https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Sunday, November 29, 2015

LADHA ZA WASANII WETU: Mwana wa Kitwana, wimbo wa kimahaba kutoka kwao Jagwa Music

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Muziki aina ya mnanda ni kati ya aina ya muziki uonekanao ni wa kihuni.  Ingawa upo muziki wa Bongo Fleva ambao nao unaitwa wa kihuni miaka ya 2005 kushuka chini, ila huu wa mnanda umezidi. Na kuonekana kwake ni muziki wa kihuni unatokana na aina ya mashabiki wake na jinsi wanavyojiweka. Muziki wa mnanda una nguvu sana. Unapopigwa mtaani, basi unaweza kukuta mashabiki wake wametoka Bagamoyo na maeneo mengine ya mbali kabisa. Na idadi kubwa ya watu hao ni wale wanaojihusisha na vitendo vya uhuni. Kwa mfano, ni rahisi kuona mtu anakwenda kuangalia muziki huo mtaa Fulani huku akiwa na burungutu la bange au dawa nyingine za kulevya.
Na wadau hao hutumia hadharani. Kwa wanaofuatilia muziki huu watakubaliana na mimi, hususan katika ngome za muziki huu kama vile Tandale, Mwananyamala, Kigogo, Mbagala na kwingineko unapopita mara kwa mara wanapoalikwa vijana hawa. Binafsi ni aina ya muziki niupendao sana. Naupenda mno muziki wa mnanda. Na kuupenda kwangu kumetokana na jinsi ya uimbaji wao. Wasanii wanaoimba muziki wa mnanda wa asili ni wenye vipaji kupita kiasi. Aidha licha ya kufanya kazi zao katika wakati mgumu hususan uhaba wa vyombo vya muziki, lakini nyimbo zao huwa nzuri sana.
Huyu ni mmoja wa wapiga vyombo wa muziki aina ya mnanda. Anaonekana anapiga kisturi.

Unaweza kushangaa kwenye shughuli wanakuja na spika ndogo, kinanda kidogo na hutegemea kuazima meza, kisturi au vinginevyo ili kupiga na kuchanganyia muziki wao. Katika video ya wimbo uitwao Mwana wa Kitwana kutoka kwa kundi la Jagwa Music watakubaliana na mimi. Ni wimbo mzuri na video iliyochangamka sana. Katika video hiyo marehemu Sharo Milionea amecheza kama Mwana wa Kitwana ambaye ni masikini, lakini anampenda msichana mzuri aitwae Jokate Mwigelo. Na Jokate pia anapendwa na Yusuf Mlela, anayeonyesha kuwa anajimudu kiuchumi.

Jamaa hawa wanavutana sana, lakini mwisho wa siku Sharo milionea anaonekana kushinda vita hii, kwa sababu msichana mwenyewe anampenda. Mashairi yanasisimua, hasa pale msanii anaposema “umenifanya niwe jasiri mbele yao sasa mimi ni jabali”. Kuna sehemu pia anasema, “umeonyesha huwa mind na tena hauna mpango nao”.  Pia mwanzo alionyesha hofu kidogo pale alisema kwamba mwanzo wa mapenzi yao waliamua kufanya iwe siri, hii ni kwa sababu mapenzi yao yalizunguukwa na vikwazo vingi, hususan ugumu wa maisha. Jagwa wanasema, “Moja ya vikwazo choka mbaya na hali duni niliyokuwa nayo mimi ohoo”. Baada ya kulalamika sana, akilalamikia upendo wake na ugumu wake wa maisha, anaingiza maneno matamu yenye kutia moyo kwamba hatokatishwa tamaa, bali atakaza uzi mpaka awe pamoja na mrembo huyo.

Ni mashairi mazuri ya ushindi. Mtu anapokuwa anafuatilia msichana mzuri, lazima kuwe na changamoto kadhaa. Hii ni kwa sababu vizuri vinapendwa na wengi.  Omba sana Mungu. Pia jaribu kuchunguza, unayempenda ana ndoto na wewe? Katika kuchunguza upendo wako, usiangalie hali yako ya mfukoni, ila angalia thamani ya moyo wako. Katika kusikiliza wimbo huu, najifunza mengi sana. Lakini pia nafarijika mno. Je, umewahi kupata muda wa kuhudhuria shoo za muziki wa aina ya mnanda? Mimi nimewahi, ni muziki mzuri mno unaovutia kusikiliza hata kuangalia wanavyocheza wahusika. Mnanda bwana, hata ukiruka ruka kachura umekwenda na biti. Ukichuchumaa na kulia, inapenda zaidi.
Ukikimbizana na mwenzako ndani ya eneo la muziki huo ndio kwanza inapendeza. Wengine wanacheza taratibu kama hawataki vile, aisee acha tu. Tatizo lao ni moja tu. Wengi wanaona bila kulewa bange au gongo hawajacheza. Na wale wengine ndio kabisa, hatari. Wenzao wanacheza wao wapo vichochoroni wanakaba wapiti njia, kisa, wapo kwenye mnanda. Hii haikubaliki. Wadau wa mnanda tuambiane. Kila mmoja awe mlinzi wa muziki huu. Tuhamasishane kuhakikisha kwamba tunafanya uhuni wetu nje ya muziki wa mnanda na sio ndani yake.
Tukifanya hivyo, muziki wetu utasonga mbele. Hebu pata muda wa kuyasoma mashairi ya wimbo huu wa Mwana wa Kitwana uone utamu wake.
…………………..Muziki uonekanao wa kihuni, wenye mashairi mazito na ujumbe wa kutisha


Tumelazimika tufanye siri na mimi na wewe demu ohoo
Tumelazimika tufanye siri mimi na wewe demu ohoo
Katika haya mapenzi yetu yaliyozungukwa na vikwazo vingi ohoo
Katika haya mapenzi yetu yaliyozungukwa na vikwazo vingi ohooo
Moja ya vikwazo choka mbaya na hali duni niliyokuwa nayo mimi ohoo
Moja ya vikwazo choka mbaya na hali duni niliyokuwa nayo mimi
Sitokatishwa tamaa mimi ohooo mwana wa kitwana nitakaza uzi mpaka tuwe pamoja
Sitokatishwa tamaa mimi ohoo mwana wa kitwana nitakaza uzi mpaka tuwe pamoja
Mimi na wewe, najua wapo wela wela wanaotutolea macho
 najua wapo wela wela wanaotutolea macho
Mimi naomba tuwapotezee hao, sitokatishwa tamaa
Mimi ohoo mwana wa kitwana, nitakaza uzi mpaka tuwe pamojaaa

Ubeti wa pili
ulivipuuza vishawishi vya wale wenye pesa
Ulivipuuza vishawawishi vya wale wenye pesa
Umeonyesha huwa mind na tena hauna mpango nao
Umenionyesha huwa mind na tena hauna mpango nao
Umenifanya niwe jasiri mbele yao sasa mimi ni jabali
Umenifanya niwe jasiri mbele yao sasa mimi ni jabali
Sitokatishwa tamaa mimi ohoo mwana wa kitwana nitakaza uzi mpaka tuwe pamoja
Sitokatishwa tamaa mimi ohoo mwana wa kitwana nitakaza uzi mpaka tuwe pamoja
Twende kazi, nachoma sana, mwanamume hasifiwi kula bwana
Weka ndoo kinga ndoo
Meneja Kwame, tupo pamoja na wewe, mwanzo mpaka mwisho
Eheeeeee Eheeeeee, habari ndiyo hiyo, habari ndiyo hiyo
Wafile wantu wasigale wantu
Waliokufa watu tumebakia watu ehee
Na watu ndio kama sieeee
Kila shetani ana mbuyu wake na kila ndege hutua kwenye mti wake
Kila shetani ana mbuyu wake na kila ndege hutua kwenye mti wake
Mimi na wewe, mimi na wewe ahaaaa
Sitokata tamaa, sitokata tamaaa ahaaa
Mimi na wewe, mimi na wewe ahaaaa
Sitokata tamaa, sitokata tamaaa ahaaa
Moja, mbili, tatu, ahaaa
Nyie wa wapi, sie wa hapa hapa
Mnapatikana wapi, tunapatikana Mwananyamala
Twende kaziiiiiiiiiiii, Olalaa, cheza cheza, cheza, choma choma
Wazee wa kuchoma, choma sasa
Bakora bado zinaendelea, hata wakinuna, tunacharaza tu
Moja, mbili, tatu
0712 053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...