Taarifa ya EWURA YA bei mpya za umeme zitakazoanza kutumika Januari, Mosi,2013
Tarehe
11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha
maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA). TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia
67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1
Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.
Vilevile
TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme
kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko
ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba
kuidhinishwa viwango vya gharama za kuunganisha umeme vinavyozingatia
ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa
huduma zitolewazo na TANESCO.
Kwa mujibu wa TANESCO, kupitishwa
kwa maombi haya kutaliwezesha Shirika (a) kupata fedha za uendeshaji na
uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya Shirika liweze kukopesheka na
hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu, (c) kuliwezesha
Shirika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya
Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa
kufanya
matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo ili kuhakikisha
kunakuwa na upatikanaji wa huduma za umeme wa uhakika kwa wateja.
Itakumbukwa
kwamba bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari
2012. Bei hizo zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya
TANESCO ambapo ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155.
Sababu ilikuwa ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa
na hali ya ukame katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya
kuzalishia umeme, toka mwaka 2011.
Hali hiyo ilipelekea TANESCO
kulazimika kununua umeme kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura
(Emergency Power Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia
umeme bado sio nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka
kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers).
USHIRIKISHWAJI WA WADAU
Kulingana
na Kifungu Na. 19(2) (h) cha Sheria ya EWURA, Mamlaka ilifanya Taftishi
ili kupata maoni juu ya ombi la kurekebisha bei za umeme. Ukusanyaji wa
maoni ulihusisha pia mikutano minne (4) iliyofanyika Iringa na
Shinyanga tarehe 15 Novemba 2013, Bagamoyo tarehe 20 Novemba na
kuhitimishwa Dar es Salaam tarehe 22 Novemba 2013. Aidha, tarehe 6
Desemba 2013, EWURA iliitisha mkutano wa mwisho wa wadau wakiwemo
wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini(MEM), TANESCO, Shirika la
Umeme la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Baraza
la Watumiaji na Baraza la Ushauri la Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa
Saruji wa Afrika Mashariki, na kiwanda cha ALAF. Katika mkutano huo
EWURA iliwasilisha mwelekeo wa maamuzi kuhusu maombi ya TANESCO na namna
zilivyokokotolewa. Wadau walipewa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu
mwelekeo wa bei na maoni yao yamezingatiwa katika kufikia maamuzi ya
mwisho.
UCHAMBUZI NA UAMUZI
Kwa kufuata sheria na kanuni
zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa bei ya umeme, EWURA ilifanya uchambuzi
wa kifedha na kiufundi ili kubaini uwezo wa TANESCO katika kutekeleza
majukumu yake ya kila siku. Uchambuzi uliangalia utendaji wa Shirika la
TANESCO katika miaka iliyopita na pia iliangalia majukumu yanayoikabili
TANESCO katika miaka mitatu ijayo. EWURA imebaini kwamba hali ya kifedha
ya Shirika la Umeme sio nzuri. Shirika limeendelea kupata hasara,
ambayo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na
kufikia shilingi bilioni 223.4 mwishoni mwa mwaka 2012. Pamoja na
mapungufu ya kiufanisi, sababu kubwa ya ongezeko la hasara ni kuongezeka
kwa gharama za uzalishaji wa umeme ambao TANESCO inanunua kutoka kwa
wazalishaji binafsi. Hali hii imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni
yake ya muda mfupi na ya muda mrefu, ambayo yamelibikizwa na kufikia
TZS 456.8 bilioni tarehe 22 Novemba 2013, hali ambayo inatishia
uendelevu wa huduma ya umeme hapa nchini.
Mamlaka imetumia Kanuni
ya Ukokotoaji wa Bei kama ilivyopendekezwa na AF-MERCADOS wakati wa
kukokotoa mahitaji ya mapato ya TANESCO. Kanuni hiyo inawezesha
kukokotoa bei zinazolandana na gharama halisi kwenye mfumo wa umeme na
kuzigawa kwenye makundi ya watumiaji umeme, kadiri kila kundi
linavyosababisha gharama kwenye mfumo wa umeme kwa mujibu wa mahitaji ya
Sheria ya Umeme ya 2008 Kifungu cha 23(2)(f).
EWURA imejiridhisha kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya TANESCO, unahitaji njia/mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi (Cost Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa gharama nafuu ama ruzuku kutoka Serikalini ili kulipa limbikizo la madeni ya Shirika.
Bodi
ya Wakurugenzi wa EWURA, katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013
pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa
viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, kama ifuatavyo:
Kundi
D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa vijijini, ambao
hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza wigo wa
mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, lengo likiwa ni
kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi
ya umeme kwa kiwango hicho, na pia kuwahamasisha kutumie zaidi umeme.
Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa
mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za
sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la
watumiaji wakubwa wa umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za
kukoboa na kusaga nafaka, taa za barabarani, mabango n.k. Bei
iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la
Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO ilipendekeza ongezeko la shilingi
131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao
hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa
mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya
kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni
kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa waliounganishwa katika
msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA imeidhinisha bei ya nishati kwa
kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 45
ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 148 kwa
uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa
waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na
zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei
iliyoidhinishwa ni shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la
shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa
uniti moja.
Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa kila baada ya
miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango na bei za mafuta;
mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha, na upatikanaji wa ruzuku
toka Serikalini.
Vilevile, TANESCO inatakiwa kutekeleza miradi
ya uwekezaji iliyoainishwa kwa kutumia fedha zitakazokusanywa kutokana
na bei zilizoidhinishwa. EWURA inaweza kurekebisha bei ya umeme ya
TANESCO kila mwisho wa mwaka 2014 na/au mwaka 2015 endapo TANESCO
itashindwa kutekeleza miradi iliyotajwa katika Jedwali husika.
Marekebisho hayo yatatokana na makadirio ya gharama za miradi ambayo
haikutekelezwa.
Kutokana na matazamio ya kuwa na mabadiliko
makubwa katika uzalishaji wa umeme (generation mix) katika mwaka 2015 na
kuendelea, kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa kwa upatikanaji wa
gesi asilia, EWURA itafanya utafiti kubaini gharama halisi (Cost of
Service Study) ya huduma ya umeme kwa wakati huo. Hivyo, bei
zilizoidhinishwa zitatumika mpaka mwaka 2016, kama utafiti unaotazamiwa
kufanywa hautakamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2015.
EWURA
ililinganisha bei za umeme kwa kila Uniti, katika nchi za Afrika ya
Mashariki, na kuona kuwa bado bei za umeme za Tanzania zipo chini
ukilinganisha na bei za katika nchi jirani kama inavyoonyeshwa hapa
chini, kwa makundi mbalimbali ya watumiaji umeme.
Pamoja na maamuzi hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, pia iliagiza TANESCO kutekeleza yafuatayo:
Bei
mpya za umeme zitaanza kutumika tarehe 1 Januari 2014. Ni matarajio ya
EWURA kwamba TANESCO watatumia fursa hii kutoa huduma bora zaidi za
umeme na kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko ya wateja kila
yanapojitokeza ili kurejesha imani kwa Shirika la Umeme la TANESCO.
No comments:
Post a Comment