Maelezo ya Ndugu Zitto Kabwe
aliyoyatoa katika Mkutano na Waandishi wa Habari kufuatia Kung’atuka Ubunge na
Kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo Jumapili, 22 Machi 2015, Serena Hoteli, Dar
es Salaam.
Ndugu Waandishi wa habari, wanachama
na wapenzi wa ACT-Wazalendo na wote mliohudhuria mkutano huu, Kama mnavyojua
siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu ya mwisho kuhudhuria
bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma.
Zitto Kabwe wa pili kutoka kushoto akifuatiwa na Afande Sele mwenye rasta wakionyesha kadi zao za ACT leo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kung’atuka ubunge kufuatia
kukoma uanachama wangu wa chama nilichotumia kuingia Bungeni, wengi mliniuliza
‘what is next?’.
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama
ambavyo baadhi yenu tayari mnajua, kwamba jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi
2015 nilijiunga rasmi na Chama cha ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na
Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa ni moja kati ya siku muhimu kabisa
katika maisha yangu ya kisiasa. Na kwa leo kwa kweli nisingependa nizungumzie
mgogoro uliokuwepo kati yangu na viongozi wangu wa chama cha zamani wala kile
kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua, yameandikwa sana na yameshapita. Sasa
ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame Nkrumah alipata kusema "forward
ever, backward never". Na kama nilivyosema Bungeni, yaliyopita si ndwele,
tugange yajayo. Kwa hiyo leo nitazungumzia uanachama wangu katika chama changu
kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli
wengi watakuwa wanajiuliza kwa nini nijiunge na chama kipya ambacho
kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine wanachama wake bado wanajaa katika
kiganja cha mkono?
Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona
kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka
yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu
kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo
msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na
ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni
chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika
Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi
taifa.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa
sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na
maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo
wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi
ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba
viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii.
Uadilifu ni nguzo muhimu katika
kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu
yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo
ninaamini kwamba ni moyo wa utumishi wa umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi
kumi ya ACT-Wazalendo, uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi
hiyo.
Uwazi ni sehemu ya jina la chama
hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba sitojiona mgeni katika chama hiki.
Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na katika utumishi wa umma. Nimejiunga na
ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii,
umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo.
Hakuna namna nchi yetu na wananchi
watapiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa
kuzingatia umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali
za Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa
sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa
taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi
iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa
bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana,
wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja.
Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi
yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi,
wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na
katika kuondoa umaskini. Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu,
afya, hifadhi ya jamii, na ajira.
Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu
namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia
sehemu yake. Mwezi Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alipokea maandamano ya
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu. Maandamano yale yalichochewa
na kasi kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya viongozi (wabenzi).
Mwalimu alifoka kwa kuuliza “
Tunajenga nchi ya namna gani”? Hatimaye Azimio la Arusha likatangazwa. Chama
hiki kipya kimeanzishwa katika mazingira yale yale ya mwaka 1966. Ni wakati wa
kujiuliza na kupata majawabu ya aina ya nchi tunayojenga. Sisi ACT – Wazalendo
tumeona jawabu ni kurudi kwenye misingi. Waingereza wanasema ‘back to the
future’ Let the new beginning begin.
Ahsante sana kwa kunisikiliza. Zitto
Zubeir Kabwe Dar es Salaam, 22 Machi 2015.
No comments:
Post a Comment