Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI wakati wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal
Malinzi kukaa chini kwa ajili ya kuangalia namna ya kuendeleza soka letu na si
kuonyeshana ubabe na wadau wengine waliokuwa ndani ya sekta hiyo au vinginevyo.
Hii ni kwa sababu mpango huo unaweza kuibua ari na maendeleo
ya soka, kuliko ilivyokuwa sasa, hususan mgogoro mzito uliokuwa ndani ya
Shirikisho hilo kwa Damas Ndumbaro kuonekana kama vile anawekewa kauzibe.
Soka letu la Tanzania limeshindwa kumea kutokana na wakati
mwingi kuwaza siasa zisizokuwa na tija kwa namna moja ama nyingine. Mara zote
hakuna mipango kamili ya wadau, wakiwamo viongozi wa soka au wengineo kuibua
vipaji vya vijana wetu.
Wanaoibua vipaji hivyo basi ni wale wanaosubiri mwaka wa
kampeni kama ulivyokuwa huu, ndipo wanapojihusisha na michezo, hususan huu
mpira wa miguu. Hapo ndipo nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia, maana
naelewa namna gani tutadumazwa.
Mpira wa miguu ni ajira. Watu wengi duniani wameendelea
kimaisha kutokana na kulipwa fedha nyingi kutokana na kucheza mpira wa miguu.
HJata hivyo wana michezo hao ingawa wametumia zaidi nguvu zao na maarifa yao,
ila pia wametumia juhudi za wadau.
Nchi zao zimejipambanua vizuri kuhakikisha kwamba kila mmoja
kwa nafasi yake anatimiza wajibu wake na sio kama Tanzania inayoendeleza soga.
Kila mtu akiingia kwenye madaraka ya mpira wa miguu anajaribu kuwawekea wengine
kauzibe.
Tulishuhudia hili kwa Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa
chama cha Mpira wa Miguu Tanzania FAT sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Michael Wambura anavyobanwa kila anapojaribu kuingia. Wakati
tunatafakari namna ya kuondoa kasumba hiyo, Malinzi tena kwa kushirikiana na
kamati zake, anajaribu kumfungia Ndumbaro kujihusisha na soka kwa miaka 2.
Hakika siwezi kuvumilia. Nikajua sasa Malinzi atashirikiana
na kila mmoja ili kuona soka letu linapiga hatua na si vinginevyo. Huu ni
wakati wa kuangalia upya nyendo zetu. Dosari na vijisababu vya kukomoana si
wakati wake.
Kinyume cha hapo tutazidi kudumaa wakati nchi za wenzetu
zinapiga hatua na vijana wao wanawika ndani na nje ya nchi zao.
Tuonane wiki ijayo
+255 712053949
No comments:
Post a Comment