Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHINDANO la urembo la kumpata malkia wa Kanda ya Mashariki limepangwa
kufanyika Agosti 8 mwaka huu kwenye Ukumbi wa hoteli ya Nashera
iliyoko mkoani Morogoro.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa
shindano hilo, Alex Nikitas, alisema kuwa warembo 14 ndio watachuana
kuwania taji la kanda hiyo.
Nikitas alisema kuwa shindano hilo litashirikisha warembo kutoka mikoa
ya Lindi, Mtwara, Pwani na wenyeji Morogoro.
Aliongeza kuwa maandalizi ya shindano hilo yako katika hatua za mwisho
na washiriki wanatarajia kuingia kambini mapema wiki ijayo kujiandaa
na kinyang'anyiro hicho.
"Mwaka huu tumejipanga kufanya shindano lenye ubora wa hali ya juu,
tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kujitokeza kushuhudia fainali za
kanda hii ambayo safari ya mshindi wa taifa itaanzia," alitamba
mratibu huyo.
Alisema kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu watapata nafasi
ya kuiwakilisha kanda hiyo katika fainali za Taifa "Redd's Miss
Tanzania 2014" zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Diana Laizer kutoka Morogoro ndiye mrembo anayeshikilia taji la kanda
hiyo ya Mashariki na katika fainali zilizopita za Redd's Miss Tanzania
alifanikiwa kuingia katika hatua ya 15 bora.
Mrembo Happiness Watimanywa wa mkoani Dodoma ndite anayeshikilia taji
la taifa na mwaka huu ndiye atakwenda kuiwakilisha Tanzania katika
fainali za dunia (Miss World).
No comments:
Post a Comment