Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA walioanza kufuatilia mpira wa miguu Tanzania, hakika
watakumbuka kile kikosi cha Mabingwa wa zamani wa Tanzania Bara, Simba SC,
katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003. Kikosi imara kilichowatoa timu ngumu
ya Zamalek na hatimae Watanzania hao kuingia hatua ya robo fainali na
kushangaza wengi.
Marehemu Christopher Alex Massawe enzi za uhai wake.
Kabla ya kuwatoa Zamalek, timu nyingi za Tanzania, ikiwamo
Yanga walikuwa wakishindwa kuzitoa timu
za Misri. Kila walipokutana inakuwa mwisho wao. Ilishazoeleka, inapotokea Yanga
au Simba wanacheza na Al Ahly, Zamalek na nyinginezo za huko tunauona mwisho
wetu.
Kwa mwaka huo ikawa tofauti. Na walioifanya Simba ifuzu
hatua hiyo ngumu ni mchezaji Christopher Alex Massawe, ambaye amefariki wiki
iliyopita mjini Dodoma, alipokuwa akiishi nyumbani kwa mama yake na kuugua kwa
muda mrefu.
Massawe aliugua sana kabla ya kufariki. Na kuugua kote huko
hakuna msaada wowote uliomfikia mchezaji huyo kutoka kwa timu yake ya Simba
aliyoichezea kwa mapenzi makubwa. Na Massawe alishawahi kulalamikia sana hilo,
akiomba viongozi na wadau wa
Simba wamkumbuke hata kwa macho tu ili wamfariji.
Hakika siwezi kuvumilia ninaposhuhudia nyota wa mpira wa
Tanzania wanavyoishi kimasikini na wasivyokumbukwa kwa mazuri yao. Hivi kweli
Simba yenye neema ya rasilimali wa watu na fedha pia, wanashindwa kuwakirimu
wachezaji wao?
Hii inakuwaje? Kwa wachezaji kama akina Massawe, Emmanuel
Gabriel, Juma Kaseja, Selaman Matola na wengineo wote waliokuwa kwenye Simba
ile kiboko ya wa Misri ilipaswa waangaliwe kwa jicho pana ili walau kuwalipa
fadhira zao.
Kwa bahati mbaya wachezaji wa enzi hizo walicheza kwa
mapenzi makubwa na hakukuwa na pesa nyingi. Ni tofauti na wachezaji wa leo
wanaoogelea kwenye Mamilioni ya fedha. Enzi hizo wachezaji walijisikia faraja
tu kuichezea Simba, Yanga au timu ya Taifa (Taifa Stars).
Kama tunashindwa kuwahudumia wakongwe japo kwa uchache tu
tunaweza kuwa na maendeleo kwenye mpira wa miguu Tanzania? Simba imejaza
wanachama, wapenzi na mashabiki wanaoweza kulia timu yao inapofungwa.
Je,
anajua kulia kwake kunatokana na jasho na nguvu za wachezaji wanaopambania
ushindi uwanjani?
Lakini pia wanajua kuwa mara zote hao waliopambania Simba
hasa katika michuano mikubwa, yenye mvuto wameishia kutupwa kama mizoga?
Nakumbuka Massawe kilio chake cha mwisho ilikuwa ni kuwaomba Simba wamtembelee
na kumfariji.
Aliamini viongozi wake na wadau wakimtembelea walau wanaweza
hata kumnunulia dawa ya kutuliza maumivu, lakini sivyo. Hii inatia kichefuchefu.
Na huenda machozi ya akina Massawe ni bakora ya kuiadhibu klabu ya Simba.
Andiko hili halina faida kwa Massawe kwasababu amekufa akiwa
hajamuona hata huyo Matola, ambaye mwaka
2003 walipoitoa Zamalek alikuwa nahodha wao. Viongozi wa Simba na klabu
zote zinapaswa kuweka utaratibu wa kuwatunza wakongwe wao. Ndio ubinadamu.
Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia, maana jambo hili linakera.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment