https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, June 12, 2014

Uchaguzi Mkuu Simba wazidi kuwaka moto, waibuka wa kumpinga Wambura



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
UCHAGUZI Mkuu wa Simba, unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu umeshika kasi, baada ya baadhi ya wanachama wake kujitokeza hadharani na kusema kuwa kumchagua Michael Wambura kuwa Rais wao ni kuiweka kubaya klabu yao hiyo kongwe.

Maneno ya wanachama hao yamekuja siku moja baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kumrudisha tena kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya awali kuenguliwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba.

Akizungumza kwa uchungu, mwanachama mwenye kadi namba 5175, Dk Mohammed Wandwi alisema kuwa Wambura ana matatizo mengi, ikiwapo kuungwa mkono na kundi kubwa la wadau na wanachama wa Yanga SC.

Alisema kuwa anabebwa na wanachama wengi wa Yanga, hivyo anapaswa kuangaliwa upya kwa maslahi ya klabu yao ya Simba.

“Huyu Wambura akishakuwa Rais wa Simba SC, Yanga watanufaikaje, maana tunaona kelele nyingi zinazopigwa kumuhusu zinatoka kwa wapinzani wetu,” alisema Wandwi.
Naye Ras Simba kadi namba 5757 amewataka wanachama wenzake wa Simba SC kumuangalia kwa jicho makini kujihadhari na mkakati unaopangwa na Yanga SC.


“Naona tabu kumuangalia Wambura kwasababu ni dhahiri kuwa anataka kutuweka katika wasiwasi wa aina yake pale atakapotaka kulipa fadhira kwa Yanga,” alisema Simba.

Naye Said Mohammed ‘Bedui’ kadi namba 547 amewasihi wanachama wenzake wa Simba SC waonyeshe mshikamano wao kwa kutompa kura Wambura katika uchaguzi wao ili kudhibiti hujuma kutoka Yanga.

Alisema kuwa Kamati ya Rufani ina wajumbe watatu wa Yanga, ambao walimpigia kura za ndiyo Wambura ili apitishwe kuwa ni Mwenyekiti Lugaziya, Juma Abeid Khamis na Rashid Dilunga, wakati wawili waliomkataa Mwita Waisaka na Masoud Isangu.

Uchaguzi wa Simba unafanyika huku joto la urais likibaki kwa Evans Aveva, Andrew Tupa na Wambura, hasa baada ya kurejeshwa tena kundini kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo kubwa kwa klabu ya Simba.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...