Na Mzee wa Bonde, Handeni
WAZEE pamoja na wananchi wa kijiji cha Kwamnele kilichopo kata ya
Ndolwa wilayani Handeni, wamesusia mikutano mikuu inayoitishwa na
serikali ya kijiji hicho kutokana na kukasilishwa na madai kwamba
uongozi wao umeuza ardhi yote ya kijiji kwa wageni.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kijiji hapo mwishoni mwa wiki, baadhi ya
wazee walisema kitendo cha kuitishwa mkutano na wao kuhudhuria ni kama
nao wameridhia na kupitisha kuuzwa huko kwa ardhi hiyo ambayo
imesababisha vijana wao wakose maeneo ya kulima.
Mwenyekiti wa
baraza la wazee la kijiji hicho kilichopo tarafa ya Mzundu, Hussein
Mavilu pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la
Mkwajuni, Ahmad Yusuph 'Semsekwa', walidai kwamba licha ya kuuza ardhi
hiyo, pia wameuza msitu wa Koluhombwa na Mjatakala wanayoitumia kwa
matambiko na faida ya kuleta mvua.
Mwenyekiti huyo alitaja majina
23 ya wageni hao ambao wameuziwa ardhi kwa kiasi cha kuanzia ekari 200
hadi 1,000 hatua ambayo imesababisha hadi mapori ya akiba ya kijiji
kukosekana ikiwemo kuuzwa kwa misitu hiyo wanayoitegemea kuleta mvua
kijijini hapo.
Mwenyekiti wa CCM akichangia suala hilo, alisema
kwamba mbaya zaidi viongozi wa kijiji wakiongozwa na Mtendaji Lameck
Feresi, waliwachangisha vijana kiasi cha kati ya sh. 5,000 hadi sh
10,000 kwa lengo la kuwapatia ardhi kutokana kijijini hapo lakini wengi
wao hawakupewa na fedha zao kuishia mifukoni mwa viongozi hao.
"Mimi kama Mwenyekiti wa Chama tuliwaita kutaka kuwaweka sawa lakini
wenzetu wamekaidi hawataki kutusikiliza wanajiona ni mabwana
wakubwa...Mbaya zaidi wanaamua mambo yao kupitia halmashauri ya kijiji
halafu wanasema ni wananchi wameamua," alisema Semsekwa.
Wakijibu
malalamiko hayo kwa nyakati tofauti Mtendaji wa Kijiji Feresi ambaye
wananchi hao hawataki tena kumwona katika kijiji hicho, na Mwenyekiti
wake wa kijiji Omari Sufiani, walikanusha madai hayo na kukiri kwamba
wameitisha mikutano Agosti na Desemba mwaka jana lakini wananchi
hawakutaka kuhudhuria.
Mtendaji huyo aliyekuwa na Mwenyekiti wa
kamati ya ugawaji ardhi Shabani Mhina pamoja na Mjumbe wake Bakari Sebo,
walisema uongozi wao umewauzia mashamba watu watatu tu na kila mmoja
wamemuuzia ekari 100 tu na wengine waliotajwa na wananchi hawakuhusika
kuwauzia mashamba wanayomiliki.
Waliwataja watu waliowauzia
kwamba ni Japhet ambaye walimuuzia ekari 100 akiwa na mtoto wake na kila
ekari moja walimtoza sh. 35,000, Ibrahim Mkaiani na Thomas Ngaiyani pia
eari 100 kila mmoja ambazo waliwatoza ekari moja sh. 30,000 ambapo
kijiji kilipata shilingi milioni 9.5 ambazo walijengea jengo.
Kuhusu kuuza msitu wa koluhombwa na Mjatakala, viongozi hao walijitetea
kwamba wameruhusu kukatwa kwa magogo makubwa kwa mzungu mmoja
waliyemtaja kwa jina moja la Zaboya na kisha watendelea kuutunza kufutia
msitu huo kuvamia na watu wasiojulikana kutoka Kabuku hivyo waliogopa
usitoweke.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Sufiani
aliwatupia lawama viongozi wa CCM wa kijiji hicho kwamba kulega kwao
kiuongozi pamoja na kutofanya vikao ndiko kulikosababisha uongozi wa
kijiji ulaumiwe na wananchi hao na amekiri kwamba hali katika kijiji
hicho kwa sasa siyo swari baada ya kuahidi kuitisha mkutano Jumatano
ijayo.
No comments:
Post a Comment