Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
wamejitoa katika mbio za kuitwaa nchi hii kwa amani inayojengwa na demokrasia
makini iliyojengwa kwenye nchi yetu.
Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema ambaye kwa sasa ni Kiongozi Mkuu wa Chama kipya cha ACT Tanzania, Zitto Kabwe, akimshawishi dereva barabarani ajiunge na chama chao hicho. Watu wengi wameonyesha kuunga mkono njia hii ya kusaka wanachama inayofanywa na Zitto.
Hii ni kwa sababu wenyewe wameshindwa kusimamia hoja makini,
badala yake wameingia kwenye vioja na vituko visivyokuwa na kichwa wala mguu.
Zaidi, tunashuhudia mtafuruku, kushindwa kuelewana na kuonyeshana tamaa kwa
viongozi au wanachama wenye mvuto na majina kadhaa.
Wakati Chadema wakisisitiza amani na shauku ya kutaka
kuichukua nchi hii, wao wenyewe wamekosa umoja na dhamira ya dhati ya
kuwashawishi Watanzania wenye mlengo wa demokrasia isiyokuwa na ghasia kwa
ajili ya kulinda mustakabali wa Taifa letu.
Kwa kuimba wimbo wa demokrasia, Chadema hao hao waliikosa
katika chama chao, ndio maana wakaamua kuingia kwenye mgogoro mzito na
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao, Zitto Kabwe, waliyeamua kumtimua kama mbwa
koko baada ya kuonyesha nia ya kugombea nafasi ya juu ya uongozi katika chama
hicho Kikuu cha Upinzani kwa sasa.
Kwa kupitia Mwenyekiti wao Taifa, Freeman Mbowe kwa
kushirikiana na ofisi nyingine za Chadema, waliamua kumuwekea zengwe Kabwe.
Alinyukwa kiasi cha kumkatisha tamaa kwenye chama hicho alichoshiriki kukijenga
kwa nguvu zake zote. Inashangaza leo hathaminiki.
Leo hii Zitto amekuwa kiongozi mkuu wa Chama Cha Alliance For
Change and Transparency (ACT), ikiwa ni siku chache baada ya kuvuliwa ubunge
wake kwa madai kuwa alikwenda Mahakamani kukishtaki chama chake cha Chadema,
kama Katiba yao inavyosema.
Hata hivyo, huo ni mchezo uliwekwa kwa ajili ya kumuondoa
kundini. Kwenye siasa suala la kuhujumiana ni jambo la kawaida. Wenyewe
wanasema hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu.
Hayo na mengine mengi, utagundua ni mwendelezo wa ishara ya
kuwa ngoma ya kitoto haikeshi. Ilikuwa lazima Chadema ianguke. Hakukuwa na njia
ya kuwanusuru hususan kwa mwaka huu wa Uchaguzi. Ukiacha suala la Zitto ambaye
mwelekeo wake unaonekana kuwa ni mwiba mkali kwao. Amekuwa akiungwa mkono na
Watanzania wengi.
Tumeshuhudia umati wa watu ukifurika katika mikutano yake
iliyofanyika Mkoani Ruvuma, Njombe, Dodoma na Morogoro. Makundi ya watu
wamekuwa na shauku ya kumuona Zitto akihutubia kwa kauli mbiu ya ACT Wazalendo.
Aidha, Chadema wenyewe na Chama Cha Wananchi (CUF)
wanaonekana kunyukana chini kwa chini kufuatia majina na majimbo waliyopanga
kuachiana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Majimbo kadhaa yamekuwa machungu nay a moto. Wanachama hao na
vyama vyao vilivyojiunga kwenye Muungano wa UKAWA havielewani. Majimbo kama
vile Morogoro Mjini, Mikumi, Segerea, Ukonga, Kigamboni yameonekana dhahiri
kutaka kuvunja muungano huo.
Kule wilayani Handeni duru zinaonyesha kuwa msuguano upo kati
ya CUF na Chadema. CUF wanasema wao wanapaswa kusimamisha mgombea maana ndio
chama chenye nguvu ukitoa CCM.
Lakini Chadema nao wanaona wao ndio wenye uwezo wa kuisumbua
CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Huu ni mtihani mkubwa kwa wapinzani,
hususan hawa waliojiunga kwenye kivuli cha UKAWA.
Vyama kama vile Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD kamwe
hawawezi kuisumbua tena CCM kwa mwaka huu. Vyama hivi vitasumbuana vyenyewe
ndani ya muungano wao wa UKAWA. Baada ya hapo, watasumbuana tena na wapinzani
wenzao kama vile ACT ya Zitto, ADC ya Hamad Rashid Mohammed ambaye naye
anaonyesha kugombea urais Visiwani Zanzibar.
Huu ni zaidi ya moto. Ni zaidi ya ngoma ya kitoto kwa
Chadema. Chama hiki kilichokuwa na nguvu kutoka kwa makundi ya vijana,
kimeyumba baada ya kukubali kuyumbishwa na viongozi wao.
Hili lazima lisemwe. Na kuna kila sababu Watanzania, hususan
wale wanaopenda vyama vilivyokuwa kwenye mgongo wa UKAWA wakajiandaa
kisaikolojia. Kamwe CCM haitatumia nguvu kubwa kushinda kwenye uchaguzi huu.
CCM itashinda kiulaini kabisa.
Hakuna kiongozi wa juu wa Chadema, CUF atakayekubali mgombea
wa ACT ashinde katika uchaguzi huu. Ikitokea hilo, watakuwa tayari kumsaidia
mtu wa CCM kushinda. Hii inaitwa ‘bora tukose wote tuheshimiane’.
Na wataheshimiana kweli. Zitto huyu wanayemsema na
kumdhalilisha mchana na usiku, kamwe hayupo tayari kuona Chadema na wenzao wa
UKAWA wanamshinda, hivyo atafanya kila awezalo kuona nao wanaanguka katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wafurukutwa wa vyama hivyo wajiandaye. Na wajiandaye pia
kupokea matokeo ya kushindwa kwa minajiri ya kulinda usalama wa nchi yetu.
Hakuna kinachoweza kuwafanya washinde na kushika dola.
Mpaka sasa hawajui nani atasimama kwenye kiti cha urais kati
ya Dkt Willbroad Slaa na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Hawa wote wana nguvu
kwenye vyama vyao. Na wote wanaheshimika katika nchi hii.
Pamoja na heshima hiyo,ili kofia ya UKAWA ikae sawa kichwani,
lazima asimamishwe mmoja kwa ajili ya kugombea urais na kuchuana na wagombea
wengine kutoka CCM nk.
Huo ni mwiba mwingine wa UKAWA. Kelele zinazopigwa kwa sasa
ni Slaa anafaa zaidi ya Lipumba au Lipumba anafaa zaidi ya Slaa. Ukiangalia
vigezo wanavyotoa vinaelemea kwenye udini, ukabila au uvyama vyao. Watu hao
hawatumii vigezo husika kwa maslahi ya Tanzania, bali vyama.
Hii haiwezekani. Ni katika hilo, bado nabaini kuwa vyama hivi
ni kama vile ngoma ya kitoto kamwe haiwezi kukesha. Watapambana sana,
watachuana mno, ila mwisho wa siku, hawana madhara.
Bado wana safari ndefu ya kuweza kuifanya CCM kiwe chama cha
upinzani katika nchi hii yenye kila zuri la kujivunia. Huo ndio ukweli wa
mambo. Kama wapinzani hao, hususan Chadema wangekuwa na nia njema ya kuwa
wapinzani wa kweli, kamwe wasingeleta chuki na ubinafsi wao kwa wao.
Leo hii wametunga wimbo wao wa msaliti. Wanamtukana sana
Zitto. Wanamdhalilisha mno Zitto. Wanamdhalilisha mtu ambaye Watanzania wengi
walionza kufuatilia siasa mwaka 1995 hadi leo wanamuona wao ndio kiongozi wao
mwenye uzalendo kwa Taifa lake.
Jambo hili linazidi kuwa chungu kwa Chadema, maana wengi wao
wanajua alionewa aidha kwa kabila lake au udini wake. Ikumbukwe kuwa, wapo watu
waliomtetea Zitto wakisema alizuiwa kugombea uenyekiti kwa sababu yeye si
Mchaga wala Mkristo.
Jambo hili linaweza kuwa si kweli, ila kwa sababu linatolewa
dhidi ya mtu aliyefukwa kwenye chama hicho, basi aghalabu baadhi yao wanahisi
kuna ukweli ndani yake.
Sidhani kama huu ni mwendo mzuri kwa siasa za Tanzania. Ni
dhahiri vyama visivyokuwa na dira vinaendelea kupiga jaramba hali ya kuwa
hawana uwezo wa kuwa na madhara dhidi ya CCM. CCM inayoheshimika kwa wakubwa na
wadogo.
Inayopendwa na wake kwa waume. Lolote wanalotaka kulisema
leo, litawekwa katika kundi la ngoma ya kitoto isiyokesha. Je, Chadema
wanafahamu makosa yao? Wanaojiita wana UKAWA wanajua mapungufu yao? Kwamba bado
wanajiamini kuwa wataiondoa madarakani CCM kwa mwaka huu 2015? Kwa lipi?
Si kweli, hivyo Watanzania wote wajipange kulinda amani ya
nchi yetu kwa kujiandaa kisaikolojia, hususan wale waliokuwa na mtazamo kuwa
huenda kuna chama cha upinzani kinaweza kushinda katika uchaguzi wa mwaka huu,
ambao tayari unaonekana CCM itashinda.
+255 712 053949
No comments:
Post a Comment