Na Kambi Mbwaana, Dar es Salaam
NAJUA kuifunga Simba au Yanga ni ujiko mkubwa. Kila mtu
anafahamu hivyo, ndio maana timu ndogo zinapigwa kila mechi wanapokutana
wenyewe, ila inapoingia uwanjani kucheza na Simba au Yanga, wanajikaza.
Wanajikaza kiasi kwamba mara kadhaa hushinda au wakishindwa
wanalazimishwa sare na timu hizo kongwe na vigogo Tanzania Bara. Hii siwezi
kuvumilia.
Ukiacha matokeo ya mechi ya Yanga na Mgambo iliyochezwa Jumamosi
katika Uwanja wa Mkwakwani, jijni Tanga, Wagosi wa Kaya hao wanaotokea Kabuku,
wilayani Handeni, walikuwa na pointi 24 na kushika nafasi ya sita katika
msimamo wa Ligi ya Tanzania Bara.
Katika mechi yao na Simba, Mgambo waliweza kucheza soka safi
na la kuvutia kiasi ambacho kiliwapatia ushind wa mabao 2-0. Matokeo hayo
yalikuwa machungu kwa mashabiki wa Simba. Hii ni kwa sababu yaliwaweka katika
nafasi mbaya kuelekea kutwaa ubingwa wa Bara.
Kama hivi ndivyo, naumiza kichwa kwanini Mgambo isiwe
inacheza soka safi la kuvutia hata inapokutana na timu ndogo? Kwanini timu zote
zisiwe zinacheza soka lao safi ili ligi izidi kuwa na msisimko?
Sio kama nimeumia kuona Mgambo wameshinda mbele ya Simba, ila
ni kuchukizwa na mfumo wa soka letu kuona timu zinajikaza pale wanapokutana na
timu kubwa za Simba na Yanga.
Timu kubwa au kongwe ni Simba na Yanga.Ni sawa na pointi 12
kama timu hiyo itashinda nyumbani na ugenini kwa mechi zote watakazokutana na
wakongwe hao kwa msimu mmoja wa Ligi.
Hii ni kuonyesha kwamba matokeo hayo hayawezi kuipa ubingwa
timu husika kwa kushinda mbele ya Simba na Yanga tu. Ni wazi timu hizi
zinapaswa kupata mafunzo mazuri kutoka kwa makocha wao. Waonyeshe soka safi kwa
timu zote ili walau zikuze kiwango chao
kama si kutwaa ubingwa wa Bara.
Lakini kufungwa ovyo na mwisho kujifariji na pointi tatu za
Simba au Yanga ni kujiharibia tu, maana inaweza kuwa dalili mbaya za kudumaa au
hata kushuka daraja. Huu ni ushauri tu.
Ieleweke kuwa napenda maendeleo ya
mpira wa miguu Tanzania, huku nikiwa siamini kuwa kucheza mechi za wakongwe tu
na kwingine kusua sua ni kujilemeza.
Huo ndio ukweli wa mambo. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia,
maana ndio timu ndogo zifanye vizuri, lakini si kwa mechi za wakongwe tu. Kuna
faida gani kumfunga Simba au Yanga na baadae timu inashuka daraja?
Au ndio kufungwa tunafungwa japo chenga twawala?
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment