Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KIUNGO wa zamani wa Simba aliyekatisha mkataba wake
Abdulhalim Humud, ataanza rasmi kuitumikia klabu yake mpya ya Sofapaka ya
nchini Kenya keshokutwa, baada ya kupata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC).
Humud ambaye kipaji chake soka kilianza kuonekana
akiwa na timu ya Mtibwa ya Sugar ya Morogoro, yupo tayari kwa ajili ya kuanza
rasmi maisha mapya ya kutumikia Sofapaka ya nchini Kenya, baada ya kumalizana
na klabu hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Humud alisema
amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuichezea Sofapaka, baada ya timu
hiyo kuonyesha nia ya kumuhitaji kwa muda
mrefu ili kutumikia klabu hiyo nchini Kenya.
Alisema kuwa Sofapaka kwa sasa ipo katika nafasi ya
nne kwenye msimamo wa ligi kuu nchini Kenya, huku akiamini klabu hiyo
itamuwekea mazingira mazuri ya kuonyesha soka la aina yake ndani ya timu hiyo.
“Mimi nashukuru mungu kwa kila jambo nimekuwa
nikikutana na mitihani mingi, lakini mungu amenipa ujasiri na kuishinda sasa
hivi nimesajili na Sofapaka, nimekuja kuaga kwa ajili ya kurudi nchini Kenya
kuanza kuitumikia klabu yangu hii.
Msimu uliopita Humud alijiunga na Simba akitokea
Azam FC, ambayo ilishindwa kutambua mchango wa kiungo huyo na kumsotesha benchi
misimu miwili, kisha baadae msimu uliofuata alirudi tena kuitumikia Simba.
Hata Hivyo Humud alishindwa kupata namba katika
kikosi cha Simba, tangu Kikosi hicho kiwe chini ya Kocha Mcroatia Logarusic
ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Simba kutoka kwa Wazawa Abdallah Kibaden na
msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio.’
Kutokana na mizengwe hiyo kiungo huyo aliamua
kukatisha mkataba wake na Simba mara baada ya msimu wa Ligi Kuu Bara kumalizika
huku timu ya Azam FC wakitawazwa kuwa mabingwa wapya.
No comments:
Post a Comment