Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIFANYA utafiti kidogo tu namna vijana wanaojihusisha na
mambo ya kimichezo wanavyoangaliwa, utabaini kuwa leo hii wameanza kuonekana
umuhimu wao. Baadhi yao katika maeneo mbalimbali wameanza kupokea vijizawadi
vya jezi au mipira.
Hata hivyo, vijana hao wameanza kupata zawadi hizo kwa
sababu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Wanaotoa zawadi hizo wanasukumwa na dhamira
zao za kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, iwe ni ubunge au udiwani.
Haya ni matatizo makubwa. Ni matatizo kwa sababu umuhimu wa
vijana hao unaonekana kila mwaka wa uchaguzi. Ingawa tunatambua umuhimu wa
michezo, lakini wadau wamekuwa kimya wakisubiria mwaka wa uchaguzi tu ndio
wajitolee.
Hakika Siwezi kuvumilia kuona siasa zinapewa nafasi kila
wakati hata kwa mambo yasiyostahili kutokana na umuhimu wake. Na wakati
mwingine natamani kuwaambia vijana hao wasisumbuke na watu hao wanaojikosha
katika mwaka wa uchaguzi.
Bali wajiweke mikakati ya kuona vipaji vyao vinawika hata
kama asipotoa mpira mmoja au jezi mwanasiasa asiyekuwa na dhamira ya kukomboa
vijana wanaokufa njaa licha ya kusheheni vipaji vya kucheza soka katika mikoa
mbalimbali.
Hii inakera na kustaajabisha mno. Tanzania imebarikiwa kuwa
na vijana wenye vipaji vya kila aina kama vile ngumi, riadha, mpira wa miguu na
mingineyo. Hata hivyo hatuna mipango ya kuwaendeleza wenye vipaji hivyo.
Tumeendelea kuwa wanasiasa.
Mtu anajiwekeza visenti vyake akijua fika anapotoa jezi seti
mbili au tatu basi ataungwa mkono na makundi ya vijana. Hii haikubaliki. Na
lazima wadau hao, wakiwamo hao wanasiasa kutafuta nafuu ya maisha kwa
wanamichezo wao. Waweke mikakati endelevu kabla ya uchaguzi na hata baada ya
uchaguzi ili faida zao zionekane dhahiri.
Tuacheni kufanya siasa hata pasipotakiwa. Lazima tufahamu
michezo ni ajira. Makundi ya watu wasiokuwa na ajira wanaweza kuishi vyema kama
wataibuliwa na kuendelezwa kutokana na vipaji vyao vya michezo, iwe ni riadha
au mpira wa miguu.
Huo ndio ukweli. Ni wakati huu makundi hayo yakawa makini
kupokea wanasiasa hao wanaoanza kuwaona leo kwa kuwapa jezi za bei rahisi ili
wawachague na bada ya hapo huwakimbia kwa kipindi cha miaka mitano, huku
wakiishi bila kujua kesho yao.
Badala yake watumie nguvu zao na maarifa yao kufanya mazoezi
kwa bidii, pamoja na kutumia fursa zozote wazipatazo, ikiwamo kutafuta timu
zenye dira ili waonyeshe vipaji vyao kwa ajili ya kuwakomboa kimaisha na
kiuchumi.
Kinyume cha hapo, vijizawadi vya jezi au mpira vitaendelea
kuwapatia maisha duni, maana licha ya kuwachagua watu hao, lakini wanashindwa
walau kuanzisha ligi yenye thamani ya Sh 10 tu kwa mwaka ili kuhakikisha kuwa
wanakuwa na Ligi yenye nguvu na ushindani kwa ajili ya kuwapatia mwangaza
makundi ya vijana wanaoamini soka au michezo ndio ajira zao.
Tuone wiki ijayo.
0712053949
No comments:
Post a Comment