Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU
ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars wanajua nini wanachokitaka Watanzania.
Wanafahamu kuwa Watanzania wamekuwa na kiu kubwa ya kushiriki au
kufanya vizuri katika michuano mikubwa ikiwamo ile ya Afrika.
Kwa
bahati mbaya, timu ya aina hiyo kwenye mpira wa miguu hamna, hususan
zile timu za wanaume ambazo mara kwa mara zinaambulia patupu. Licha ya
kuambulia patupu, lakini watu wamekuwa na matumaini nao, kiasi cha
kuwaunga mkono mara kwa mara.
Wanajitahidi kuingia uwanjani kwa
wingi au hata kumwaga udhamini wao mnono huko kwa minajiri ya kuwaunga
mkono. Kwa Twiga Stars hapana. Hapa ndipo ninaposhindwa kuvumilia.
Ona
sasa, Twiga Stars wamefanikiwa kufuzu michuano mikubwa ya Fainali za
Mataifa Afrika kwa Wanawake (AWF 2015) zitakazofanyika baadaye mwaka huu
nchini Congo-Brazzavile, baada ya kuwafunga She-Polopolo kwa mabao 6-5.
Awali
Twiga Stars walishinda bao 4-2 nchini Zambia na juzi Ijumaa katika
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, walifungwa bao 3-2, hivyo Twiga
kufuzu kwa kufanikiwa kupata ushindi wa bao 6-5.
Huu ni ushindi
wa Watanzania wote, wakiwamo wale wanaoshindwa kuwaunga mkono akina
Sophia Mwasikili, Fatuma Rashidi na wengineo wanaoitangaza vyema nchi
yetu kwa kupitia soka la wanawake.
Huo ndio ukweli. Twiga Stars
wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuonyesha kiu ya mafanikio ya soka,
jambo linalohitaji kuigwa na kaka zao, Taifa Stars au hata timu za
Tanzania.
Ikumbukwe Twiga wanafanya vizuri kwa jitihada zao.
Hawana Ligi nzuri kama ilivyokuwa ile ya Vodacom. Tangu enzi za kocha
wao Boniface Mkwassa hadi leo Rogasian Kaijage, wachezaji wanafanywa
kuokotezwa tu kisha wanaingia kwenye timu ya Taifa.
Ni wakati
huu wadau wa soka kuzidi kushangazwa na matokeo ya mabinti hawa wa Twiga
Stars, ikiwezekana wawaunge mkono kwa namna moja ama nyingine ili
kuwapa nguvu zaidi.
Wachezaji wa soka la wanawake wawekewe mkazo
kuwaibua na kuwaendeleza zaidi na zaidi kwa maendeleo yao. Soka la
wanawake liwe na dira, ikiwamo ya kuwaingizia kipato wachezaji kuliko
ilivyokuwa sasa.
Kinyume cha hapo tutaishia kuangalia soka la
wanaume lisilokuwa na tija kwa mechi za Kimataifa, huku wale
wasioangaliwa wakisonga mbele mara kwa mara, hivyo kuwa aibu yao au aibu
yetu?
Tuonane wiki ijayo
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949
No comments:
Post a Comment