https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Friday, November 27, 2015

Turudie uchaguzi Zanzibar ili wananchi wampate wanayemhitaji, iwe ni Dk Shein au Seif

ILI uwe rais unahitaji kuwa na wananchi. Wananchi ndio kila kitu. Hawa ndio wanaopaswa kupiga kura ili wakuchaguwe wewe kwa ajili ya kuwaongoza. Na inafahamika kwamba uongozi ni kuonyesha njia. Ikiwa uamuzi wao ni wewe kuwa rais wao, watafanya hivyo. Ikitokea upande mmoja hautaki, basi demokrasia ikifuatwa, watamchagua yule yule wampendaye. Kama hivi ndivyo, kwanini Zanzibar isirudie Uchaguzi wao baada ya ule wa awali kufutwa kutokana na matatizo kadha wa kadha? Wafuasi wa CCM wanaamini Dk Ali Mohamed Shein angeshinda kama sharia zingefuatwa. Maalim Seif Sharrif Hamad naye anasema alikuwa mshindi na ndio maana akajitangaza kama rais mpya wa Zanzibar anayesubiri kuapishwa tu.
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kushoto, akisalimiana na Maalim Seif Shariff Hamad, katika matukio yaliyowakutanisha mara kadhaa nchini Tanzania.
Kwa nini alitangaza? Si kwa sababu aliamini Wazanzibar wanamuhitaji? Kama wanamuhitaji, hapana shaka watamchagua tena hata uchaguzi ukifanyika usiku wa maneno. Sitaki kuamini kuwa kurudia kwa uchaguzi kutamfanya Seif ashindwe wakati anaamini alishinda kwa kura nyingi. Na siwezi kuamini kwamba Shein aliyeshindwa katika uchaguzi huo uliyofutwa atashinda, wakati wananchi ni wale wale. Kurudia kwa uchaguzi, mshindi atakuwa yule anayependwa na kuhitajiwa na Wazanzibar wenyewe.
Hivyo basi, bila kujali vyama vyetu, dini zetu, koo zetu au elimu zetu. Shime Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla tunapaswa kuafikiana na kurudia uchaguzi huo ili wapiga kura waamue wenyewe, kidemokrasia tu. Hakuna mbora kati ya Shein na Seif. Mbora ni Mzanzibar mwenyewe. Kamwe tusisikilize maneno ya waropokaji. Tujali zaidi udugu wetu, uhusiano wetu na nchi yetu. Turudie uchaguzi huu kwa Amani. Aliyechaguliwa na Mungu kuwa kiongozi wetu atakuwa tu, hakuna wa kumzuia. Wewe kama ni mfuasi wa CUF, kipende zaidi chama chako, ila mwisho wa siku jenga uzalendo pia kwa nchi yako. Na ikiwa ni Mwana CCM, unapaswa kujua bila nchi hakuna chama chako cha siasa. Hivi kwa mfano tukianza kugombana, kutoana roho, hao tunaowapigania watamuongoza nani? Na je, wote tunaweza vita? Wote tunaweza kupaa angani kujihifadhi katika nchi za wenzetu kama watakavyofanya wanasiasa tunaotaka kuwapigania?

Si kweli. Kundi kubwa litaangamia. Na zaidi ni wale wenzangu na mimi wanaoaminishwa uchaguzi haupaswi kurudiwa kwa kuwa Seif ni mshindi, wakati wanajua fika hakuna Tume ya Uchaguzi iliyotangaza matokeo ya Uchaguzi huo wa Zanzibar. Twende mbele na kurudi nyuma. Tumekaa mezani, tumeafikiana kurudia uchaguzi, wasioafiki waambiwe waafiki ili matokeo halali ya uchaguzi huo yapatikane kwa ajili ya kuipatia maendeleo Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukiona una hasira, hutaki uchaguzi urudiwe, jifungie ndani ili uzuie hasira zako zisichochee fujo wala vurugu wakati Wazanzibar wanaamua kwa ridhaa yao kurudia uchaguzi wao kama sehemu ya kujenga mfumo bora wa kiutawala.
Asante
Kambi Mbwana,
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
@MGODI UNAOTEMBEA

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...