TANGAZO
Tamasha la Utamaduni la NSSF Handeni Kwetu limefanyika Handeni Mjini mara mbili mfululizo, mwaka 2013 na 2014. Tamasha hili limefanyika kwa mafanikio makubwa. Limeendelea kupokea wageni na vikundi mbalimbali hata nje ya wilaya ya Handeni. Mipango iliyokuwapo ni kulifanya tamasha liwe na mvuto kwa kuhakikisha kwamba linaandaliwa vizuri zaidi. Mwaka huu mwanzoni tulipokea maoni kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), wakisema kulingana na hadhi ya tamasha la NSSF Handeni Kwetu, kibali chake kinapaswa kutoka BASATA na si Halmashauri tena. BASATA walisema hivi kama taratibu za matamasha makubwa yanavyofanyika.
Hili limetupa moyo mkubwa. Mwanzo tuliamini hatutaweza, ila tumeweza. Wakati sisi tunaona ni tamasha dogo, kumbe wadau wakubwa wa sanaa wanajua ni tamasha kubwa. Bahati iliyoje? Vyuo mbalimbali vya sanaa vimekuwa vikifundisha wanafunzi wao kwa kupitia tamasha la NSSF Handeni Kwetu, hususan lile la mwaka 2013. Ni kutokana na kiu ya kulifanya tamasha hili liwe na mvuto mkubwa zaidi, mwaka huu halitafanyika. Hii ni kwa sababu mwaka huu ulijawa na matukio mengi makubwa, ukiwamo Uchaguzi Mkuu.
Si kwetu tu, ila kwa wadau mbalimbali. Kutofanyika kwa tamasha hili si kigezo cha kusema NSSF Handeni limekufa. Yapo matamasha mengine ambayo mwaka huu hayajafanyika.
Naomba hii iwe taarifa rasmi kuwa tamasha hili kwa mwaka huu halitafanyika, ila kutofanyika kwake mwaka huu ni sehemu ya maandalizi ya mwaka 2016. Maandalizi yake yatakuwa bab kubwa mno. Tutakuwa tunaambizana hatua kwa hatua. Tamasha la mwakani litakuwa na matukio tofauti tofauti. Kilele cha tamasha hili kitashangaza wengi. Tunatamani tamasha la mwakani liwe kubwa zaidi, ukizingatia kuwa kupata kibali cha BASATA, ndio kusema wataalamu wao watakuwa bega kwa bega na sisi. Tunatamani pia NSSF Handeni Kwetu iwe zaidi ya siku moja. Tunatamani pia tamasha hili lizidi kupokea wageni kutoka nje ya Tanzania ili kuchochea maendeleo. Tunafanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza, ikiwamo sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali. Tunatamani tamasha lijalo liwe la utamaduni na biashara pia.
Kwa walioathiriwa na kutofanyika kwa tamasha hili msimu huu wa 2015 tunatoa pole. Tunawaomba wajipange kwa mwaka ujao. Na tunaamini kuwa watafurahia zaidi. Msimu ujao wa NSSF Handeni Kwetu 2016 utakuwa wa aina yake.
By Kambi Mbwana, Mratibu Mkuu
kambimbwana@yahoo.com
0712053949
No comments:
Post a Comment