Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, amesema kila mtu ana
haki ya kugombea urais, ila si muhimu agenda ya ujana ikaendelea kuungwa mkono, maana haina jipya wala faida katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Akizungumza katika kituo cha luninga cha Star Tv leo asubuhi,
Sumaye pichani, alisema kwamba sera ya ujana haina mashiko, maana mtu anachaguliwa
kutokana na sifa na vigezo alivyokuwa navyo.
Alisema hali hiyo inamfanya aone wasiwasi mkubwa kutokana na
baadhi ya watu kuanza kupita kwa visingizio kuwa huu ni wakati wa ujana kupewa
maajukumu makubwa yaa kiuongozi.
“Naweza kukubaliana na mahitaji ya watu wote wenye sifa ya
kugombea uongozi, lakini si sahihi kofia ya ujana ikapewa chapuo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Sumaye alisema wapo baadhi ya watu
wanafanya kazi kubwa kuwanunua wa kuwaunga mkono jambo ambalo si sahihi na
linapaswa kuangaliwa upya na Watanzania wote.
Alisema mwanasiasa wa aina hiyo akitoa fedha nyingi kununua
watu wake, matokeo yake ni magumu kwasababu anaweza kuingiza nchi kwenye hatari
kubwa.
“Mtu kama amepewa fedha nyingi ili apate uongozi kutoka kwa
watu wake, akiwa rais huyo sidhani kama anaweza kusimamia jukumu zito la
ulipaji kodi,” alisema.
Kwa mujibu wa Sumaye, chama kina utaratibu wake wa kuwapata
viongozi, hivyo hakuna shaka utasimamiwa vizuri sanjari na kupambana na watoa
rushwa, maana nchi itaingia kubaya.
No comments:
Post a Comment