https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, October 14, 2012

‘Bebaneni mkichoka mtaacha’


 
 
SIWEZI KUVUMILIA
 
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HUWEZI kumkataza mtu asitumie nafasi yake kufanya kile anachokipenda katika tasnia ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu. Kila mtu anafanya kile anachokiona kwa manufaa yake na marafiki zake anaokula nao.
 
Katika hilo, hata kama watu wawe wakali vipi, lakini itatungwa sababu, uongo wa kila aina kusafisha au kusawazisha kinachopingwa na wadau wao. Kwangu mimi nasema, bebaneni mkikochoka mtaacha na kuendelea na maisha mengine.
 
Nayasema haya kwa uchungu mkubwa baada ya watu kulazimisha maji yapande mlima. Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodgar Tenga, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa elimu kwwenye kuongoza soka sio lazima.
 
Tenga anayasema haya huku akijua wanachama wao wengi, wamelazimika kusimamisha chaguzi zao, au kusogeza mbele ili wabadilishe katiba zao kwa ajili ya kuingiza kipengele cha elimu ya kidato cha nne kuingizwa.
 
Wengi wamekutana na kadhia hii. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amekumbana nayo na kuachia nafasi yake ya uongozi wa Simba. Lakini leo hii kwakuwa kuna mtu anahitajiwa, ulazima huo unafutwa.
 
Tenga amelazimika kusema haya maana TFF inamuhitaji mgombea wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Amini Bakheresa. Bakheresa amekuwa akiwekewa pingamizi na wadau mbalimbali wa michezo.
 
Hata hivyo, wanaomuwekea pingamizi hushindwa baada ya watu wenye nafasi zao kuingilia kati kwa ajili ya kubebana. Ndio maana nasema, kwangu mimi siumizwi na suala hilo la kuwasaidia marafiki zenu, ila sioni haja ya kipengele cha elimu kuwa hoja.
 
Vinginevyo waheshimiwa watajizalilisha tu. Tenga na jopo lake la TFF linajipaka kinyesi, maana hawawezi kuwakataza wachache na kuwaruhusu wengine. Tangu mwanzo, sikuwahi kukubali mabadiliko ya katiba ili kuingizwa kipengele cha elimu.
 
Nilifanya hivyo kwakujua uongozi hausomewi kamwe. Uongozi ni kipaji na sio kila mtu anaweza kuwa viongozi. Nilifanya hivyo kwakuangalia viongozi wengi mahiri katika Taifa hili ambao hawak,uwa na elimu kubwa.
 
Hata kwenye soka, Dalali aliongoza kwa  mafanikio makubwa akiwa Simba. Aliweza kuipa ubingwa timu yake bila kufungwa hata mechi moja. Lakini kipengele cha elimu kikamuondoa, tena kwa kubarikiwa na TFF.
 
Leo hii vipi DRFA wembe huo usitumike? Kuna nini hapo kwenye ofisi za TFF na DRFA? Aibu hii itakwisha lini? Hakika siwezi kuvumilia. Aidha, iwekwe wazi kuanzia sasa kuwa yoyote anaweza kuwa kiongozi hata kama akiwa hana elimu ya kidato cha nne.
 
Kila mwenye uwezo huo wa kuongoza, apewe nafasi na sio kwa watu wachache. Nalisema hili hadharani, maana kuna siku kutatokea mkanganyiko wa kiuongozi na kuzua balaa. Hili linawekwa kwenye kumbukumbu na vizazi vijavyo watalifanyia kazi.
 
Hakika siwezi kuvumilia na nitaendelea kusubiri wenye mtazamo wao, harakati zao na wanaotaka kuweka kumbukumbu sawa kuwa wakali zaidi katika hilo.
 
Kwakuwa mimi sina nia yoyote ya kuwania nafasi hiyo kwa sasa, pia siwezi kulia wala kucheka ninapoona sheria hazifuatwi, maana najua fika hata niseme vipi, wakubwa hao wakiamua lao hakuna wa kuwazuia, ndio maana mbeleko yao kwa maswahiba zao zipo pale pale.
 
Tena kwa dharau tele. Eti wanasema kelele za chura hazimnyimi tembo kunywa maji na dua ya kuku haipati mwewe. Haya bwana nyie endeleeni kubebana hadi mtakapochoka wenyewe na kuanza kufuata sheria na taratibu mlizoweka wenyewe.
 
Tukutane wiki ijayo.
 
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...