Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
VIJANA wenye vipaji na uhitaji wa kucheza soka wametakiwa
wacheze soka kwa kujituma ili wafikie malengo, badala ya kutegea katika mazoezi
hivyo kujiweka katika hatari ya kushindwa kufika mbali na kutimiza malengo yao.
Hayo yamesemwa na kocha wa timu ya soka ya Komsala, wilayani
Handeni, mkoani Tanga, Sufian Omary, katika mazoezi ya vijana wake wanaoendelea
katika mashindano ya Mbuzi Cup inayokutanisha timu mbalimbali za Kata ya
Kwamatuku.
Akizungumza mapema wiki hii wilayani humo, Omary alisema
kwamba vijana wengi wanaopenda kuwika katika soka, wameshindwa kufika mbali
kutokana na kutegea katika mazoezi yao
uwanjani.
“Wachezaji wote wenye malengo yao
lazima wafanye mazoezi makali na kuweka bidii uwanjani, hivyo lazima mcheze kwa
bidii, ukizingatia kuwa hakuna mashindano madogo hata kama
tungekuwa tunagombea kuku.
“Naamini tukifanya hivyo itakuwa ni njia ya kuiweka timu
yetu katika nafasi nzuri zaidi, huku ikiwa njia ya wachezaji wenyewe kuwa katika
wakati wa kuwaza maendeleo katika mashindano,” alisema.
Timu ya Komsala ni miongoni mwa maeneo yenye wachezaji
wazuri kiasi cha kutia hamu kuwaangalia wanavyokuwa uwanjani, huku wakishiriki
katika mashindano ya kugombania mbuzi katika Kata ya Kwamatuku, yanayofanyika
katika Uwanja wa Kijiji cha Kweingoma.
No comments:
Post a Comment