https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, October 19, 2012

MAMBO FULANI MUHIMU


Mpe moyo, usimkatishe tamaa

              Wawili wapendanao.

MAMBO FULANI MUHIMU 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI dhahiri kila mtu ana mapungufu yake katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi.

Sio wote ni wajuzi wa mambo. Sio wote wanaelewa wapi kwa kuwashika wenzao, hadi wajisikie raha katika suala la mapenzi.

                                                     Kambi Mbwana, Mwandishi wa Safu hii
Kila mtu na utundu wake. Wapo ambao ni wazito kabisa, wakikosa mbinu nzuri zinazoweza kustawisha mapenzi yao kwa wale waliowapenda.

Ndio, maana watu hao husubiri hulka na utundu wa wenzao tu, wakitaka waendeshwe kwa kila hatua. Waambiwe simama, inuka, lala au fanya hivi!

Bila kuendeshwa, kamwe hawawezi kung’amua wenyewe na kubuni yale yanayoweza kuwapa raha wenzao. Hayo ndio ya kujadili leo.

Naamini nitaweza kutoa darasa japo kwa kiasi kidogo, huku nitarajia kujibu maswali yako, hasa kama sitaingia moja kwa moja, kutokana na sababu za kimaadili, maana gazeti linasomwa na watu wengi, wakubwa na watoto.

Nimeamua kusema haya, huku nikijua fika, ingawa baadhi yao ni wazito, lakini wachache wao hupenda kujifunza na kuwagurahisha wapenzi wao.

Ni kutokana na hilo, kuna kila sababu ya kuwapa moyo, pale tutakapogundua kwamba kwa siku hiyo, wapenzi wetu wamejituma, kukazana na kufanya yale yaliyotupa raha na amani katika uhusiano wetu.

Tusiwanyanyase na kuwaona bado ni mizigo. Tuone kama walioamua kuwa na sisi kwa raha na tabu, ndio maana wanaamua kujitoa kwa moyo.

Kuna watu ambao hujikuta wakitoa matamshi makali kwa wapenzi wao. “Huna lolote, bado mgeni kwenye ulimwengu wa mapenzi na mengineyo.

Kuna mtu aliwahi kulalamika juu ya jambo hili. Dada huyo alisema, “sijawahi kusifiwa hata siku moja na kila siku naambiwa sifai”.

Kwa sababu hiyo, dada huyo alijikuta akihoji labda hayupo moyoni kwa mwanaume huyo, ambaye kwa hakika yeye amempenda na kuamua kujitoa kwake.

Sawa, lakini hapa udhaifu upo kwa mwanaume. Nasema hivyo, maana hajui harakati na jinsi gain wasichana wanatakiwa kupikwa kadri unavyotaka wawe.

Haya utayafanya siku chache baada ya kuingia naye kwenye makubaliano ya kuanzisha mapenzi, hivyo hakuna haja ya kuwaona si lolote si chochote.

Kama wewe ni hodari wa mapenzi, pia una wajibu wa kuelewa, si wote ni wajuzi, huku pia ukiwa mwepesi wa kumsifia mwenzako katika siku zote za uhusiano wenu, hasa kama amefanya kitu cha tofauti.

Kama leo unaona kabisa mpenzi wako amefanya jambo geni, kwanini usimsifie ili aongeze bidii? Haina haja ya kumuona mgeni kila wakati.

Kama mabadiliko yapo, ni wakati wako wa kuona kumbe uliyekuwa naye, angalau anaumiza kichwa, kuwaza namna ya kukutosheleza.

Anafanya hivyo maana hataki akukose. Hataki kuona unakuwa na uhusiano mpya kila wakati, ukizingatia kwamba wapo wanaoanzisha uhusiano mpya kwa kisingizio kuwa wapenzi wao, wake au waume zao hawawatoshelezi katika mambo fulani muhimu.

Huo ndio ukweli wa mambo, Tunapaswa kuwa makini kwa ajili ya kulinda, kudumisha na kustawisha uhusiano wetu, maana hapo ndipo utamu wa mapenzi unapoanzia na kushika kasi siku zote.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...