https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, December 19, 2015

Wizi wa simu za mikononi, simu feki wafikia tamati, TCRA waja na mwarobaini wake nchini Tanzania

TAARIFA KWA UMMA
MFUMO WA RAJISI YA NAMBA ZA UTAMBULISHO WA SIMU ZA KIGANJANI (CENTRAL EQUIPMENT IDENTIFICATION REGISTER (CEIR)
UTANGULIZI:
Vifaa vya mawasiliano vya mkononi – hususan simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) – vina namba maalum inayovitambulisha. Namba hiyo inajulikana kama IMEI ambacho ni kifupi cha International Mobile Equipment Identity.
Kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka kuwepo kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Rajisi hii inajulikana kwa kiingereza kama Central Equipment Identification Register, kwa kifupi CEIR. Sheria inataka rajisi hiyo ihifadhiwe na kuendeshwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Aidha Kanuni za mwaka 2011 za EPOCA kuhusu mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi inawataka watoa huduma wa mawasiliano yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi (Equipment Identity Register – EIR) za vifaa vya mkononi vinavyotumika kwenye mitandao yao.  Mfumo huu wa kielektroniki ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano. Vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza kufanya kazi kwenye mitandao ya mawasiliano kutumia vifaa vya mkononi.

UFAFANUZI
Taarifa kwenye mfumo huu wa rajisi zitakuwa na aina tatu za kumbukumbu; ambazo ni orodha ya namba tambulishi ambazo vifaa vyake vinaruhusiwa, orodha ya namba tambulishi ambazo zimetolewa taarifa kuwa zimefungiwa na namba tambulishi ambazo zimefungiwa kwa muda au kuruhusiwa kwa muda.
Orodha Nyeupe:  Orodha ya vifaa vya mkononi vya mawasiliano vinavyoruhusiwa kutumika katika mitandao ya huduma za simu za kiganjani
Orodha Nyeusi:  Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa na mtoa huduma kwenye mfumo wao wa EIR na kutumwa kwenye mfumo wa CEIR kwa ajili ya kufungiwa ili zisitumike kwenye mitandao mingine ya simu za kiganjani kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na kukubaliwa miongoni mwa watoa huduma. Simu zote za mkononi zilizoibiwa au kupotea zitafungiwa ndani ya saa 24 ili zisitumike kwenye mtandao wowote wa simu za mkononi Tanzania.  Ikitokea simu ya mtumiaji ikafungiwa kinamosa, anatakiwa kutoa taarifa mara moja kwa mtoa huduma wako kwa ajili ya kuifungua. Watoa huduma wanatakiwa wafungulie, ndani ya saa 24, simu zote zilizofungwa kimakosa.

Orodha ya kijivu:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa au kufunguliwa kwa muda kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuzifuatilia.
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya angalau miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.
2. Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea ( risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo). Mtoa huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa 24.
3. Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.
KUTAMBUA NAMBA TAMBULISHI
Ili kutambua namba tambulishi ya simu ya kiganjani au vifaa vya mawasiliano ya kiganjani, mtumiaji anatakiwa aandike tarakimu *#06# kwa kutumia kifaa chake. Baada ya kufanya hivyo, kutaonekana namba ndefu. Mtumiaji anatakiwa kuandika namba hiyo kama ilivyoonekana kwenye kifaa chakena kuihifadhi katika hali ya usalama kwa ajili ya rejea ya baadae.
Baada ya hapo mtumiaji atume ujumbe mfupi wenye hiyo namba tambulishi kwenda namba 15090. Atapokea meseji itakayomjulisha kuhusu hali halisi ya simu yake ya kiganjani. Mtumiaji atapokea ujumbe kuhusu uhalisia wa simu yake. Majibu yatakayokuja yatasomeka: Kama IMEI haioani na aina ya simu yako, wasiliana na aliyekuuzia. Usipoweza,ibadilishe kabla ya Juni 2016 kwani simu hiyo inaweza kuwa BANDIA.
Watumiaji wanaweza pia kuhakiki uhalisia wa simu zao za kiganjani kupitia tovuti ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa kuandikahttp://www.tcra.go.tz/index.php/imei-code-verification
HATUA ZA KUCHUKUA IWAPO SIMU ITAONEKANA HAIKIDHI VIWANGO, SI HALISI NA NI BANDIA
Mtu yeyote ambaye atatambua kwamba simu yake ya kiganjani si halisi,ni bandia na haikidhi viwango atapewa muda wa kuendelea kutumia simu hiyo. Baada ya muda huo kumalizika, simu hiyo itaingizwa katika orodha nyeusi na kufungiwa isitumike kwenye mitandao mingine yoyoye ya simu za kiganjani.
Watumiaji wote wenye simu za kiganjani ambazo namba tambulishi zao zinaonyesha kwamba simu hizo si halisi, ni feki na hazikidhi viwango watagharamia ununuzi wa simu nyingine. Watumiaji wote ambao namba tambulishi za simu zao zinaonyesha kwamba vifaa hivyo si halisi, ni feki na havikidhi viwango watatakiwa kubadilisha simu hizo na kupata zinazokidhi viwango na halisi katika muda wa miezi sita kuanzia siku ya uzinduzi wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa simu za kiganjani.
Ni vyema ifahamike kwamba simu zote za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) ambazo zitakuwa na namba tambulishi bandia zitafungiwa kuanzia 16 Juni 2016.
HITIMISHO
Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets). Uanzishwaji wake ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010. Ni vyema watumiaji wakazingatia maelekezo kuhusu utaratibu wa kuhakiki namba tambulishi, kutoa taarifa wanapopoteza au kuibiwa simu.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
18 December 2015

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...