Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KIKAO cha
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania
kilichoketi jumanne ya tarehe 24, Machi 2015 jijini Dar es salaam, kimepitia
taarifa mbalimbali za michezo iliyochezwa na kutoa adhabu kwa wachezaji na
vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom.
Katika
mechi namba 107 iliyowakutanisha wenyeji Ndanda FC dhidi ya Coastal Unioni,
klabu ya Ndanda imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni
ya 42(1) ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na washabiki wake kumrushia
chupa za maji mwamuzi msaidizi Anold Bugado.
Mechi
namba 108 iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, (Stand United dhidi
Simba SC), wenyeji timu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki
tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(8) kutokana na timu yake kuchelewa kufika
uwanjani kwa dakika ishirini.
Mchezo
namba 117 uliozikutanisha Simba SC dhidi ya Yanga SC kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam, timu ya Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu)
kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kukataa kuingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo.
Nayo
klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni
ya 42(11) baada ya timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano kwenye mchezo dhidi
ya Simba SC, huku mshambualiji wake Dany Mrwanda akipigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(12) kwa kutopeana mikono na
wachezaji wa timu hiyo.
Mchezaji
Haruna Niyonzima wa Yanga amepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu
wa Kanuni ya 37(f) kwa kupiga teke meza ya mwamuzi wa akiba baada
ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Suala la mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe
kumshika korodani beki wa Simba SC Murshid Juuko limepelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu.
Kipa
wa timu ya Simba SC, Ivo Mapunda amepewa onyo kwa kufunika tangazo la mdhamini
wa Ligi Kuu (Vodacom) kwa kutumia taulo lake wakati wa mechi dhidi ya
Yanga, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake iwapo atarudia kufanya
tukio la aina hiyo.
Nao
wachezaji Salum Abubakar wa Azam FC na Richard Maranya wa JKT Ruvu wamepigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kila mmoja na kusimamishwa mechi tatu kwa
mujibu wa Kanuni ya 37(3) kwa kupigana uwanjani kwenye mechi namba 123 ambapo
walitolewa nje kwa kadi nyekundu.
Klabu
ya Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni
ya 14(9) baada ya timu yake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo
kwenye mchezo namba 130 dhidi ya Young Africans uliofanyika kwenye Uwanja wa
Taifa.
Mechi
namba 132 iliyozikutanisha Azam na Ndanda SC kwenye uwanja wa Chamazi, klabu ya
Ndanda imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1)
baada ya washabiki wake kuwamwagia maji na kuwarushia chupa za maji washabiki
wa Azam.
Aidha
klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa
Kanuni ya 14(8) kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi namba 134 dhidi ya
timu ya Mbeya City, pia imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa
mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo
kwenye mchezo huo.
Kiongozi
wa Stand United, Muhibu Kanu amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya
kuondolewa kwenye benchi na mwamuzi wa mchezo dhidi ya Mbeya City kutokana na
kutumia lugha ya kuhamasisha vurugu kwa timu yake na kupinga uamuzi wa refarii.
Katika
mchezo namba 135 uliochezwa jijini Tanga na kuwakutanisha wenyeji Mgambo
Shooting dhidi ya Yanga SC, Yanga SC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano)
kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuvamia uwanja baada
ya mechi namba 135 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
No comments:
Post a Comment