https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Wednesday, March 11, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Aveva angalia jahazi lako lisizame

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATU wana kumbukumbu. Unapowaahidi jambo, hakika watakuja kukuuliza pale wanapohisi halijafanyiwa kazi. Na wasipokuuliza, bado haitakuwa sababu ya kutokuchukia.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Simba uliofanyika mwaka jana, Rais wa sasa wa Klabu ya Simba, Evance Aveva, aliwaahidi wanachama na mashabiki wa timu hiyo mambo mengi, ukiwamo ushindi kila kila mechi.

Matokeo ya timu yanaonekana ni ya kusua sua. Na wadau wa mpira wa miguu wanajua fika, haiwezekani timu ikashinda kila mechi, huenda ilikuwa kampeni tu ili aweze kupata urais.

Ukiacha hilo la ushindi kwa kila mechi, bado Aveva akawa na ahadi nyingi, hususan ile ya kujenga uwanja, kuwa na vitega uchumi vyake pamoja na kuwa na taratibu nzuri zitakazowafanya wawike Kimataifa.

Na hapa ndipo ninaposhindwa kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu sioni juhudi za dhati za kuipatia mafanikio timu hii kongwe iliyoanzishwa mwaka 1936, mwaka mmoja baada ya kuanzishwa Yanga SC.

Ingawa naweza kusema nyingi zilizotolewa na Aveva zilikuwa kampeni tu, lakini ahadi hizo ni kama kumbukumbu ya wanachama wake. Kesho watamuuliza na pengine kumtusi mchana na usiku.
Ukiacha matokeo dhidi ya mtani wao wa jadi Yanga, Simba bado haina mfumo mzuri unaoiwezesha kujiandaa kikamilifu ili wapate njia ya kushiriki michuano ya Kimataifa.

Utaratibu wa kutimua timua makocha umeendelea kuwatafuna. Katika Mkutano wa dharula wa wanachama wake, Aveva aliwaambia wanachama wake matokeo mabaya zaidi yametokana na kumfukuza kocha wao Mzambia, Patrick Phiri.

Wakati wanamfukuza hawajajua kuwa kocha atakayeletwa atakuwa mpya kwa kila kitu, hususan kwa wachezaji wake? Ni bora sasa klabu ya Simba ikaendeshwa kisasa, kama alivyoahidi Aveva.

Kwa bahati mbaya kumekuwa na taarifa mbaya za misigano ya viongozi kwa viongozi jambo linaloweza kuiweka Simba katika nafasi mbaya Kitaifa na Kimataifa. Simba ni timu kubwa na kongwe.

Simba pia ni timu inayofahamika kwa ubora wake, hivyo lazima viongozi wafahamu wajibu wao na ahadi zao kwa wanachama wao wakati wanaomba kura ya kuitumikia klabu hiyo.

Haina haja ya kuweka nguvu kubwa kwa mechi moja ya mtani wa jadi, wakati timu haina mipango ya kutafuta mafanikio makubwa, hata yale ya kuunda wachezaji wazuri wanaoweza kuuzwa kwa timu kubwa ndani na nje ya nchi, kama ilivyokuwa kwa Mbwana Samatta, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya TP Mazembe ya Kongo.

Huo ndio mpango wenye dira na tija. Kinyume cha hapo, hakuna jambo litakaloiendeleza Simba zaidi ya porojo na ahadi hewa.
Tuonane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
0712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...