https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Sunday, December 13, 2015

Ziara za kushtukiza zashika kasi, Waziri wa Afya na Naibu wake wavaa vibwebwe

IMG_8379
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akiwasili katika Hospitali ya rufaa ya Amana iliyopo Ilala, Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza baada ya sherehe za kuapishwa.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).

Na Rabi Hume, Modewjiblog
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala ikiwa ni masaa machache tangu kutoka kuapishwa na Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Wizara hiyo. Mhe. Ummy aliwasili katika hospitali ya Mwananyamala, majira ya saa 8 mchana na kuanza kuzungumza na wananchi mbalimbali waliokuwa wamekaa eneo la hospitali hiyo kuhusu matatizo yanayowakabili pindi wanapofika hospitali hapo kupatiwa huduma ambao wengi wao walionekana kutoridhishwa na huduma wanazopatiwa wanazozihitaji.
Mmoja wa wananchi ambao alielezea kwa masikitiko yaliyomkuta pindi alipofika hospitalini hapo ni, Bi. Khadija Meso ambaye alisema kuwa walikuwa na siku tatu tangu wamefika hospitalini hapo ambapo walikuwa wamempeleka mtoto wao ambae alikuwa anaumwa lakini alikuwa hapatiwi huduma hali imeyopelekea kupoteza maisha kwa mtoto huyo. Mwingine aliyezungumza aliyejitambulisha kwa jina la Mama Madohoro alisema kuwa anashangazwa na hospitali ya rufaa kuwatoza wazee pesa licha ya sera ya afya kusema wazee na watoto chini ya miaka 5 kupatiwa bure huduma za kiafya.

Alisema kuwa alimpeleka hospitalini hapo ndugu yake mwenye umri wa miaka 90 ambae alikuwa akihitajika kulipia vipimo vilivyo na gharama kubwa huku vya gharama ndogo akipatiwa bure na kutokana na uwezo mdogo wa kifedha alionao ukapelekea kupoteza maisha yake kwa mgonjwa huyo. Nae Othaman Rwambo alimuomba Mhe. Waziri kuwa ajaribu kuzungumza na wauguzi wa hospitali hiyo kutokana na kutoa majibu machafu kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
IMG_8386
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akikagua vyumba vya madaktari baada ya kuona mlundikano wa wagonjwa wakisubiri huduma.
Alisema kuwa kasi ya rais wa awamu ya tano ni kufanya kazi na wao kama watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuwahudumia watanzania na kuwataka watumishi hao kuweka uzalendo mbele kuliko maslahi binafsi.
Akiwajibu wananchi hao pamoja na kuelezea sababu ya ziara yake, Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa amefika hospitalini hapo ili kujua changamoto zinazowakabili wananchi lakini pia kujifunza ni kitu gani ambacho wananchi wanahitaji kuboreshewa katika sekta ya afya.
Alisema kuwa matatizo aliyoyakuta ni changamoto kwake na wizara yake na watakaa kama wizara kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua matatizo yanayojitokeza katika hospitali hiyo na kuutaka uongozi wa hospitali hiyo kumaliza matatizo yaliyo ndani ya uwezo wao ndani ya siku 3.
“Mambo ambayo nimeyakuta hapa ni kujifunza na kuona ni hali gani wanakumbana nayo wananchi wanapokuja kupata huduma za kiafya lakini pia kwangu ni changamoto lakini kwa kasi aliyonayo rais wetu wa awamu ya tano hatuna budi na sisi kuwa na kasi hiyo na mimi napenda kuwaambia wananchi wanaopata huduma katika hospitali hii tutatatua matatizo yanayowakabili,
“Nimeupa uongozi wa hospitali kazi ya kumaliza matatizo yaliyopo wanayoweza kuyamaliza kama neti kwenye wodi kama ile ya wajawazito, na hata mambo ya feni kwenye wodi za wanaume na mengine tutakaa kama wizara kuyajadili tuone jinsi gani tutayamaliza,” alisema Mhe. Ummy.
IMG_8392
Mh. Naibu Waziri, Dkt. Hamis Kigwangala akiingia katika chumba cha X-Ray kuangalia utendaji wa kazi unavyoendelea.
Aidha Mhe. Waziri alisema siku ya Jumatano wanatarajia kutambulisha namba ambayo wananchi watakuwa wanaitumia kutoa taarifa wizarani kuhusu kero wanazokutana nazo hospitalini wanapokwenda kupata huduma za matibabu.
Nae Naibu Waziri wa Wizara hiyo ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufaa ya Amana na kukuta baadhi ya huduma za afya katika hospitali hiyo zikiwa zimesimama kwa sababu mbalimbali.
Baadhi ya matatizo ambayo amekutana nayo hospitalini hapo ni pamoja na kutokuwepo kwa mtoa huduma katika chumba cha Utra Sound, Ubovu wa mashine ya kuchunguza matatizo yaliyopo mwilini (MS4S) na kubakia moja ikifanya kazi ambayo inachukua muda mrefu kutoa majibu.
Matatizo mengine ambayo amekutana nayo ni uchache wa vitanda, kutokupatikana kwa dawa katika duka la hospitali huku maduka ya nje ya hospitali zikipatikana na kutokuwepo kwa baadhi ya watumishi ofisini kukiwa ni muda wa kazi.
IMG_8395
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akizungumza na mtoa huduma katika chumba cha X-Ray ambapo aliridhishwa na utoaji huduma wa mtumishi huyo.
Akizungumzia matatizo hayo alisema kuwa kuna uzembe umekuwa ukifanyika kwa baadhi ya watumishi hali inayofanya hospitali hiyo kuwa na wagonjwa wengi bila kupatiwa huduma na badala yake wanawapa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Tunachotaka ni kuona wananchi wanapata huduma, nimefika hapa nakuta hata chumba cha Utra Sound anaehusika hayupo na hata wagonjwa wakija hawatapata huduma na kinachofata hapo wanampeleka Muhimbili ndiyo maana Muhimbili imejaa wagonjwa kumbe sababu ni uzembe uliopo huku kwenye hospitali za rufaa,” alisema Dkt. Kingwangala.
Aidha Mhe. Naibu Waziri ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kufika wizarani siku ya jumatatu saa 10 jioni ili kupewa maelekezo jinsi ya kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi na kwenda sawa na kasi ya rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye anahitaji kuona serikali yake ikifanya kazi kwa kuhudumia wananchi.
IMG_8404
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akizungumza na baadhi ya wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma wanazopata hospitalini hapo ambao wengi wao hawajaridhishwa na utendaji wa wahudumu wa zamu wa siku hiyo.
IMG_8408
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akizungumza na mmoja wa Daktari (ambaye hakutaka sura yake iyonekane) kuhusu utaratibu wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaosubiri huduma hizo.
IMG_8425
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akimuulizia Kiongozi wa zamu katika ofisi za mapokezi ya hospitali hiyo.
IMG_8433
Muuguzi Kiongozi wa Hospitali ya rufaa ya Amana, Bupe Mwakalenge akijibu maswali ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu kutokuwepo kwa baadhi ya Madaktari katika baadhi ya vitengo.
IMG_8475
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akitazama moja ya cheti cha mgonjwa aliyekuwa akilalamika kusubiri kwa muda mrefu bila kupatiwa huduma.
IMG_8498
Mwanasayansi wa Maabara ya Hospitali ya rufaa ya Amana, Jabir Mukhsin (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Dkt. Hamis Kigwangala kuhusu ubovu wa mashine inayotumika kufanya vipimo mbalimbali (MS4S) ikiwemo mzunguko wa damu mwilini ambayo kwa sasa imeharibika na kubakiwa na mashine moja ambayo ufanyaji wake wa kazi unachukua muda mrefu kutoa majibu sahihi.
IMG_8517
MS4S Mashine ambayo imeharibika.
IMG_8525
Mmoja wa wagonjwa waliokuwepo wakisubiri huduma ya kipimo cha MS4S akimwelezea Mh. Naibu Waziri kuhusu kutokufanyika kwa kipimo hicho licha ya kuwa hospitali wamepokea malipo yake ya kufanyiwa kipimo hicho.
IMG_8542
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akionekana kushangwazwa na jambo fulani wakati akiendelea na ziara yake hospitalini hapo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Gideon Malabeja.
IMG_8550
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akiwa nje ya chumba cha Ultra-sound ambacho kimefungwa kufuli licha ya maelezo ya Muuguzi Kiongozi wa Hospitali hiyo Bi. Mwakalenge kuwa mashine hiyo ni nzima na haina tatizo lolote.
IMG_8590
Muuguzi Kiongozi wa wagonjwa wa nje, Francis Itima akimwelezea Mheshimiwa kuhusu changamoto ya upungufu wa vitanda katika wodi ya wakina mama waliojifungua.
IMG_8599
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akikagua wodi ya watoto ambayo aliridhishwa na hali iliyopo katika wodi hiyo.
IMG_8611
Mfamasia wa zamu katika hospitali ya Amana, Anna Kajiru akimpa maelezo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala kuhusu upungufu wa dawa uliopo katika duka hilo la dawa hospitalini hapo.
IMG_8614
Baadhi ya wananchi wakipatiwa huduma ya dawa katika duka la dawa lililopo hospitalini hapo.
IMG_8667
Pichani juu na chini ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala akitoa mrejesho kwa waandishi wa habari kuhusu ziara yake ya kushtukiza, matatizo yanayoikabili hospitali hiyo na hatua ambayo wizara itachukua.
IMG_8691

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...