Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
WANANCHI na wakazi wa Kata ya Misima, wilayani Handeni mkoani
Tanga, wameombwa kutokuwa na wasiwasi na hatua ya kuingizwa kwenye Halmashauri
ya mji kwakuwa mpango huo sio mbaya kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni Thomas Mzinga, akiwa kwenye moja ya matukio ya kijamii wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Handeni, Thomas Mzinga, alipozungumza na Mtandao wa
Handeni Kwetu, juu ya hatua mbalimbali za kuunganisha eneo hilo na Handeni
Mjini.
Alisema mchakato wote wa kuunganisha mji huo na Kata ya
Misima ulifuata sheria zote, huku akisema woga wa wananchi unatokana na hoja
dhaifu kuwa viwanja vyao vitauzwa na serikali.
“Sio kweli kama kuingia kwenye Halmashauri ya Mji basi
viwanja vyote na mashamba yaliyokuwapo yatauzwa ovyo na watendaji wa serikali,
maana hiyo si sababu ya kupanua mji wetu.
“Wananchi wameaminishwa uongo ili suala hilo lisiwe na
mafanikio, hivyo tunaamini tutaendelea kuhamasisha wananchi wetu na Watanzania
kwa ujumla ili kwenye mambo ya kimaendeleo tufanye kama inavyopangwa na
viongozi wa serikali kwa ujumla wake,” alisema Mzinga.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hatua ya kuunganisha eneo la
Misima katika Halmashauri ya Mji ni kuweka mikakati kabambe ya kuupanua mji
wote wa Handeni na kusogeza pia maendeleo karibu na wananchi.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa, wananchi wa Misima wamekuwa
wakivutana na viongozi wa serikali ya wilaya ya Handeni wakigoma kuingizwa
kwenye Halmashauri ya Mji kwa madai kuwa bado mapema na kijiji hicho kipo mbali
kabisa, huku wakiona kuwa huenda ni mipango ya waheshimiwa hao kusogea karibu
ili kuteka mashamba yao.
No comments:
Post a Comment