Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
akiwa na Rais mpya wa Malawi Prof. Arthur Peter Mutharika wakiwa katika
picha ya pamoja baada ya rais mpya wa Malawi kukabidhiwa madaraka leo
jijini Brantyre kwenye hoteli Sunbird. Baada ya kukutana viongozi hao
walipata fursa ya kuzungumzia masuala la kidiplomasia baina ya nchi hizi
mbili na kukubaliana kuendelea kuwa na mahusiano mema kama nchi
zinazoishi ndugu na jirani. Picha kwa Hisani ya Ikulu ya Malawi
Na Mwandishi Wetu, Malawi
MAKAMU wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DkT. Mohammed Gharib Bilal jana
Jumatatu Juni 02, 2014 alishiriki katika sherehe za kukabidhi madaraka
kwa Rais mpya wa Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika katika sherehe
zilizofanyika kwenye uwanja wa Kamuzu Banda jijini Blantyre. Sherehe
hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Botswana sambamba na wawakilishi wa
nchi za Zimbabwe, Msumbiji, Afrika Kusini na nyinginezo.
Akihutubia
baada ya kukabidhiwa sime ambayo ni ishara ya kuwa kiongozi wa watu wa
Malawi, Rais Mteule Mutharika alisisitiza kuwa, katika kipindi cha
utawala wake atahakikisha kuwa anaifanyia makubwa Malawi sambamba na
uhakikisha kuwa anaifanya Malawi itimize majukumu yake ya kimataifa
kufuatia kutambua kuwa kujitenga kunaweza kuifanya Malawi kutonufaika na
fursa zilizopo duniani.
“Nchi
hii ipo katika dunia na siyo rahisi tena kuwa na fikra kwamba Malawi
inaweza kubaki peke yake kama kisiwa. Tunahitaji kuwa na wenzetu wa
kusaidia maendeleo ya Malawi. Tunawahitaji wahisani toka Kusini ama
Mashariki, tunayahitaji mataifa tajiri na mataifa yanayoendelea.
Tutafanikiwa sana kama tutaendeleza urafiki kwa wote. Tufanye hivi bila
kujali kuwa sisi ni taifa kwani hali ya sasa inahitaji kila mmoja wetu
kushirikiana na mwenzake,” alisema.
Katika
hotuba hiyo pia amesisitiza kuwa kipindi chake cha utawala atajitahidi
kukabiliana na rushwa na kwamba hatakuwa na mchezo kwa wala rushwa
katika kipindi akiwa madarakani. Pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa
kuiunganisha Malawi kwa miundombinu bora ili kuboresha maisha ya
wananchi sambamba na kusogeza huduma za wananchi karibu.
Rais
Mutharika aliapishwa juzi baada ya kuwashinda washindani wake akiwemo
Rais aliyemaliza kipindi chake Joyce Banda ambaye hata hivyo hakuweza
kutokea katika sherehe hizi za kukabidhi madaraka. Akizungumzia suala la
kutohudhuria kwa Rais Banda, Rais Mteule Mutharika alisema alitegemea
Rais Banda kuwepo lakini hakufika na yeye anatambua kuwa wakati wa
uchaguzi kulikuwa na tofauti baina yao lakini kwa sasa uchaguzi umeisha
na amesahau yaliyopita ili kuanza ukurasa mpya wa kuijenga Malawi.
Katika shughuli hiyo pia Rais wa zamani wa Malawi Kamuzu Banda
alihudhuria.
Makamu
wa Rais Dkt. Bilal na msafara wake walitarajiwa kurejea nyumbani leo
hii Jumatatu mara tu baada ya kukamilika kwa kazi hii ya makabidhiano.
No comments:
Post a Comment