https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Saturday, June 28, 2014

Waajiri Tanzania wapigwa mkwara mzito

 Mkurugenzi Msaidizi  Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu  Bw. Robert Kibona akitoa mada wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini mjini Dodoma leo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini wakifatilia mada mjini Dodoma leo.


Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini imepanga  kuwachukulia hatua waajiri wote nchini kwa kushindwa kuwasilisha taarifa  za wahitimu wa elimu ya juu wanaodaiwa na Bodi hiyo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi  Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu  Bw. Robert Kibona alipokuwa akitoa mada kuhusu
urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa
Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini mjini Dodoma leo.

“Mpaka sasa tumewachukulia hatua jumla ya waajiri watano ambao wameshindwa kuwasilisha taarifa za watumishi wao  wanaodaiwa na
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu” alisema Bw.Robert.


Alisema, mwajiri atakayeshindwa kutoa taarifa za wahitimu wa elimu ya juu katika Bodi kwa wakati atatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni saba au kutumikia kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja. Aidha,Bw. Robert alisema kuwa mpaka sasa takribani waajiriwa 18 wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Bw.Robert alifafanua kuwa ili kufanikisha zoezi la urejeshaji  mikopo kutoka kwa wadaiwa,  Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inatunga sheria na mifumo  mbalimbali ya kuwadhibiti wadaiwa hao. “Tunatengeneza
sheria ambazo zitawazuia wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kupata hati ya kusafiria nje ya nchi au kibali cha kusafiri hadi atakapowasiliana na Bodi.”

Pia,alisema mhitimu atakayeshindwa kulipa mkopo taarifa zake zitatangazwa kwenye vyombo vya habari na kwenye taasisi za mikopo ili asipate huduma yoyote ya kifedha.

Naye, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Dk. Veronica Nyahende amewataka wahitimu wa elimu ya juu nchini kutumia elimu waliyonayo kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa. Alisema
changamoto ya kurejesha mikopo  ni kubwa kwa upande wa wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana kazi ama hawajajiajiri.


“Changamoto iliyopo ni wahitimu kushindwa kulipa mikopo hiyo kutokana na kuwa na kipato cha chini ama kukosa ajira.” Alisema Bodi imeingia mkataba na kampuni zitakazokusanya mikopo kwa walionufaika na
mikopo hiyo na kushindwa kuilipa .

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iko katika mchakato wa kuelimisha umma na watendaji wakuu Serikalini ili kuhakikisha wanawasilisha taarifa za watumishi wao wanaodaiwa mikopo hiyo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...