Na Absalom Kibanda, pichani na haya ndio maoni yake.
MHESHIMIWA
Rais wangu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa salamu ya utii
inayotambua na kuheshimu kwa dhati mamlaka makubwa na ya juu uliyonayo
kama mkuu wa taifa letu ambalo mazingira yake ya leo yanapaswa yawe
wenye mwelekeo wa kushangilia kama si kujivunia uhuru ambao tuliupata
mwaka 1961 na 1964 kwa kutegemea upande tulipo katika muungano wetu.
Mheshimiwa
Rais, najisikia faraja iliyojaa majonzi moyoni kupata fursa hii adhimu
kukuandikia waraka ambao msukumo wake unasukwasukwa na dhamira njema
kabisa ambayo aghalabu kiini chake si kingine bali mapenzi mema kwa nchi
na viongozi wetu wote.
Ni
faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali na adimu ya kuteta na kiongozi
wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa kujiamini, huku nikiwa na uchungu pia
kwa sababu ujumbe ambao unabebwa na waraka huu ni wa kuumiza sana
nafsi, roho, akili na mwili.
Mheshimiwa
Rais, wewe ni kiongozi wa Watanzania wote tukiwamo sisi ambao baadhi ya
wateule wako wameamua kwa sababu wanazozijua wao na wakati mwingine
wakidai kwa maelekezo ya wakuu wao kutujengea taswira zinazotufanya
tuonekane tu watu wa ovyo na kada ya wanajamii waliokosa utu na eti
tunaopaswa kufundishwa hekima na somo la uzalendo ambalo limekuwa sehemu
ya makuzi yetu nyumbani, shuleni, jeshini na ndani ya jamii.
Kabla
sijafikisha ujumbe ambao nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito moyoni,
napenda kwanza kupitia fursa hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema na neema kwa kuniwezesha kuuona mwanga wa siku hii
njema ya leo ambayo kama si kwa kudra na mapenzi yake, yumkini
ingeongeza hesabu za siku ambazo kiwiliwili changu kingekuwa katika
kaburi la sahau ambalo kila kukicha linameza roho za makumi kama si
mamia ya Watanzania wasio na hatia wanaopoteza maisha kutokana na kazi
za mikono ya majahili, miungu watu waliojitwalia haki ya kuchagua aina
ya maisha na vifo vya watu wengine.
Baada
ya hilo, kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wenzangu ambao hawana
fursa ya kuwasiliana nawe kwa njia kama hii ya waraka niliyoitumia,
napenda kutumia pia wasaa huu kukushukuru wewe binafsi kwa namna
ulivyojitoa usiku na mchana pasipo kuchoka kuliongoza taifa hili katika
mazingira magumu yaliyojaa changamoto za kila namna ambazo wakati
mwingine sina shaka hata kidogo kwamba zimekuwa zikikunyima raha na
kukosa usingizi.
Wakati
nikikuandikia ujumbe huu, picha na taswira yako inayonijia ni ile ya
Machi 8, mwaka huu siku uliponitembelea kando ya kitanda nilichokuwa
nimelazwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesburg kule Afrika Kusini
ikiwa ni siku mbili tangu nilipovamiwa, nikajeruhiwa na kupewa ulemavu
na majahili ambao hadi leo hii wameweza kuukwepa mkono mrefu wa vyombo
vya dola unavyoviongoza.
Mheshimiwa
Rais, japo nilikuwa nina maumivu makali na machungu ya kupoteza jicho,
kidole na kupasuliwa kwa mifupa ipatayo minane katika paji langu la uso,
ukiacha taya lililoachanishwa kikatili na watesi wangu wale, bado
ninaweza kukumbuka kwa ufasaha namna ulivyozungumza nami ukionyesha
jinsi ulivyokuwa ukiguswa na kuumizwa sana na tukio lile.
Ni
jambo la bahati mbaya sana kwamba, tangu niliporejea nchini miezi sita
iliyopita sijapata kukutana nawe ana kwa ana ingawa nilipata fursa ya
kukutumia salamu zangu za shukrani kupitia kwa marafiki zako kadhaa
akiwamo msaidizi na mshauri wako nambari moja, Makamu wa Rais, Dk.
Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote wakati nikiwa katika matibabu
nchini Afrika Kusini na hata baada ya kurejea nchini, alionekana kuwa
mtu wa kukosa amani kabisa pasipo kunijulia hali kwa njia ama ya simu,
wasaidizi wake na mwisho kwa kuonana nami ana kwa ana.
Nayarejea
haya yote huku nikitambua kwamba, wakati ninapoandika waraka huu ndiyo
kwanza umerejea kutoka nchini Marekani ambako ulikwenda kuchunguzwa afya
yako ambayo nina matumaini makubwa ni njema hasa kwa kuzingatia ukweli
kuwa, ulikwenda huko siku chache tu baada ya kuiwakilisha vyema nchi
yetu katika msiba mzito wa shujaa wa mapambano ya ubaguzi wa rangi
nchini Afrika Kusini, mzee wetu, Nelson Mandela.
Ninapoyatafakari
matibabu ghali niliyopata nchini Afrika Kusini kwa msaada wa mwajiri
wangu na safari yako nchini Marekani, vinanikumbusha swali la mmoja wa
wasaidizi wangu hapa ofisini aliyetaka kujua ni sababu gani hasa ambazo
zimekuwa zikisababisha wasomi na viongozi wetu kuchunguzwa na kutibiwa
katika hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa kwa Madiba ambaye kwa
nyakati zote tangu afya yake ianze kumtatiza alikuwa akipata matibabu
huko huko kwao Afrika Kusini?
Niseme
kweli, japo nilikuwa na jibu au majibu ya swali lake, sikuwa na maelezo
ya kutosheleza yaliyokuwa na mwelekeo wa kukata kiu ya swali lake,
ingawa kwa kupapasa nilifanya kila juhudi kuutetea utaifa wangu na
viongozi wake ilhali miye mwenyewe nikiendelea kukosa raha kwa namna
nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo yalikuwa yakionyesha hali ya kuukubali
unyonge, kukiri ufukara, kuficha udhaifu wetu kama taifa na kutetea
makosa ambayo aghalab ninyi viongozi wetu na wale wa kabla yenu mngeweza
kuwa watu mliostahili kuwa na majibu halisi.
Rais
wangu, swali na majibu vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali
mengi mengine na moja ya maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia
hata tukafikia hatua ya kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu
waliokata tamaa, wanaoteswa na ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina ya
kero na karaha zinazozonga maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa
Rais, hali hiyo ilinipeleka moja kwa moja nchini Afrika Kusini na
hususan katika Hospitali ya Milpark ambako huko ndiko miye mwenyewe na
Watanzania wenzangu wengine tulikonusuru maisha yetu, huku baadhi kama
ilivyo kwa Dk. Sengondo Mvungi wakipoteza maisha yao baada ya kukimbizwa
huko.
Mheshimiwa
Rais, naomba unisamehe kwa kulisema hili nitakaloliandika hapa kwamba,
jibu nililolipata haraka haraka kuwa moja ya chagizo la matukio ya namna
hii kutokea, halikuwa jingine bali ni kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa
viongozi wetu hususan wale tuliowapa dhamana ya kuongoza sekta kadhaa
nyeti kama ya afya na ustawi wa jamii.
Ushahidi
wa kupwaya huko kwa viongozi hususan wale walio chini yako, ndiko huko
huko ambako kumedhihirika pia wiki iliyopita bungeni Dodoma, ambako
tulishuhudia zahama nyingine iliyowang’oa madarakani mawaziri wako
muhimu wanne kwa sababu kama hizo hizo za mkwamo wao au watendaji wa
chini yao katika kusimamia ipasavyo na kuchukua hatua kwa wakati, kila
yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo wanayoyaongoza.
Nitakuwa
sijaitendea haki nafsi yangu, mheshimiwa Rais iwapo nitaficha shauku ya
moyo wangu ambayo ilikwenda sambamba na tukio lile la Dodoma
lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao anguko lao linaweza likaelezwa
kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia msamiati ulioutumia wewe mwenyewe
kwa mara ya kwanza ulipozungumzia tukio la kujiuzulu kwa waziri wako
mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.
Haja
ya moyo wangu, nikiwa mhariri, mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) na mdadisi wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa kuona
anguko la namna hiyo hiyo likimfika Waziri wa Habari ambaye
amethibitisha pasipo na shaka kuwa pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya
Falsafa (Phd), ni kiongozi asiyejua anachofanya kwa kiwango cha kuwa mtu
ambaye vichwa vya watu wengine ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.
Nilitamani
afikwe na zahama hiyo si kwa sababu ya kuwa na hasira au kumchuria
mabaya, bali kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye bado
anasongwa na matongotongo ya mfumo wa kibabe wa zama za magazeti ya
Serikali na yale ya chama tawala, ambayo yanalazimika kuandika yale tu
yanayofurahisha nyoyo na akili za watawala.
Mheshimiwa
Rais, ingawa natambua na kuheshimu ukweli mchungu kwamba, suala la nani
awe waziri na nani asiwe ni jambo la wewe mwenyewe kupenda na kuchagua
na kwamba ulishasema mapema kabisa mbele yetu kwamba urais wako hauna
ubia, bado naamini pia kwamba, wewe ni mtu msikivu na mkweli uliye
tayari kusikia na kustahimili mambo mengi machungu unayokabiliana nayo
kila siku.
Kwa
sababu hiyo, basi napenda kukueleza kwa kuweka kumbukumbu sahihi ili
mbele ya safari kabla na baada ya kumaliza urais wako uje kuyatafakari
na kuukumbuka ushauri huu kwako kwamba, waziri uliyempa dhamana ya kulea
na kuendeleza vyombo vya habari, ni mtu wa kuhofiwa, jeuri, mwenye
kiburi, asiyeshaurika na dikteta asiyekutakia mema wewe binafsi, vyombo
vya habari, serikali yako na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa
rais sijui kama unajua kwamba tangu umteue amefanya kazi na vyombo vya
habari vya umma na hata baada ya sisi kufanya juhudi kubwa ya kuwa
karibu naye kikazi kwa makusudi na kwa ujeuri mkubwa, amekataa wito na
kupuuza maoni na ushauri wetu na kwa namna ya kusikitisha amesikika
akitamba waziwazi kwamba anao uwezo wa kulifungia au kulifutia usajili
gazeti lolote ambalo ataliona linakwenda kinyume cha maadili ya uandishi
wa habari.
Waziri
huyu ambaye alitarajiwa kuwa na silika za kuwa mlezi bora kutokana na
jinsia yake na historia yake ya kupata kuwa mwanaharakati kabla ya
kuingia serikalini, ndiye ambaye mamlaka makubwa uliyomtwisha,
ameyageuza na kuwa mwavuli wa kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye
uthubutu wa kukosoa serikali na kuandika ukweli mchungu ambao
asingependa kuona ukiripotiwa.
Mheshimiwa
Rais, pengine baya zaidi kwa tasnia hii ni kwamba waziri huyo ana
bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa wasaidizi na washauri wake katika sekta
yetu ya habari ambaye naye, hulka zake tangu aingie katika tasnia ya
habari amekuwa ni mtu wa kujipendekeza, kupenda makuu, kuzusha na
kutokuwa na mawazo huru. Huyu si mwingine bali Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (MAELEZO).
Ni
jambo la bahati mbaya kwamba waziri huyu msomi pengine kwa sababu ya
kutojua vyema rekodi na historia ya msaidizi wake huyo, ambaye japokuwa
naye pia ni mteule wako, amejikuta akiwa mhanga wa fikra pandikizi
zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu mahususi unaofanywa na baadhi
ya wateule wako ambao wameshaanza kujipanga kusaka urais baada ya wewe
kustaafu.
Mheshimiwa
Rais, nimelazimika kuyasema yote haya baada ya kula kiapo cha moyoni
huku nikirejea mafunzo tuliyokuwa tukikaririshwa utotoni chini ya imani
ya wana TANU, ambayo hata sisi ambao hatukuwa wanachama wa chama hicho
tulilazimika kuikariri kwa kuitamka kila kukicha; ‘Nitasema kweli daima,
fitina kwangu mwiko.’
Rais
wangu, gazeti la MTANZANIA limerejea tena mitaani. Japokuwa ni rahisi
kuhesabu miezi, napenda kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi mitatu
michungu sana kwetu kihisia na katika hali halisi.
Nitakuwa
mzushi sawa sawa na hao ninaowashangaa leo, iwapo nitasema kulikuwa
hakuna hitilafu au makosa ya kiuandishi ambayo yaliwapa kisingizio cha
mikakati waliyoipanga mapema kabisa, wasaidizi wako hao kwa kulifungia
gazeti letu hili.
Mheshimiwa
Rais, nasema haya kwa sababu ni ukweli ulio bayana kabisa kwamba,
habari zilizoandikwa na kutoa mwanya kwa serikali yako kutuadhibu gazeti
hili, hazikulenga kuchochea na wala hazikuchochea kabisa chuki yoyote
dhidi ya yeyote na mamlaka unazoziongoza kwa namna na kwa njia yoyote
ile.
Siyo
siri hata kidogo, mkurugenzi aliyetangaza uamuzi huo alifanya hivyo
akijua watu wengi hawajui mapito na dhamira yake. Tunajua yeye
alimshauri vibaya waziri na serikali huku akijua vyema kwamba, yuko hapo
alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la watu wenye malengo binafsi
ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati wowote na mahali popote
kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati utakapotaka kuchukua maamuzi
ya haki na kweli ujue undani halisi wa mambo haya.
Leo
hii wakati tukirejea tena sokoni, tayari tumeshasikia kuendelea kuwapo
kwa mikakati ile ile ya kuhakikisha gazeti hili na jingine ambalo
halipendwi na watu hao hao kwa sababu binafsi yakiinaingizwa tena
mtegoni na kufungiwa kifungo kingine kama hiki tulichomaliza au
kinachofanana na kile kilichoifika MwanaHalisi.
Mheshimiwa
Rais, naandika waraka huu nikikumbuka semi zako mbili unazotumia;
‘tunajenga nyumba moja kwanini tugombee fito?’ na ile ya ‘akili za
kuambiwa changanya na zako’ ambazo kwa muktadha wa waraka wangu huu
kwako zinaweza zikawa za msaada sana kwako na pengine kwetu sisi wa
MTANZANIA ambao tunashangilia kurejea mtaani kwa gazeti letu
lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa muda wa siku 90.
Nimelazimika
kukutumia wewe Rais si kwa lengo la kuchosha akili zako au kukupotezea
muda, isipokuwa kwa kutambua hadhi, heshima na mamlaka makubwa uliyonayo
juu ya wateule wako hao ambao wameamua kwa sababu ya jeuri za kimamlaka
walizonazo kuumiza watu na kutupa sifa na majina mabaya tusiyostahili.
Hakika wazungu walikuwa sahihi waliposema ‘power currupts’.
Mheshimiwa
Rais, lingekuwa ni jambo la kheri kwa Serikali na kwa taifa letu zima
iwapo kusudi la kufungia magazeti linalopangwa na wateule wako kuwa
utamaduni wa kudumu, lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema kwako wewe
binafsi, chama chako, Serikali unayoiongoza na nchi yetu kuliko hili la
sasa lenye dhamira ya kufunga watu midomo, kutesa, kuzusha na kuharibu
taswira yetu kama watu binafsi, taasisi na taifa.
Ni
kwa sababu hizo, mheshimiwa Rais ndiyo maana baada ya kusukwasukwa na
moyo na kuumizwa mno kifikra nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi
yangu na haki za maelfu ya Watanzania ambao tunaamini wanahitaji huduma
ya magazeti haya katika kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha, kielimu
na kiufahamu kila kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani
zikiendelea kuongoza sekta yetu.
Mheshimiwa
Rais, siyo siri hata kidogo kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi ya uhuru
wa kikazi na kiwajibikaji wa vyombo vya habari na wanahabari yanaonekana
kutawala kauli na maamuzi ya baadhi ya viongozi na washauri wako kwa
kiwango cha kukushawishi hata wewe binafsi kukubaliana nayo, ukweli ni
kwamba, nyuma ya maneno matamu wanayotumia kutupaka matope, kutujeruhi
na kutupa kila aina ya sifa mbaya kuna ajenda za kutuharibia sisi,
kukuharibia wewe, kukomoa, kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.
Nitakuwa
mhariri nisiyewajibika, iwapo nitakaa kimya ilhali nikijua fika kwamba,
leo hii ndani ya wizara iliyopewa dhamana ya kulea vyombo vya habari,
baadhi ya wateule wako na watendaji wake wamekalia viti walivyonavyo si
kwa sababu ya kuwa kwao na uwezo kustahimili ukosoaji, au upeo wao wa
kuchochea maendeleo ya kitaaluma, bali kwa kuendeleza na kuyatumikia
matakwa ya utarishi wa kifikra na kimatendo.
Kwa
waraka huu mheshimiwa Rais, wakati tukikuahidi kwa dhati kabisa wewe
binafsi na Watanzania wenzetu kwamba, tutaendelea na kazi kwa kuzingatia
miiko na maadili ya uandishi wa habari, sambamba na kuheshimu sheria
zilizopo, tunapenda kuliweka hili bayana kwamba, tutakuwa wa mwisho
kuwatii viongozi dhalimu, madikteta, waliokosa utu na ambao kwao hila
ndiyo msingi mama wa kupotosha na kupindisha mambo kwa sababu tu ya
kulinda maslahi na malengo yao binafsi au yale ya makundi yenye hila.
Rais
wangu, nimeona nitakuwa mtu nisiyekutakia mema wewe binafsi na taifa
kwa ujumla, iwapo nitakaa kimya na kuruhusu fikra za kikaburu
zikijijenga vichwani mwa viongozi wetu.
Mheshimiwa
Rais, tutakuwa tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama wanahabari,
wahariri na viongozi iwapo tutahalalisha kwa sababu ya ukimya wetu
majina mabaya tunayoitwa leo na wateule wako kama wasaliti, wachochezi
na wazushi.
Miye
binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba iwapo wewe utaamua kwa moyo na
nia njema kulinusuru taifa letu na majahili hao walio ndani ya Serikali
yako, basi siku moja historia itakuja kuandika kwa usahihi na ufasaha
jina lako na letu..
Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment