Na Kambi Mbwana, Handeni
KWA wiki kadhaa sasa, nipo katika mkoa wa Tanga, nikiwa
kwenye majukumu mengine ya Kitaifa, ukizingatia kuwa ili Dunia isonge mbele
lazima kuwe na pilika pilika za kimaisha. Nimetembelea wilaya kadhaa na
kujionea mambo mengi ya kunifurahisha, hasa yanayohusu mchezo wa mpira wa
miguu.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto, moja ya viongozi wanaopaswa kuwa makini katika utendaji wao ili kuendeleza mpira wa miguu kwa vitendo.
Mchezo huo unaopendwa na watu wengi duniani, ni kati ya sekta
ambazo tunashuhudia mwingiliano mkubwa sanjari na kuvutia vijana wetu
wanaopenda kujiingiza katika kandanda.
Mpira wa miguu ndio michezo mizuri na rahisi kuchezwa na
inayovutia wengi, maana hata watoto mtaani utakuta wameweka mawe yao manne,
mawili huku na mawili kule kama goli zao.
Hii inavutia kusimama na kuangalia jasho linavyotoka kwa
watoto hao. Utajisikia raha kuona chenga na nyodo zinavyoonyeshwa kwa watoto hao
ndani ya uwanja, wenyewe wanaita ‘Chandimu’.
Hata hivyo, mawazo yakikujia kuwa watoto hao wachache unaoona
kwa macho yako, ni kati ya mamia yanayoibukia uswahilini na kutokomea
kusipojulikana kwa ajili ya uzembe wetu.
Ndio ni uzembe wetu, maana tuliokuwa wengi tumezoea kuangalia
majina ya akina Mrisho Ngassa, Juma Kaseja, Kelvin Yondan, yakitawala kwenye
vyombo vya habari na kushindwa kuweka sera nzuri kuhakikisha kuwa vijana wengi
wanapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao.
Hapa ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi Kuvumilia kwasababu
wengi wao wanaangalia walipokuwapo. Hatuna dhamira ya kweli.
Pamoja na kusema yote hayo, najikuta nikihema, nikiona kwa
sasa sina kwa kuelekeza lawama zangu, hasa ukiangalia kuwa utawala mpya ndani
ya Shirikisho la Soka nchini TFF umeingia.
Alikuwa Leodgar Tenga kama Rais wa TFF na sasa ni Jamal
Malinzi. Huyu Malinzi ameingia kwa mkwara mzito sana. Kila siku ya Mungu
nasikia matamko kiasi cha kupasua kichwa change.
Sawa, nikisema sana nitaambiwa muda bado. Lakini je, Malinzi
ameingia TFF na watu wote wapya? Bila shaka utagundua kuwa baadhi yao
walikuwapo katika utawala wa Tenga.
Zaidi ya hapo utaona ni ubabaishaji tu. Hakika hatuwezi
kusonga mbele kama hatugundua makosa yetu.
Ukweli ni kwamba sehemu za mikoani, katika vijiji mbalimbali vimejaa
vipaji, lakini hatuna mipango zaidi ya kuona wale waliokuwa kileleni wanaendelea kubabaikiwa na kufifisha ndoto nyingine.
Si mara moja kupokea simu kutoka kwa watu wa mikoani
wakililia mahali kwa kuonyesha uwezo wao. Viongozi wetu wa chama na serikali
nao wamekalia siasa, kutoa sera zao kwenye kampeni na baada ya kupata
wanachohitaji wanajifanya hawaoni wala kusikia.
Mechi za mchangani katika maeneo yao hufanyika wanapokwenda
kuzindua kampeni zao sanjari na kuwanunua vijezi vya bei rahisi ili kuwarubuni
katika mchakato wao wa kisiasa.
Huu si wakati wa kupiga porojo wakati maelfu ya vipaji
yanatokomea katika vijiwe vya gongo na bange. Nani asiyependa kuona akina
Ngassa wapya wanatokea katika maeneo yenye changamoto mbalimbali?
Je, tunaona thamani gani kushindwa kubuni walau ligi ndogo za
mikoani, au kusaidiwa vifaa vya michezo kwa timu za mikoani kabla hata ya
Uchaguzi Mkuu? Kila mtu atomize wajibu wake.
Kinyume
cha hapo, siwezi kuvumilia kuona hatuna jipya katika
kubuni mikakati yenye tija na soka letu. Sio siri, huku nilipokuwa
katika
vijiji mbalimbali vya wilaya ya Handeni, natamani nisihudhurie mechi za
mchangani maana naona aibu kuwa vijana hawa wanaishia gizani miaka nenda
rudi. Au kama kweli tuna dhamira ya kuendeleza soka letu, tukitoka
kwenye soka la magazetini, tuhamieni chandimu.
Tukutane tena wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment