Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU chache baada ya kusajiliwa rasmi chini ya Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, Taasisi inayojulikana kama Handeni Kwetu
Foundation, imepangwa kuzinduliwa August 5 mwaka huu, katika Ukumbi wa Vijana
Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutafuta namna ya kusaidiana na
serikali katika mambo mbalimbali, ikiwamo Kujenga uwezo kwa jamii kujikwamua
kiuchumi na kuhamasisha utawala.
Akizungumza hilo, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa taasisi hiyo,
Kambi Mbwana, alisema taasisi hiyo imeanzishwa na itafanya kazi zake bila
kuvunja masharti yaliyowekwa na serikali ili kuhakikisha kuwa malengo
yaliyokusudiwa yanapatikana.
Alisema kuwa taratibu za kuelekea kwenye uzinduzi huo zinaendelea
kuwekwa katika hali ya kukutana pamoja kwa wageni walioalikwa kushuhudia
uzinduzi huo wa aina yake.
“Kwa miezi kadhaa sasa taasisi ilikuwa kwenye mchakato wa usajili
wake, hivyo baada ya kukamilika, kinachofuata sasa ni kuzindua ili ianze kazi
zake kama ilivyokusudia.
“Taasisi hii itakuwa na Makao yake Makuu wilayani Handeni, lakini
itafanya kazi zake nchi nzima na huko mbele itakuwa na ofisi katika kila eneo
itakaloona inafaa,” alisema.
Sababu nyingine za kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuleta ustawi
kwa jamii katika njanya mbalimbali, kutoa mafunzo kuhusu kilimo bora na jinsi
ya kutafuta masoko, kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha misingi ya utawala
bora, kutoa elimu na ushauri kuhusu mbinu bora za kuimarisha afya na elimu ya msingi kuhusu Virusi vya
Ukimwi na Ukimwi.
Malengo mengine ni kutoa elimu kuhusu makundi rika katika elimu ya
uzazi, kuhamasisha na kushawishi jamii kuzingatia ustawi wa mtoto katika jamii,
kufanya utetezi kwa makundi maalum ambayo haki zao zinakiukwa na kufanya tafiti
mbalimbali zenye malengo ya kuboresha maisha ya jamii, kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment