Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa zamani wa Simba, Michael Wambura amepingana
na maamuzi ya Rais wa Simba, Evans Aveva ya kupeleka hoja ya kujadiliwa
uanachama wake kwenye Mkutano Mkuu wa timu hiyo, unaotarajia kufanyika Agosti 3
mwaka huu akidai ameshasafishwa na Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Juzi Aveva alitangaza kuwasimamisha uanachama
wanachama 69, waliofungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam
ya kusimamisha uchaguzi wa Simba uliofanyika Jumapili iliyopita, pamoja na
kujadili uanachama wa Wambura, ambaye naye aliipeleka Simba mahakamani mwaka
2010.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Wambura
aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa madai ya kufanya kampeni
kabla ya muda alisema, Kamati hiyo ya TFF ilithibitisha kuwa yeye ni mwanachama
halali ingawa alienguliwa kugombea kwa kosa hilo la kampeni, huku akidai
kuwasimamisha wanachama hao kutaongeza makundi kwenye timu hiyo.
“Hilo mimi sioni kama kuna sababu ya kulijadili
lakini nawataka Kamati hii iliyoingia madarakani kufuta maamuzi yao ya
kuwasimamisha wanachama hawa, kwani hawajatenda haki kwa mujibu wa Katiba ya
Simba ibara ya 41(d) kwa kuwanyima wanachama fursa ya kujitetea na kusikilizwa
kabla ya kuchukua hatua , hivyo ni uvunjifu wa haki za msingi za binadamu. Kama
zinavyoainishwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya
13(6)a pamoja na kanuni za nidhamu za FIFA ibara ya 94(1) na kanuni za adhabu
za TFF Ibara ya 35 (1),” alisema.
Wambura pia amedai kuwa, kusimamishwa wanachama hao ni
kusababisha mpasuko kwa klabu hiyo na wameenda kinyume cha utaratibu wa katiba
ya Serikali, TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hivyo wametumia
udikteta.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya Simba Ibara ya 54
(3), uamuzi wowote wa kufukuza wanachama lazima upigiwe kura za siri na wajumbe
theluthi mbili waunge mkono na ndipo maamuzi yafikiwe, lakini sio kama
walivyofanya wao hivyo hali hii italeta matabaka mawili ya wanaounga mkono
uongozi na wanaopingana nao.
Alisema uongozi wa Aveva, hauwezi kupambana na
wanachama zaidi ya 500 na hawataweza vita hiyo zaidi watasababisha migogoro,
hivyo wakae chini na kuliangalia hilo ambapo atawapelekea nakala yake ya taarifa
hiyo aliyoisoma kwenye vyombo vya habari kama ushauri.
Licha ya Wambura kutetea wanachama hao ambao walikuwa
wakimuunga mkono, lakini anakinzana na katiba ya Simba ibara ya 11(1)b inayokataza
kupeleka masuala ya soka mahakamani, sambamba na ibara ya 55 inayofafanua
adhabu ya atakayetenda kosa hilo, ambayo ni kusimamishwa uanachama na baadaye
kujadiliwa kwenye mkutano mkuu.
No comments:
Post a Comment