Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NASHAWISHIKA kusema kwamba baadhi ya viongozi na watendaji wa
serikali katika wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, hawanazo kichwani. Na kama
wanazo, basi wamegubikwa na maslahi zaidi. Wameshindwa kusimamia mambo yenye
tija kwa wananchi na wakazi wao wilayani Handeni.
Mmoja wa wakulima wadogo walioporwa mashamba yao katika moja ya vijiji vya wilaya ya Handeni, Hausi Zuberi pichani.
Ndio hawanazo. Maana yapo mapungufu ya wazi ambayo kwa mtu
mwenye akili hawezi kuyaacha yashamiri. Mtu mwenye nazo kichwani, atayafanyia
kazi matatizo yanayowahusu watu, ukizingatia kwamba ndio kusudio la uwapo wake
kwenye nafasi nyeti za serikali, kama ardhi, maji, afya, kilimo na mengineyo
muhimu.
Baadhi ya mambo hayo hayahitaji hata elimu ya kidato cha nne kubaini mapungufu. Ni kutokana na hilo,
nadiriki kusema viongozi wa serikali wamenyamaza, wakiwa na lengo la kuona
Handeni inamwaga damu kutokana na migogoro ya ardhi.
Katika kila kijiji cha wilaya ya Handeni kina migogoro
mikubwa ya ardhi. Hali hiyo inatia hofu. Migogoro hiyo ni ile inayohusisha
wakulima na wafugaji, wakulima wadogo na wafanyabiashara waliopewa jina la
madalali wa ardhi, ama mipaka inayohusisha vijiji, bila kusahau wilaya kwa
wilaya katika baadhi ya maeneo.
Na migogoro hiyo imekuwa kero kiasi cha kuwafanya wananchi
wakose imani na viongozi na watendaji wa serikali katika maeneo yao. Wanafanya
hivyo kwa sababu kero zao hazitatuliwi.
Kilio cha wananchi kimeendelea kuwa cha samaki, machozi
yanakwenda na maji. Hii n hatari. Tulipofikia ni kubaya na wakati wowote
wananchi wataanza kupigana.
Watamwaga damu kama wanavyomwaga damu katika maeneo mengine
ya nchi. Ajabu, licha ya wakulima na wananchi kulalamikia suala hilo, lakini
hawasikilizwi. Watendaji wa serikali wamebakia kuwatumikia wenye nazo.
Wanachumia tumbo.
Chaguo lao kwanza ni wafugaji wakiamini kuwa watalipwa
fedha au rushwa ya wanyama, kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo. Ama wale
wakulima wakubwa wenye nazo.
Hao ni rahisi kwenda Polisi na kupata askari wa
kuongozana nao eneo la tukio kwa ajili ya kuwaogopesha wananchi.
Hakuna haki anayeipata mlalahoi. Katika vijiji 112 vya wilaya
ya Handeni hakuna kilichokuwa na ahueni. Huko watendaji wa vijiji baaadhi yao
wamekuwa madalali wa kuuza ardhi. Na wenyeviti wengi wamefikia kughushi
mihutsari inayogawa ardhi kwa wafanyabiashara bila kuangalia sheria ya ardhi.
Kesi nyingi zipo kwenye makaratasi. Hazisikilizwi kwa wakati.
Na zikisikilizwa, basi mwenye nazo anapewa haki wakati mkulima mdogo akiendelea
kulia bila kupata msaada wowote.
Kwa mfano, katika Kata ya Kwamatuku, kijiji cha Komsala na
Kwamatuku ambayo ni kata zipo kwenye mgogoro mkubwa mpaka uliosababisha ardhi
kuporwa na kupewa mwekezaji anayejulikana kwa jina la Optimal. Shamba hili la
Optima limechukua eneo kubwa, kiasi cha kuingia hadi Komsala bila kufuata sheria.
Hapo hujaugusa mgogoro wa mpaka wa wilaya ya Korogwe uliyoingia hadi karibu na
eneo la kijiji cha Komsala. Korogwe wameamua kujenga mnada wa ng’ombe katika
eneo la kijiji cha Komsala.
Aidha katika kijiji hicho pia kuna mivutano ya wenye nazo
kupewa mashamba makubwa hali ya kuwa walalahoi wameachwa mikono mitupu. Hakuna
kinachowafanya waendelee na kulima. Ardhi kubwa inamilikiwa na wenye nazo.
Yupo mwanamama anayejulikana kwa jina la Amina Singa ambaye
licha ya kuwa na eneo linalozidi heka 120 bila kujua sheria iliyompa ardhi
hiyo, lakini bado ameingia kwenye maeneo ya wakulima wadogo wanaomiliki heka
nne hadi tano.
Huu ni zaidi ya ufisadi. Na kesi kama hizi hazitoi haki kwa
masikini, wakiumizwa na msemo usemao mkono mtupu haulambwi. Kwa ujumla, kata
zote za Handeni hususan zile za vijijini ni migogoro iliyostawishwa na
viongozi. Katika Kata ya Misima ambayo leo inaitwa Mabanda ni mtihani mzito.
Licha ya kesi kusikilizwa kwenye Baraza la Ardhi la wilaya
Korogwe kutokana na Handeni kutokuwa na Baraza hilo, lakini bado wakulima
wadogo wanakamatwa na kufunguliwa kesi katika mahakama ya mwanzo wilayani
Handeni.
Hii hutokea kinyume cha sheria. Hakuna sababu ya kufungua
kesi mpya wakati kesi kama hiyo haijapatiwa ufumbuzi. Katika mgogoro mkubwa
unaomuhusisha Michael Panga maarufu kwa jina la NADA katika Kata hiyo na
wananchi ni unyanyasi mtupu.
Kumbukumbu za kiofisi zinaonyesha NADA aliazimwa alime katika
shamba ambalo uongozi wa mtaa wa Kwedigongo, kijiji cha Misima kwa kupitia
mwenyekiti wake Idd Kisege, waliamua kuichota aradhi hiyo kwa ajili ya kupewa
wakulima wadogo.
Jambo hilo lilimfanya NADA akimbilie kwenye Baraza la Ardhi
Machi 4 na kupewa Stop order, ambapo kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mwezi
Aprili mwaka huu. Kumbukumbu zinaonyesha waliopokea barua ya Baraza la Ardhi na
Nyumba la wilaya ya Korogwe ni pamoja na Mkurugenzi, Mkuu wa wilaya, OCD, OCS,
Katibu Tawala Sindeni na WEO Kata ya Mabanda.
Kama hivyo ndivyo, nani ameruhusu kumkamata Idd Kisege ambaye
ni mwenyekiti wa Mtaa wa Kwedigongo na kumfungulia mashtaka wakati kesi kama
hiyo itasikilizwa mwezi wa nne?
Hii ni aibu kubwa. Viongozi na watendaji wa serikali
wanaendelea kuikalia vikao migogoro ya ardhi kwa nia ya kuvuta posho na si
kuchukua hatua kwa maslahi ya wananchi na wakazi wa Handeni. Wananchi wapo
mashakani.
Serikali inashindwa nini kuchukua hatua? Serikali hii sikivu
inasubiri damu kumwagika? Kila uchao wananchi wanalalamika. Huko kwenye
mabaraza la ardhi ya Kata ni mtihani mzito.
Kumekuwa na kesi nyingi kiasi kwamba wajumbe hao wanashindwa
kuyatatua, huku kelele za ugumu wa maisha na ukosefu wa weredi katika kuendesha
kesi zenye utata zikiwagubika.
Hii ni hatari kubwa. Wakati wowote damu itamwagika Handeni.
Wakati wowote wananchi watatoana roho. Hii ni kwa sababu viongozi wao wamekosa
busara.
Viongozi wao wamekuwa wachumia tumbo. Wameona kwenye migogoro
ya ardhi ndio mahali wanapoweza kuvuna fedha chafu kutoka kwa walalamikaji au
walalamikiwa.
Wakati hayo yakiendelea kutokea, wananchi nao wameanza
kujiandaa kwa heri au kwa shari. Wameanza kunoa silaha zao, wakiamini kuwa
yatakapotokea machafuko waweze kujihami.
Vijana wanaharakati wamekuwa wakishawishiana namna bora ya
kujihami dhidi ya kadhia ya ardhi. Swali la kujiuliza, unawezaje kumiliki heka
100 wakati wananchi wenyewe hawana hata robo heka kwa ajili ya kulima?
Je, muhutsari wake unasemaje? Sheria gani imeruhusu kutoa
ardhi kubwa kwa mtu bila kuangalia kitu wanachoweza kunufaika wananchi katika
eneo hilo? Huu ni wizi na ufisadi.
Ni wakati wa wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao wa
vijiji kupambana usiku au mchana kuzikomboa ardhi zao. Waanze kuwanyang’aanya
wale wote wenye ardhi inayozidi heka 50 na waliopewa bila kufuata sheria.
Watu hao wapo wengi mno. Wamekwenda vijijini na visenti vyao
kwa ajili ya kuwarubuni
wakulima na viongozi wa vijiji ambao mwisho wa siku
wametoa haki zao kwa matapeli hao.
Hii haiwezi kukubalika. Wananchi wasikubali kupoteza haki zao
za msingi, kama ardhi ambayo ndiyo inayoweza kuwapatia mwangaza wa kimaisha na
kiuchumi.
Haiwezekani kundi kubwa la wananchi likose mahala kwa kulima,
wakati mtu mmoja ana heka zaidi ya 100. Mbaya zaidi amezipata kiwizi wizi,
akishirikiana na viongozi wa vijiji wasiokuwa waaminifu.
Ni wakati huu wa Mkuu mpya wa Wilaya ya Handeni, Husna Rajab,
akaliangalia suala hilo kwa mapana yake. Hatuwezi kulalamikia ugumu wa maisha
kwa wananchi wetu, wakati fursa zinazotoa ajira kama kilimo hazifanyiwi kazi
kutokana na nguvu kazi kubwa kukosa eneo la kulima.
Tunaweza kupiga soga sana. Tunaweza kulala katika majumba na
ofisi za umma, lakini lazima tufahamu kwamba damu inaweza kumwagika wakati
wowote, chanzo kikiwa ni migogoro ya ardhi isiyopatiwa ufumbuzi na
inayochochewa na viongozi wezi, watendaji mafisadi waliokubali migogoro iwe
njia ya kuwapatia rushwa kubwa na ndogo kwa manufaa yao binafsi.
+255712053949
No comments:
Post a Comment