Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA hali ilivyokuwa ndani ya klabu za Tanzania, hususan zile
kongwe za Simba na Yanga, utaamini kuwa hata aje kocha wa aina gani, bado
mabadiliko yanaweza kuwa ya kubangaiza.
Siku kocha mpya wa Simba, Zdravko Logarusic alipowasili Tanzania.
Hii ni kwasababu mara kadhaa utaona jinsi baadhi ya viongozi
wa soka na wadau wao wanavyojifanya hawanazo katika kubuni mikakati yenye
kuleta maendeleo ya klabu zao.
Wakati nasema haya, nakumbuka jinsi kocha mpya wa Simba,
Zdravko Logarusic alivyopokewa kwa mbwembwe na mashabiki wa timu hiyo yenye
maskani yake mitaa ya Msimbazi.
Hata hivyo, utagundua kuwa aina ya mapokezi ya Logarusic si
kitendo kigeni, maana tayari walishawahi kupokewa kwa vishindo kiasi cha wao
wenyewe kujishangaa.
Hakika siwezi kuvumilia. Siwezi Kuvumilia, maana najua kocha
huyo hatakuwa na maisha mazuri ndani ya
Simba. Anapita njia tu. Labda amekuja kutalii au kujionea viongozi wa soka
wasiokuwa na dhamira ya kweli ya kuokoa soka letu.
Ama amekuja kuangalia mashabiki na wanachama wenye mihemko ya
aina yake. Ukifiria sana unaweza kulia. Ni pale makocha hao wa kigeni, mfano wa
Logarusic wasivyokuwa na heshima mbele ya jamii yao pale matokeo yanapokuwa
magumu.
Kwa wasiojua, chokochoko huanza tararibu mno. Kwanza utaona
kocha anavyopangiwa wachezaji wa kucheza uwanjani na wale wanaotakiwa wawekwe
benchi.
Kesho utaona anavyoingia kwenye mkwaluzo na viongozi wake na
mwisho wake wanachama au mashabiki wanaingilia kati. Matusi na kejeli yanapamba
moto.
Mwisho wa siku ni safari ya aibu. Matusi lukuki kuelekezwa
kwa makocha ambao hapo kabla walipokewa kama wafalme. Kwa klabu za Simba na
Yanga, naweza kusema kwa miaka hii hata kama aje Sir Alex Ferguson au Rafael
Benitez, bado hakutakuwa na kipya.
Ndio, maana makocha hao watakapofanikiwa kuunda program zao
hazitakuwa na mashiko na badala yake wataambiwa namna ya ufanyaji wa kazi wenye
kutafuta sifa za kijinga.
Hakika siwezi kuvumilia hata kidogo. Hali hii inanifanya
nione bado kuna kila sababu ya kujiangalia upya katika harakati za kukuza na
kuendeleza soka letu.
Hii hali ya kuwashangalia makocha wa kigeni leo na kesho
kuwatukana bila sababu za msingi zimepitwa na wakati. Huu ndio ukweli. Ifikie
wakati kila mmoja ajitambue.
Ndio maana nasema, karibu kocha mpya wa Simba, ila pia
ujiandaye kwa mengi maana Simba hii uliyoshangiliwa wewe siku zote haitabiriki
na haina mipango ya kweli ya kimaendeleo.
Tukutane wiki ijayo.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment