Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
AWALI sikuamini, hadi
nilipohakikishiwa kuwa picha za umati wa Watanzania wenzetu, 10,800 hadi 10,900
ni kweli walikusanyika katika Uwanja wa Taifa, kwa ajili ya kusaka nafasi 70 za
ajira kutoka Uhamiaji.
Sehemu ya Watanzania 10,800+ waliohudhuria usaili wa kuomba kazi Uhamiaji. Tukio hilo lilifanyika Juni 13, mwaka 2014 katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ndio, maana nilitegemea kuwa umati
ule ungepigwa katika mikutano ya kisiasa au matukio ya mpira wa miguu, hususan
Simba, Yanga au timu ya Taifa (Taifa Stars). Lakini sivyo. Uamuzi wangu wa
kumpigia simu swahiba au kijana mwenzangu aliyekuwa miongoni mwa watu hao
waliokwenda kufanyiwa usaili ulikuwa wa muhimu.
Alinijibu, “Ni kweli picha hizo ni za
waliokwenda kufanyiwa usaili wa nafasi 70 za Uhamiaji, nzuri zaidi na mimi
nilikuwapo hapo uwanjani Juni 13, mwaka 2014,” alijibu. Maneno haya yalinikera.
Yalinikera nikiamini kuwa hakukuwa na ulazima wa kuitwa watu wote hao kufanyiwa
usaili.
Huu ni udhalilishaji wa wazi wazi kwa
Watanzania wenzetu. Ikiwa wanaohitajika ni watu 70, sitaki kuamini kuwa
wahusika wangeshindwa kuwachagua kulingana na mahitaji yao. Pengine ingekuwa
nzuri zaidi kuchagua watu 200 na kuwachuja katika siku hiyo ya usaili.
Uhamiaji walikwenda kujua nini? Sifa
gani wanazohitaji kutoka kwa Watanzania hawa 10,800 waliozagaa katika Uwanja wa
Taifa? Naogopa. Mtizamo wa waliokuwa katika nafasi nzuri serikalini wanajua
wenyewe.
Na ndio maana mchakato huu unaidhalilisha
serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sikatai kuwa ajira ni tatizo
kubwa. Watanzania wengi hawana ajira kwasababu ya kufa kwa viwanda vyetu. Pia
baadhi yao wanaona kuajiriwa ndio suluhisho ya matatizo yao.
Kwa bahati mbaya, huenda pia
suluhisho halijulikani, ikiwamo kuwaandaa vijana kusoma kozi kulingana na soko
la ajira au hata kuwawezesha kwa mtindo mwingine, kama vile biashara, kilimo au
mengineyo muhimu.
Vijana hawa hawajaandaliwa kujiajiri
bali kuajiriwa. Inapotokea nafasi za kazi, utaona mahitaji ni watu 10 lakini waombaji
kazi makumi kwa mamia. Hivyo basi; badala ya kuwajaza kama walivyofanyiwa hawa,
ni bora utaratibu ni wengi. Kwa mwaka wanaoingia kwenye soko la ajira ni wengi
kutokana na vyuo vingi kuzalisha makundi kwa makundi. Wingi wa watu hao hauendi
sambamba na wingi wa nafasi za ajira serikalini na sekta binafsi pia.
Hivyo utaratibu huu ungekuwa wa
kuwachagua kulingana na sifa na mahitaji husika kabla ya kuitwa kwa idadi kubwa
isiyolingana na mahitaji yao. Narudia tena, hakukuwa na ulazima wowote wa
kuwajaza uwanjani Watanzania hawa.
Huku ni kuwavunja moyo. Ni
kuwapandikizia sumu dhidi ya serikali yao. Wakitoka pale, watatoka na picha
moja kubwa. Picha ya serikali kuwanyima ajira. Nani ametoa uamuzi huo wa
kuwachoma na jua nguvu kazi hii ya Taifa?
Baadhi ya mambo yanavyofanyika
yanazalisha chuki kwa serikali hii ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Rais ambaye
umakini wake, utukufu wake na uchapakazi wake unatatizwa na watu anaowaamini
wasimamie baadhi ya mambo serikalini.
Hii si haki hata kidogo. Hivi kweli
tunajivunia elimu zetu wakati zinashindwa kutambua baya na zuri kwa manufaa ya
nchi yetu? Au tunawapa watu maneno ya kusema? Kwamba watu wajuwe nchi hii ina
janga kubwa la ajira?
Hebu tujiulize, inapotokea tatizo la
mripuko au janga lolote kwa tukio hilo la usaili wa nafasi chache za ajira nani
wa kumlaumu? Narudia tena, nimeumizwa na kuchukizwa. Waliopendekeza usaili
ufanyike kwa siku moja, muda mmoja ni nani? Aibu.
Hii ni aibu na pengine walitaka
iingie kwenye kumbukumbu za Kidunia. Saa chache baada ya kufika kwenye usaili
huo, mitandao ya kijamii ilipendeza picha hizo. Kila mtu alisema lake, wakiwapo
wale walioisema vibaya serikali.
Mbaya zaidi, wapo wanaoamini kuwa
waliokwenda kufanyiwa usaili si wale watakaopewa ajira hizo kutokana na sababu
wanazosema wao. Hii inaonyesha ni jinsi gani watu wanavyokosa imani na
Watanzania wenzetu.
Sawa, fikiria mtu aliyechomwa na jua
katika usaili huo kisha ajira yenyewe anakosa. Nini afanye mtu huyu? Nani wa
kumfariji? Ndio, anaweza kuona ushindani ulikuwapo, lakini kwanini watu hao
makundi kwa makundi wasingeganywa? Au hata kuwachuja kama nilivyosema hapo juu?
Hii haiwezekani. Kila mmoja lazima afanye
kazi kwa bidii pamoja na kuweka sawa fikra sahihi kabla ya kuamua lolote. Tabia
hii ya kuwakusanya Watanzania wenzetu kwa kisingizio cha usaili wa nafasi za
kazi zikome mara moja.
Watafutiwe utaratibu mwingine mzuri.
Huu ni udhalilishaji, ingawa huenda wengine wanaona kawaida. Nasema haya kama
Mtanzania, maana tukio hili limefanyika katika ardhi ya nchi yangu na
waliokwenda kwenye usaili huo ni Watanzania wenzangu.
Nimekerwa na kuchukizwa, nikiamini
kuwa si wote wataipata kazi hiyo ya Uhamiaji. Kweli?
ANGALIZO; Maneno haya ni mtazamo wangu
binafsi. Si msimamo wa Taasisi ya Handeni Kwetu Foundation.
Kwa maoni na ushauri
+255 712053949
No comments:
Post a Comment