Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, ameitakia kila la kheri timu ya Taifa
ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) katika mchezo wake wa kesho wa marudaino
dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo) utakaochezwa Uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Azungumza na wachezaji wa
Twiga Star na benchi la Ufundi katika chakula cha pamoja cha mchana leo katika
hosteli za TFF zilizopo Karume, Rais Malinzi amesema watanzania wote wana
matumaini na timu yao kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa marudiano.
Aidha Rais Malinzi
amewaambia bechi la ufundi na wachezaji wa Twiga Stars kuwa pesa zote
zitakazopatikana katika mchezo wa kesho baada ya makato ya Uwanja na VAT,
wagawane kwa pamoja wachezaji na viongozi.
Naye Mgeni mualikwa Ryhs
Torrington ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Luninga cha Azam, alisema
anaitakia kila la kheri Twiga Stars katika mchezo wao wa kesho, na kusema mechi
hiyo itaonyeshwa moja kwa moja na Azamtv, hivyo waitumie vizuri nafasi hiyo
kujitangaza kimataifa.
Kocha mkuu wa Twiga
Stars Rogasian Kaijage na nahodha wake Sophia Mwasikili, wamewahakikishia
ushindi katika mchezo wa kesho, na kuwaomba watanzania kujitokeza kwa
wingi uwanjani kuja kuwashangilia.
Mechi inatarajiwa kuanza
majira ya saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, na tiketi za mchezo
zitauzwa kesho saa 2 asubuhi eneo la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku
viingilio vya mchezo huo vikiwa ni tsh. 5000 kwa VIP na tsh. 2000 kwa majukwaa
yaliyobakia.
Twiga Stars ambayo
katika mchezo wa awali iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, inahitaji sare ya aina
yoyote ili kuweza kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanyika
nchini Congo-Brazzavile mwezi Septemba.
No comments:
Post a Comment