Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
NI Dr John
Pombe Magufuli tu, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila kona anatajwa
yeye. Kwenye usafiri wa umma, daladala na mabasi anatajwa yeye. Kwenye
maeneo ya huduma za kijamii kama vile hospitali, shuleni na kila kona
anazungumziwa yeye. Hii inaonyesha ni dalili njema za kukubalika kwa mwanasiasa
huyo ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa rais wa Tanzania. Kutajwa kwa
Magufuli kumetokana na kuanza vema katika ngwe yake ya uongozi, akifanyia kazi
kwa vitendo yale aliyozungumzia kwenye kampeni zake, akiwa mgombea urais wa
Tanzania, kwa kofia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli, pichani.
Siku chache
tangu alipoingia madarakani, Magufuli amepiga marufuku safari za nje ya nchi
kwa viongozi wa serikali ili serikali yake kuokoa mabilioni ya shilingi
yaliyokuwa yanatumika katika kugharamia safari. Mbali na
hilo la safari, pia amezuia sherehe za Siku ya Uhuru, 9 Desemba, akiamini kuwa
ni njia ya kuokoa pesa. Awali Magufuli alitangulia pia kuzuia pesa za wabunge
zilizotengwa kwa ajili ya sherehe yao. Jambo hili
na mengine linatia moyo mno. Angalau sasa watu wanaweza kupata picha ya namna
gani Dr Magufuli ataiongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa. Ni kutokana
na hilo, naamini Dr Magufuli anastahili pongezi naa kuungwa mkono pia kwa
aliyozungumza na hata yale asiyozungumzia pia. Kwa mfano, asilimia kubwa ya
Watanzania wanaishi vijijini.
Na watu wa
vijijini wanaishi kwa kutegemea kilimo. Kama hivyo ndivyo, kazi ya kilimo
haiwezi kukamilika kama hakuna ardhi ya kutosha. Maeneo mengi ya nchi, hususan
vijijini kumekuwa na shida kubwa ya ardhi.Vigogo na
wafanyabishara wamekuwa wakigawana ardhi kubwa, jambo linalowafanya wananchi
masikini wakose maeneo ya kulima. Hili halikubaliki. Serikali ya Magufuli
ilifanyie kazi suala hili kwa vitendo. Ndio alionyesha kulipinga wakati wa
kampeni zake, ila kwakuwa ameshafanikiwa kuwa rais, ni wakati wa kulitatua. Utumike
utaratibu mzuri wa kuipima ardhi na kufanya utafiti ni kwa kiasi gani ardhi
imeporwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa walalahoi. Tunajua si wote
wameipora, ila pia wapo waliofanya hivyo. Tuwajue wanaomiliki ardhi kihalali na
wale waliojimilikisha wenyewe.
Wapo watu
wanaomiliki heka zaidi ya 120 na bado wanaingia kwenye vieneo vya walalahoi.
Kesi nyingi za ardhi zinazoendeshwa vijijini zinaishia kwa masikini kuonekana
wana makosa. Hili linasikitisha. Namna gani Dr Magufuli ataungwa mkono? Nadhani ili
suala hilo lifanyiwe kazi kwa vitendo, ni wakati wa Wakuu wa Mikoa kujipanga
kikamilifu. Kila Mkuu wa Mkoa asimamie kuundwa kwa Kamati ya Ardhi katika
wilaya husika. Kamati ya Ardhi iwe na wajumbe mchanganyiko, akiwamo Mkuu wa
wilaya na Mkurugenzi. Kamati hii na Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wake kadhaa.
Kamati hii iwe na mamlaka ya kutembelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya
husika kuchunguza, kusikiliza kero za ardhi. Kamati hii pia iwe na mamlaka ya
kutatua kero ndogo ndogo. Baada ya
kukamilisha utendaji kazi wake, Kamati hii itawasilisha kwenye Kamati ya Ardhi
ya Mkoa, ambayo hapana shaka Mwenyekiti wake anaweza kuwa Mkuu wa Mkoa husika,
ambapo baadaye itawasilisha mezani kwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais.
Utaratibu huu utumike katika kila wilaya na Mkoa.
Tukifanya
hivi, tunaweza kunusuru muda na gharama za maisha kwa Watanzania. Tunashuhudia
miji na majiji makubwa yakipokea wageni wengi wanaotoka vijijini kwao. Ujio wa
watu hao hususan vijana unadai kuwa katika maeneo yao hakuna ajira, maisha
magumu. Ni kweli
wanaishi maisha magumu. Ikiwa unaishi vijijini na huna eneo la kulima, utaishi
vipi? Vijana hao ambao wengi wao ni nguvu kazi ya Taifa, wanaingia katika miji
na majiji ili kutafuta maisha yao. Acheni waje tu. Kama hatupendi waje mijini,
basi wapatiwe ardhi, walime. Tunaambiwa kwamba kilimo ndio uti wa mgongo. Kwa
Tanzania ya leo, kilimo hakiwezi kuwa uti wa mgongo. Watalimaje?
Hakuna ardhi, pembejeo. Wanaolima wanatumia nguvu kubwa na mavuno ni hafifu.
Wataalam wa kilimo nao wapo ‘busy’ na maisha yao. Hatuwezi kufika. Tunapaswa
kujitazama upya. Wapi tunapotoka na wapi tunataka kwenda kama nchi.
Tuwe na
mipango imara kama tunataka maendeleo. Natambua, tukiwekeza kwenye kilimo,
walau tutakuza uchumi wetu. Kila mtu atakuwa na sehemu ya kumuingizia kipato
katika maisha yake. Si kama ilivyokuwa sasa. Mtu yupo kijijini, ila hana eneo
la kulima.
Katika
kuliangalia suala la ardhi na migogoro yake, maeneo mengi imesababishwa na
viongozi wa vijiji husika. Wameuza ardhi bila kuangalia athari wanazoweza
kupata watoto wao miaka michache ijayo. Viongozi hao wameshindwa pia kutambua
sera ya ardhi inayoelekeza namna gani wanapaswa kutoa ardhi kuanzia heka 50 kwa
mtu binafsi, kampuni au shirika. Hali hiyo imewafanya wauze ardhi yao kama
njugu. Na wilaya zinazoongoza kwa matatizo haya ni Handeni na Kilindi, mkoani
Tanga. Katika kila
Kata za wilayani Handeni wananchi wanalia. Mtu mmoja ana heka nyingi zilizokaa
tu. Miaka 20 ijayo, wananchi wa Handeni wataanza kukodisha ardhi kwa walioingia
kwa wingi na kuinunua ardhi yao kwa fedha za chai. Mapungufu haya na mengine
yamulikwe. Tufanye tathimini ya ardhi yetu. Ipigwe marufuku kuuza ardhi.
Serikali Kuu
itoe amri kurudisha ardhi inayomilikiwa na watu wachache. Hii inawezekana. Mtu
anayemiliki heka nyingi, basi aachiwe heka 50 na zinazoongezeka wapewe wananchi
wasiokuwa na mashamba ili walime. Na wananchi hao watakaopewa ardhi hiyo,
wapigwe marufuku kuiuza kwa watu wengine. Na mtu
anayemiliki heka 50 na asiyezilima, abakiziwe heka 10 hadi 20. Utaratibu huo
utakuwa mchungu kwa wachache lakini ni mtamu kwa wengi. Itakuwa ni funzo na
mpango wenye tija kwa wananchi.
Binafsi
naamini hili linawezekana. Ni kuamua na kufanyia kazi kwa vitendo. Utendaji
mwema na ushirikiano kwa watendaji wa serikali na wananchi husika jambo hilo
linawezekana. Huo ndio ukweli wa mambo.
Kama
nilivyosema hapo juu, wasimamizi wa kwanza wa suala hilo la kuokoa ardhi iwe
kwa Wakuu wa Mikoa na wilaya. Kwa mfano, Mkuu wa Wilaya ndio Mwenyekiti wa
Ulinzi wa Usalama wa wilaya husika. Hivyo anapoingia kwenye harakati hizo ni
jambo la busara. Najua ni kiasi gani suala la migogoro ya ardhi ni zito, ila
hatuna jinsi. Wengi wanaomiliki ardhi kubwa si watu wadogo. Wana ukwasi. Na
pengine wana mtandao mpana. Hata hivyo
sidhani kama nguvu za mabeberu hao wa ardhi zinaweza kufanikiwa, maana suala hilo
litaendeshwa na serikali. Ilikuwa kwenye ahadi za mgombea urais. Na hata baada
ya kushinda, ameendelea kulizungumzia jambo hilo kwa nguvu kama kawaida yake.
Aungwe mkono. Apewe ushirikiano wa kutosha. Kila mtu afanye kazi yake kwa
vitendo ili miaka miwili ijayo, kila mtu awe na eneo la kulima kwa ajili ya
kumuingizia kipato.
Kwanza
wapate ardhi ya kulima, kisha wapewe elimu ya namna bora ya kulima kwa
mafanikio badala ya kuendelea kulima kwa mazoea, jambo linalowafanya washindwe
kupiga hatua miaka nenda rudi. Asichekewe wala kuonewa huruma yoyote
anayemiliki ardhi kubwa wakati wananchi wanakosa maeneo ya kulima. Wawekezaji
walioyageuza mapori ni vichaka vya kufuga nyani wamulikwe. Wapo
waliokwenda vijijini na kununua heka nyingi za ardhi kwa gia ya kulima, kumbe
ni kukata mkaa. Baadaye wakapata kibali cha kusafisha shamba, wakakata mkaa,
wakapakia kwenye magari na kwenda kuuza. Shamba likaachwa. Serikali ianze na
hao kwanza.
Kwa bahati nzuri, wananchi wana Imani kubwa na serikali ya Dr
Magufuli. Huu ndio wakati mzuri wa kuwafanya wananchi wajivunie na serikali yao
kwa kusimamia kila lenye tija kwao. Kinyume cha
hapo hakutakuwa na jipya. Dhihaki zitaendelea. Serikali itaonekana ya kujuana,
kuchezeana kiasi cha kuwafanya wananchi washindwe kusonga mbele, huku utendaji
kazi wote wa Dr Magufuli ukionekana si lolote wala si chochote.
0712053949
No comments:
Post a Comment