https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, October 24, 2012

MGODI UNAOTEMBEA




Washindi chaguzi za CCM, wapime viatu vyao


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAGUZI za ndani za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimekuwa zikiendelea huku kukiwa na malalamiko mengi ya rafu kutoka kwa baadhi ya wagombea. Wapo wanaolalamika juu ya kufanyiwa mchezo mchafu, ukiwamo kumwaga fedha kwenye uchaguzi wao.

Malalamiko hayo yamekuwa yakisemwa baada ya uchaguzi au kabla, jambo ambalo hata hivyo ni kawaida katika chaguzi zenye upinzani na ushindani wa wagombea.

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
 
Kwa mfano, juzi katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wapo watu waliolalamika kuwa kuna kundi likikuwa likitoa rushwa chooni, ikiwa ni muendelezo wa vituko vilivyotokea kwa wingi kwenye uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma.

Kituko kingine cha aina yake ni purukushani iliyoibuka baada ya mwanachama wa CCM, ambaye pia Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy Rose Bhanji, alipomuuliza mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba namna ya kuitumikia nafasi yake ipasavyo na kwa manufaa makubwa ndani ya chama chake hicho.

         Siphia Simba, mwenyekiti UWT

Majibu ya Simba inaonyesha hayakumfurahisha Shy hasa aliposema kuwa bado ni mchanga kisiasa na hajui watu wanavyofanya. Ni majibu mepesi katika uchaguzi mzito unaotingisha nchi nzima, hasa jumuiya hiyo, ambayo kila mtu anaifuatilia.

Ikumbukwe kuwa, ndani ya CCM yenyewe, uchaguzi wa jumuiya hiyo ulikuwa na nguvu kiasi cha kutingisha makundi mawili ambayo yalikuwa kati ya Simba na Anne Kilango.

                             Shy Rose Bhanji, mbunge wa Afrika Mashariki
 
Kila mtu alikuwa akiamini kuwa ana ari na sababu ya kuongoza kiti hicho, ambacho ni dhahiri kina manufaa makubwa na chama chao.

UWT endapo inatumika vizuri, inaweza kutangaza sera za chama pamoja na kuwavuta akina mama wengi zaidi kwenye chama chao pamoja na kuwabakiza waliopo kwa kunadi vitu vya kimaendeleo ama kuwaunganisha wanawake Tanzania Bara na Visiwani.

Ni kwa kulijua hilo, naamini sasa kuna haja ya washindi wa chaguzi za ndani za chama hicho, kujipima kama viatu walivyovaa vinawatosha. Nimekuwa nikilisemea hili katika makala zangu mara kwa mara kwa ajili ya kuijenga CCM imara.

Nimekuwa pia nikiikosoa mwenendo wowote mbaya ndani ya CCM, ikiwamo rushwa, ingawa wachache wao wanashindwa kunielewa na kuanza kunitumia meseji zisizokuwa na kichwa wala miguu kwa sababu wanazojua wenyewe.

Ukiacha nafasi za mwenyekiti wa Mkoa, wilaya, mweka hazina au Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, chaguzi za jumuiya za CCM ni nyeti na zimeanza zamani mno.

Umoja wa Wanawake Tanzania pamoja na Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), ulianzishwa zamani, huku Bibi Titi Mohamed akiwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja wa wanawake Tanzania.

Kwa mujibu wa historia na harakati za CCM, tangu wakati huo inaitwa TANU, jumuiya hizo ziliundwa kwa ajili ya kukiweka chama hicho katika hali nzuri, sambamba na kuwavuta wengine, mfumo ambao hadi leo umeendelea.

Kwa bahati mbaya, nyakati za leo, mambo yamekuwa yakibadilika kutokana na wanaopewa nafasi hizo, baadhi yao kutokuwa na jipya. Ni watu ambao viatu wanavyolilia kupewa na chama, haviwatoshi.

Kwa wale wanaojua adha ya kuvaa vatu visivyokutosha, iwe kidogo au kikubwa, watakubaliana na mimi kuwa ni mbaya mno. Ndio maana nasema, walau sasa wale ambao wameshapata bafasi hizo za chama, wajiangalie tena.

Wajipime wenyewe kama kweli wanaweza kuwa na mchango na CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Wameingia madarakani katika kipindi kigumu mno. Kipindi ambacho fikra za watu wengi zinaamini enzi za CCM zimekwisha.

Kipindi ambacho wakati wao wanawania nafasi hizo, wengine wanapita chini chini kujaribu kutafuta namna ya kupenyeza watu ambao baadaye iwe turufu kwao. Hizi ni dalili mbaya kwa CCM, hasa kama watu hao wamefanikiwa.

Ni wakati sasa wa Viongozi wa CCM Taifa, akiwamo mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete na wenzake kukaa na kuwapima kwa vitendo washindi wao. Hili sio baya likifanywa na CCM, maana lengo ni kuwaweka sawa.

Kama walitoa sera zao mbele ya wajumbe na wapiga kura wao katika uchaguzi huo wa ndani, basi waseme pia namna ya kukisaidia chama ili kiende sambamba na presha ya vyama vya upinzani vyenye hamu ya kuongoza dola.

Ni dhahiri CCM ipo kwenye kipindi cha hatari. Kama juhudi zisipochukuliwa, dalili za kuanguka katika uchaguzi mkuu ujao ni kubwa. Hili lisemwe hata kama watu wachache halitawafurahisha.

Wale waliozea kusifiwa au kudanganywa kuwa mambo yapo vizuri, wakati hali ni mbaya na jamii imekuwa ikiweka chuki za wazi wazi kwa viongozi wa ndani wa chama na wanachama wao kwa ujumla.

Kwa mfano, kampeni za kuwania nafasi za udiwani katika baadhi ya maeneo zimekuwa zikiendelea kwa vyama kuwania viti hivyo. Ingawa wakati wa kura bado, lakini matokeo katika chaguzi hizo pia ziwe kipimo cha CCM.

Wanachama na viongozi wa CCM wasikubali kuweka viongozi ambao kwa miaka mitano hawatakuwa na mchango wowote. Wasiwe viongozi wa kukaa ofisini tu, au wafanya kazi kwa simu, wakizungumza kwa  wao.

Viongozi wa chama, kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa wapende kuzungumza na wananchi ambao hao ndio walengwa wakuu. Wazungumze na wapiga kura, ambao hao ndio watakaokuwa na kazi moja ya kuibakisha CCM madarakani au kuimwaga.

Kama hivyo ndivyo, basi tuanze kwanza kuangalia uhalali wa nafasi za chama na kuangalia pia viatu vya washindi ili wajipime pia utendaji wao katika kipindi cha uongozi wao.

Najua wapo watakaohoji sababu hiyo ukizingatia kwamba asilimia kubwa ya viongozi wameshapatikana, ila huko kushinda, ndio iwe sababu ya wao wenyewe kuangalia namna ya kuongoza kwa manufaa na CCM.

CCM wilaya, mkoa na Taifa hili lazima walijuwe ili chama kibaki salama katika Uchaguzi Mkuu ujao, utakaofanyika mwaka 2015. Uchaguzi ambao huenda ukawa mchungu sana kwa CCM, maana watu wengi, wakiwamo vijana ambao ndio wapiga kura, wamekuwa na hasira na chama hiki kikongwe na kutamani kukiweka kando.

Wapinzani wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali, zikiwamo za mikutano katika maeneo tofauti, jambo ambalo CCM nao lazima walijuwe.

Wasikae kucheka, kuwaona wapinzani ni majuha, wakati elimu ya uraia inasambazwa kwa kasi ya ajabu na watu wanaanza kujua wajibu na haki zao za kuongozwa na vyama tofauti na CCM.

Nasema hili bila kuangalia wale rafiki zangu wanaonisema au kunitukana. Wale ambao nia yao haswa watu tubaki kimya, tuchekee matatizo ya CCM, ili iwe nafasi ya kuanguka katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Nalisema hili pia bila kuangalia wanachama wangapi wa CCM na viongozi wake watanikosoa, wakisema makala yangu yameegemea kukichafua. Huo ndio ukweli. Daima hauwezi kuwafurahisha kila mmoja duniani.

Sitarajii kukaa kwa bashasha na kusubiria kuwafurahisha kila mmoja, maana katika Dunia hilo jambo sio rahisi. CCM wajiangalie katika kipindi ambacho chama kimewaona wanafaa hivyo nafasi zao lazima ziwe na tija kwa chama.

Yale makundi hasimu za wagombea yavunjwe na wanachama wote wawe kitu kimoja, bila kuangalia aliyeshinda au aliyeshindwa. Bila hivyo, makundi hayo pia yatazidi kuwa mwiba mchungu kwa chama hicho, ndio maana ninahoji uhalali wa viatu vya watu hao.

Huo ndio ukweli, ikiwa ni mwelekeo wa mwisho mwisho katika chaguzi za Chama cha Mapinduzi zenye joto kali katika wilaya na mikoa mbalimbali, huku kila mtu akiona ana kila sababu ya kuwa kiongozi wa chama, ingawa lengo lake haswa linashindwa kujulikana, hasa eneo lake linapotawaliwa zaidi na upinzani siku baada ya siku.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...