Hayati Dkt. Mohamed Mitha Mekuru Genzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi anasikitika
kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu (mstaafu) Dkt. Mohamed Mhita
kilichotokea siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili 2015 katika hospitali ya Agakhan
jijini Dar es Salaam.
Marehemu Dr Mohamed Mhita enzi za uhai wake, aliyesimama, aliyetarajiwa kuzikwa leo jioni wilayai Handeni, mkoani Tanga
Dkt. Mhita alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa
iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa kwa kipindi cha miaka 8 kuanzia 1992 hadi
1999 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kipindi cha
miaka 9 kuanzia 1999 hadi 2008.
Dr. Mhita kwa kushirikiana na uongozi wa
iliyokuwa idara Kuu ya Hali ya Hewa alishiriki katika kuishauri Serikali kuhusu
kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya
Hali ya Hewa.
Pamoja na nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pia
alikuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani
kuanzia mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza Kuu la
Shirika la Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995 hadi 2007.
Alichaguliwa kushika nafasi ya Rais wa
Jumuiya ya Hali ya Hewa katika Bara la Afrika (RA 1) kuanzia mwaka 1998 hadi
2007. Dkt Mhita alikuwa Rais wa ‘Tanzania Meteorological Society’ sambamba na
nafasi nyingine nyingi mbalimbali alizoshika ndani na nje ya nchi.
Akielezea baadhi ya mambo makubwa
yatakayomfanya Dkt. Mhita aendelee kukumbukwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt.
Mhita atakumbukwa kwa mchango wake
mkubwa katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa hapa nchini, katika Bara la
Afrika na Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki wake wa kuianzisha
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na dhamira (mission)
ya Mamlaka kwa kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia mwaka 2000 hadi
2015’.
Dkt. Mohamed Mhita ni mmoja kati ya
wanasayansi waliokuwa zao la chuo kikuu cha Stolkholm, Sweden ambako
alitunukiwa shahada ya hali ya hewa (BSc. Met) mwaka 1977. Kuanzia mwaka 1981
hadi 1984 alikuwa mafunzoni katika chuo Kikuu cha Reading, Uingereza ambako
alitunikiwa shahada ya uzamivu (PhD).
Hapa nchini alipata mafunzo ya Sekondari
katika shule za Tanga na Kamrimjee zote zikiwa mkoani Tanga. Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania inajumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kuomboleza
msiba huu. Innalilah Wainnailaih Rajiun.
Imetolewa na Monica Mutoni
Afisa Mahusiano wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania
No comments:
Post a Comment