwe hawezi kupinga au kuhujumu mradi wa tiketi
za eletroniki maana ni jambo lenye dira na mguso.
Wachache wanatajirika kwa biashara hiyo isiyodhibitiwa.
Kutodhibitiwa huko kumezidi kuongeza watu wanaohujumu mradi wa tiketi huo kwa
sababu ndio kwenye pona yao. Hapa siwezi kuvumilia.
Vyema juhudi zikawekwa ili kuhakikisha kwamba juhudi za
ununuaji wa tiketi za eletroniki zinawekwa ili kulinda mfumo huo na wahujumu
wanaofanya mbinu za aina mbalimbali kuukwamisha.
Wachache wenye mapenzi na mpira wa miguu na ndoto ya kuona
nchi yetu inapiga hatua, hatuwezi kukubali vitendo vya wizi wa tiketi za bandia
unaofanywa na hawa hawa wanaopiga vita uuzwaji wa tiketi za eletroniki kwa
faida zao binafsi wao na familia zao.
Kinyume cha hapo mfumo huu hautafanikiwa.
Tuonane wiki ijayo.
+255 712053949
No comments:
Post a Comment