https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, March 15, 2015

Nashukuru kwa kuiona siku ya kuzaliwa, vijana tuchape kazi, tuache kulalamika ovyo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Jana ilikuwa ni Machi 14 mwaka 2015. Machi 14 ni siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwangu baada ya kutimiza miaka kadhaa tangu kuzaliwa kwangu. Ingawa nafurahia kuzaliwa huko, lakini hudhuni inamea nifikiriapo kila ninachokifanya leo au nitakachofanya kesho nikiwa na uhai, hakitaaweza kuonwa na baba yangu, mzee Mbwana Hemed Masoud, maarufu kama Mzee Kajembe.

Kambi Mbwana, pichani
Mzee huyo aliyefanikisha uwapo wangu duniani akishirikiana na mwanamke jasiri na mkarimu na mwenye upendo kwa familia yake na jamii kwa ujumla, Bi Fatuma Omary, alifariki mwaka 2012 katika Hospitali ya Wilaya Korogwe (Magunga) na kuzikwa kijijini kwake Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Lala pema peponi baba yangu. Baada ya kusema hayo, nachukua fursa hii kuwatakia kheri wote walionitakia kheri ya kuzaliwa hiyo jana. Nimekuwa mwenye furaha kubwa nionapo jamaii yangu inaniheshimu na kunithamini. Kila nionapo mtu anayeguswa na mwenendo wangu, hakika nafarijika kupita kiasi.
Mdau wa Maendeleo na mmiliki wa mtandao wa Handeni Kwetu, akizungumza jambo katika moja ya matukio aliyoandaa likiwamo la NSSF Handeni Kwetu lilofanyika mwishoni mwa mwaka jana, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Nimekuwa nikifanya mambo mengi kwa ajili ya kuitumikia jamii na Tanzania kwa ujumla. Kama ilivyokuwa kawaida ya mambo mazuri hayakosi changamoto, nimekuwa nikitatizwa na baadhi ya mambo ambayo mwisho wa siku yanakuwa kama funzo kwangu.

Funzo hilo ni kuona naendelea kuishi kwa kufanya juhudi zote kama nilivyopanga bila kuona wangapi wananikubali na wangapi wananichukia. Nimeamua pia kukaza msuri kuanzisha vitu ambavyo ni active vyenye mchango na jamii yangu.

Mwaka 2013 nilianzisha tamasha la Handeni Kwetu linalofanyika kila mwisho wa mwaka, yani Desemba. Mwaka huu likifanyika litakuwa ni mara ya tatu mfululizo. Aidha, sehemu ya bajeti ya tamasha hilo kwa mwaka jana, pia lilitumika kugharamia safari vijijini na baadhi ya viongozi wa taasisi ya Handeni Kwetu Foundation, ambayo ni miongoni mwa waasisi kwa nia ya kuikomboa jamii ya Handeni na Tanzania kwa ujumla.
Nashukuru kwa ushirikiano mkubwa ninaopata kutoka kwa wana jamii yangu, wakiwamo wa wilayani Handeni, mkoani Tanga, bila kusahau Watanzania wote. Nawashukuru viongozi wa serikali wanaoshirikiana na mimi. Nawashukuru pia viongozi wa vyama vya siasa, mashirika na taasisi zote za serikali na zisizokuwa za kiserikali.

Kwa heshima ya kipekee niwashukuru Mfuko wa Hifadhi ya jamii (NSSF) na Taasisi ya  Kifedha ya Bayport Financial Services kwa kuniunga mkono katika mambo mengi, hususan tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2015.

Nawashukuru pia ndugu zangu waandishi wa habari, vyombo vya habari kama vile radio, magazeti, televisheni na bloggers ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakinisaidia mno kutangaza kile ninachofanya au ninachokusudia kukifanya.

Wakati naendelea kusema hayo, naomba Watanzania wenzangu tujiandikishe kwa wingi kwenye daftari la kudumu la kupiga kura ili tupate haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Kujiandikisha kwetu pia kutatupa nafasi ya kushiriki katika kuipigia kura Katiba Pendekezwa.

Mchakato huo wa kura ni muhimu kwa mustakabali wan chi yetu. Kamwe asitokee mtu wa kutuhadaa kwamba tuache kuipigia kura Katiba wala kuacha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao. Kupiga kura ni haki ya msingi kwa wananchi wote.

Hata kama huitaki Katiba hiyo au mgombea wa udiwani, mbunge na urais, ila dawa si kususa bali kupiga kura ya kukataa kama sheria zinavyosema. Najua wapo baadhi ya wanasiasa wanapita pita kutupumbaza kwamba Katiba haina tija, kwamba haijakamilika na kuongea kila wapendacho wao. Mimi nasema Katiba yetu pendekezwa ni nzuri na imezingatia mambo yote yenye tija kwa Watanzania wote.

Kwa wale ambao hawajafanikiwa kuisoma, watafute namna ya  kuisoma ili wajiridhishe kabla ya kuipigia kura ya ndio au hapana. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr Jakaya Mrisho Kikwete atakumbukwa kwa kitendo cha kufanya bidii kubwa kuhakikisha kwamba mchakato huo wa Katiba mpya unafanyika kwa mafanikio.

Pia atakumbukwa kwa kufanikisha mambo mengi mazuri ndani ya utawala wake kama vile shule za Kata kuendelezwa na kujengwa maabara, barabara, vituo vya afya na Hospitali nyingi kujengwa bila kusahau miradi mikubwa kuanzishwa itakayokuwa na tija kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naamini mambo mengi yaliyoanzia kwenye kipindi cha uongozi wake yataendelezwa hata pale atakapofikia mwisho wa utawala wake. Namaliza kwa kuwaomba tena ushirikiano ndugu zangu Watanzania juu ya mambo yote nifanyayo na nitakayopenda kuyafanya siku hadi siku kwa kipindi cha mwaka huu na miaka mingine ijayo.

Najua ninayo nafasi kubwa ya kuifanyia mambo mema nchi hii. Najua pia ninayo kiu na shauku ya kuona akili yangu, kichwa change na mikono yangu inachangia kwa kiasi kikubwa kuwapatia nuru wengine walionizunguuka.

Itakapotokea napatwa na tatizo, naomba ndugu zangu tuendelee kushirikiana kwa kuniombea, kunisaidia na sio kunililia kwa naamna yoyote ile. Pamoja na changamoto kadhaa ninazokutana nazo hususan za baadhi ya viongozi wasiopenda kuona nafanya mambo makubwa kwenye nchi hii, lakini kwa dua zenu, utu wenu, ushirikiano wenu naamini kwa pamoja tutaweza kumpiga adui yetu huyo na kuambulia aibu. Nawashukuru wote mlionitakia heri ya kuzaliwa kwangu na hata wale walioshindwa kufanya hivyo mmewakilishwa na wengine. Nitashindwa kuwataja kwa majina yenu wote, maana ni wengi mlionitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yangu na kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha mapenzi yenu kwangu. Asanteni sana. Sina cha kuwalipa, ila Mungu pekee ndiye wa kuwalipa.

Mwisho kabisa naomba tufanye kazi kwa bidii kujenga uchumi wa nchi yetu. Tuache kulalamika bila sababu za msingi. Tutumie fursa yoyote hata kama iwe ndogo kwa ajili ya kufanikisha maendeleo yetu na ya nchi yetu Tanzania. Tukifanya hivyo, hakika tutapiga hatua na kujimudu kiuchumi jambo litakalotufanya tushindwe kutumika vibaya kwa wanasiasa wanao

Mungu naomba unisaidie; tusaidie pia kwa kuilinda nchi yetu iwe ya amani na utulivu. Mpe afya njema rais wetu ili amalize kipindi chake kwa amani.
+255712053949
+255753806087


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...