Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NAPOKEA simu ambayo nashindwa kuielewa. Simu hii inatoka kwa
rafiki yangu anayeishi mjini Dodoma, anayejulikana kwa jina Mustafa Mussa
Seiph. Kijana huyu ananiuliza juu ya habari za kifo cha Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Kapteni John Komba.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akimuaga marehemu Kapteni John Komba.
Komba amerafiki Dunia
huku akiwa anategemewa kwa kiasi kikubwa kwa jimbo lake la Mbinga
Magharibi, bila kusahau Chama Cha Mapinduzi kinachojiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Mwezi Oktoba mwaka huu nchini kote.
Kuulizwa juu ya kifo cha Komba kiliendelea kutoka kwa watu
tofauti waliokuwa wameshangazwa na habari hizo juu ya msiba wa nguli huyo wa
muziki, ambaye mara kadhaa nyimbo zake zimekuwa zikitumika kwa matukio muhimu.
Marehemu Kapteni John Komba, enzi za uhai wake
Baada ya kufuatilia katika vyanzo tofauti, hatimae
nilikubali matokeo kuwa Kapteni Komba hatupo naye duniani, yani ametangulia
mbele ya haki, Februari 28 katika Hospitali ya TMJ, jijini Dar es Salaam,
akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari. Ni majonzi makubwa kumpoteza mtu kama
Komba, hii ni kutokana na umuhimu wake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika kufuatilia suala la kifo cha Komba, mtu anaweza
kufika mbali kwa kuona ni bora angebaki yeye na kuondolewa watu kadhaa ambao
kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wa kawaida ndani ya chama na serikali kwa
ujumla.
Hata hivyo, wakati tunaendelea kuomboleza kifo cha Komba,
wanajitokeza wachache wenye roho mbaya na kufurahia kifo chake. Kwanini? Ni
binadamu gani mwenye roho ya utu anayeweza kufurahia kifo cha binadamu
mwenzake?
Hata jamii hiyo inatofautiana kisera, kidini au kiitikadi
bado si sababu ya kuona mtu anashangilia kifo cha mwenzake, kama anavyoweza
kushangilia mnyama aliyeangushwa. Nchi yetu yenye amani na utulivu, watu wa
aina hii wanatokea wapi.
Inashanaza na kuumiza. Ni punguani pekee anayefurahia kifo
cha Kapteni Komba. Ingawa alikuwa mwana CCM, lakini pia alikuwa mbunge na
mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Mbinga Magharibi Tanzania Bara.
Hakuwa na uadui kiasi hicho. Ndio maana tulishuhudia watu
wengi wakipokea kifo cha Komba kwa masikitiko makubwa. Nani atairithi sauti
yake. Nani atatumia muda mchache kutoa nyimbo bora zinazosimamia uzalendo na
kuhamasisha mengi nchini kwetu.
Inasikitisha kuona siasa zinaondoa utu wetu. Kama viongozi
wa upinzani wote wameumizwa na kifo cha Komba, mfuasi gani anayeweza kuwa
tofauti na wakubwa wao? Hata kama alikuwa na jambo lisilofurahisha wachache
wao, bado sio sababu ya kuanza kumdhihaki kwa namna moja ama nyingine, hata
pale tunapoliona jeneza lake.
Binadamu duniani tunapita tu. Safari yetu ni moja. Unapoona
mwenzako ametangulia mbele za haki, jua na wewe unafuata. Huo ndio ukweli.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbroad Slaa,
alizungumzia kifo cha Komba kwa huzuni za aina yake.
Kama hivyo haitoshi, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba, alionyesha mapenzi kwa Komba. Idadi kubwa ya viongozi
kutoka vyama vya upinzani walionekana kwenda kwa wingi kumuaga marehemu Komba,
aliyezikwa jana kijijini kwao Lituhi.
Hii ni kuonyesha kuwa upinzani na kushindana ni kwenye siasa
tu. Inapotokea suala la kifo, hakika kila mmoja wetu anapaswa kuumia. Kama
hivyo ndivyo, hakika nawashangaa wanaotumia muda mwingi kumdhihaki, wakitumia
mwanya huo kutokana na misimamo yao tofauti.
Hizo sio siasa. Angalia, Komba alikuwa akiamini kuwa
anayestahili kumrithi Rais, Dr Jakaya Mrisho Kikwete ni Edward Lowassa tu.
Alilisema hili mchana na usiku. Alisimamia kwenye hoja yake hiyo bila woga
wowote. Lakini kuonyesha ukomavu wa kisiasa na pia huzuni katika matatizo, bado
haikuwa sababu ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, kuacha kuhudhuria msiba wa mwanasiasa huyo.
Si Membe tu, kundi la wagombea urais wengi ndani ya CCM
walimiminika kwa wingi kuomboleza msiba huo bila kuangalia Komba aliwaunga
mkono au aliwapinga. Ndio siasa zinavyotaka moyo na uzalendo wa hali ya juu.
Ukiacha katika majukwaa ya kisiasa, bado sote ni binadamu na
Watanzania halisi. Tunapaswa kuishi kwa upendo. Hatupaswi kufurahia matatizo
yanayotokea wenzetu. Huo si ubinadamu. Ni zaidi ya unyama usiostahili kuungwa
mkono.
Mara baada ya kupata taarifa za msiba huo, sikuridhishwa
hata kidogo juu ya watu waliokuwa wakisambaza picha mbaya za marehemu Komba.
Wengine walifika mbali kwa kusambaza picha ya saa chache baada ya kifo chake.
Bado najiuliza. Watu wa aina hii hawajui uchungu wa kufiwa?
Hivi kama aliyefariki ni baba zao, mama zao au mtu wao wa karibu anaweza kupata
ujasiri wa kuisambaza picha ya marehemu? Hata kama anao moyo huo, bado hauwezi
kumtuma awatumie picha isiyoridhisha wengine.
Huu si uungwana. Fikiria usambaziwe picha ambayo kiuhalisia
tu haifai, utajisikiaje? Kama sababu ni siasa, je picha hizo za marehemu
zimesambazwa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar,
Salum Mwalimu au viongozi wengine?
Upuuzi huo unafanywa na watu wasiofahamu hata gharama za ada
ya uanachama wa Chadema kwa kipindi cha mwaka mmoja. Watanzania tusifike huko.
Msiba wa Komba si wa CCM na familia yake tu, ila Watanzania wote wameguswa.
Kabla ya kuingia kwenye siasa, Komba alikuwa mwalimu. Pia
akawa mwanajeshi. Nafasi zote hizo zilikuwa ni za kuwatumikia Watanzania wote.
Na kama kelele zinakuja kwa sababu ya kupingana juu ya maoni ya Katiba, sidhani
kama ni sahihi.
Hii ni kwa sababu kila mtu alikuwa na ruhusa ya kutoa maoni
yake aliyoona yanafaa kwa ajili ya kujenga mustakabali wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Na si Komba tu, ila inapotokea msiba, hakuna haja ya kuonyesha
chuki dhidi ya wenzetu hao.
Tuwaombee dua tukiamini nasi tunaelekea huko. Hakuna
atakayeishi milele. Leo ni Komba, kesho ni wewe au mimi. Pamoja na mambo hayo
machache ambayo wasiojua nini maana ya siasa wanalalama, bado Komba alikuwa
mmoja wa viongozi makini na wenye mchango katika Taifa letu.
Komba aliweza kusimamia hoja zake bila haya wala soni. Siasa sio chuki wala uadui. Mtu anayeweza
kuudhihaki mwili wa marehemu huyo ana walakini. Ni punguani pekee anayeweza
kufurahia msiba wa Komba au binadamu mwenzake yoyote.
Watanzania sisi wote ni wamoja. Rais Kikwete alidhihirisha
namna gani kifo cha Komba kimemgusa yeye na Watanzania wote baada ya kushindwa
kujizuia kutoa chozi. Wengine walionekana kutoa chozi ni Katibu Mkuu mstaafu wa
CCM, Yusuf Makamba na wengineo wengi waliomiminika katika Viwanja vya Karimjee
kumuaga Kapteni Komba.
Huenda viongozi hao wa CCM walijaribu kuvuta picha katika
kampeni zijazo. Lakini pia wengine wanajaribu kuangalia namna gani umuhimu wa
Komba ulipaswa kuendelea kuwapo katika nchi yetu inayopambania maisha bora kwa
kila Mtanzania.
Ni kutokana na hilo, naomba Watanzania tuwe wamoja katika
kumuombea marehemu Komba akapumzike kwa amani, sanjari na kuomba dua kwa
viongozi na wananchi wote katika sekeseke la uchaguzi lililozidi kushika kasi.
Hakuna haja ya kumdhalilisha marehemu hata kama kuna aliyokuwa
akiyafanya huvutiwi nayo, hii ni kwa sababu hakuna aliyekamilika hapa chini.
Nenda Komba. Tutakumbuka, ila ni punguani pekee anayefurahia kifo chako.
+255712053949
No comments:
Post a Comment