Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Juzi Juni 29, klabu ya soka ya Simba ilifanya uchaguzi wake
mkuu baada ya mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, kumaliza muda wake wa miaka
minne wa kuongoza.
Katika uchaguzi huo watu mbalimbali walijitokeza
kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye klabu hiyo. Nafasi za juu za uongozi zilikuwa ni rais ambapo
Evans Aveva alikuwa akichuana na Andrew Tupa na makamu wa rais ilikuwa
ikigombewa na Geofrey Nyange Kaburu, Jamhuli Kihwelo ‘Julio’ na Swed Mkwabi.
Sitaki kusema nani aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro
hicho ila kuwakumbusha wanachama wote na viongozi wapya walioingia madarakani
kusimama kwenye ukweli, kuwa Simba haina maendeleo licha ya kuasisiwa miaka
1936.
Hii ni aibu
kubwa kwa klabu kama hii. Nilibahatika kutembelea maeneo mbalimbali kusikiliza
kampeni za wagombea, hususan Temeke, Ilala na Kinondoni, ambapo kampeni
zilifanyika katika Ukumbi wa Urafiki na kuhudhuriwa na watu wengi sana.
Kila mmoja alikuwa akijaribu kuonyesha cheche zake
juu ya nafasi anayogombea. Wote walionyesha wana kitu cha kufanya. Hata hivyo,
mara nyingi mtu anapotaka jambo lake hutumia ufundi mwingi kuomba kura
ikiwezekana hata kuongopa.
Anafanya hivyo kwasababu anataka achaguliwe. Baada
ya kuchaguliwa baadhi yao husahau na kufanya mambo yao binafsi. Hii si sahihi.
Kwa klabu kama Simba inahitaji mipango na mikakati kabambe kwa ajili ya
kuipatia maendeleo.
Ajenda ya kwanza iwe kuijenga Simba imara na ya ushindi.
Hili likifanikiwa Simba itafanya vizuri kwenye ligi
na mashindano mbalimbali ili kurudisha heshima na hadhi ya klabu hii kongwe.
Ajenda ya pili iwe kuendeleza soka la vijana.
Hii inajulikana kuwa Simba ilishaweka misingi ya
kuendeleza vijana, ndio maana waliibuka akina Jonas Mkude, Ramadhan Singano na
wengineo.
Hili lifanyike bila kuangalia nani yupo madarakani
kwasababu ni sera nzuri zenye manufaa kwa maendeleo ya Simba. Ajenda ya tatu ni
kuhakikisha kuwa Simba inakuwa na uwanja wake wa kisasa ili kuondoa gharama za
kukodi viwanja vya michezo.
Imeshakuwa
kero na aibu kubwa kwa Simba hii kongwe kukosa uwanja wake. Imezidiwa ujanja na
Azam FC iliyozaliwa miaka ya karibuni.
Ndio, Azam inamilikiwa na mfanyabiashara inajimudu.
Lakini katika msingi wa soka la Tanzania mtaji mkubwa kwa klabu hizi ni watu.
Simba ina wanachama wengi bila kusahau mashabiki
nchini kote. Ina uwezo wa kufanya lolote kutokana na hadhira ya mashabiki wao.
Hii ni tofauti na Azam wanaosubiri mashabiki kutoka
Simba au Yanga.
Aidha viongozi hao wapya lazima wafahamu kuwa ili waendelee ni
pamoja na kuiendesha klabu kibiashara.
Kuleta umoja,
utulivu na mshikamano ili kuwavutia wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuwekeza
kwenye klabu hii. Kampuni inayojitambua haiwezi kuingia mkenge kwa klabu
isiyokuwa na dira. Klabu inayozalisha mizozo kila baada ya miezi miwili.
Nasema hili huku nikiamini kuwa utawala wa Rage
ulikuwa na kasumba. Mengi yalisemwa na kusikika mchana na usiku. Wapo
walioambiwa ni mambumbumbu. Wapo walioambiwa barua zao ni za uchumba si za
kikazi.
Hili liliweza
kuwavunja moyo wanachama na kujikuta kuisusa timu yao. Ikafikia hatua mbaya
Simba kuingiza mapato madogo uwanjani sambamba na kupata matokeo mabaya
uwanjani.
Kutokana na hilo, najikuta nikiwakumbusha viongozi
wapya wa Simba kufanya kazi kama timu moja kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao
kongwe.
Watu wanataka maendeleo si porojo za kikampeni.
Wahakikishe kuwa wanakaa chini kubuni sera, miradi kwa maendeleo yao. Waunde
timu yenye ushindi, sanjari na kuzalisha mapenzi mema kwa klabu hii ya Tanzania
Bara.
Simba ina wadau wengi. Inao viongozi wa juu wa Serikali,
wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Iwatumie hao kutafuta vyanzo vya mapato vya
klabu badala ya kuchangishana kila siku.
Kwa kufanya
hivyo, tunaamini Simba itajiendesha yenyewe na si kutegemea fedha za wafadhili
zilizoanza kulalamikiwa na baadhi ya Watanzania, huku ikidaiwa kuwa wafadhili
hao wapo kwa ajili ya kuinyonya Simba.
Mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Friends of Simba,
Zacharia Hanspope alitumia muda mwingi kuwaelezea wanahabari uwapo wa kundi
hilo na faida yake.
Mengi aliyosema yana ukweli. Pope alisema ili Simba
iweze kujitegemea yenyewe kunahitaji mipango na si porojo tu za kampeni. Pia
akasema ghafla haiwezi kujiendesha maana haina vyanzo vingi vya mapato na
inahitaji fedha nyingi za usajili, gharama za safari, maandalizi ya ligi na
gharama nyingine lukuki.
Ukisitisha ufadhili hasa fedha za wana Simba, nani
mwingine atachangia wakati mapato ya milangoni ni kiduchu? Haya ni maswali
muhimu ambayo mwisho wa siku utagundua yana tija. Ili upate 10 ni lazima uanze
kwanza na moja.
Hivyo naamini kwa pamoja klabu hii itapiga hatua
kama itawatumia watu wake kusimamia sera na mipango ya klabu. Yale
yaliyoahidiwa kwenye kampeni, yale yenye tija basi yasimamiwe kwa vitendo ili
kuona klabu inapiga hatua kubwa ndani na nje ya nchi.
kambimbwana@yahoo.com
+255712053949
No comments:
Post a Comment