https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Wednesday, December 16, 2015

Kwa hili la shamba la mkonge la Kwamdulu Estate, nakubaliana na wanaosema kwamba masikini hana haki

Na Kambi Mbwana, Handeni
Wakati mwingine viongozi wetu wanashindwa kutumia busara kufanya uamuzi wenye tija kwa Taifa na wananchi wake. Angalia, nimekuja Kata ya Segera, Kitongoji cha Kwedihangala, wilayani Handeni, mkoani Tanga, nilipopata taarifa kwamba wananchi wamevunjiwa nyumba zao na wawekezaji wa shamba la Mkonge la Kwamdulu Estate, linalopita katika vijiji kadhaa vya Korogwe na Handeni. Wananchi hao waliovunjiwa nyumba zao wameishi hapo tangu mwaka 1982. Shamba lenyewe halilimwi. 

Kampuni yenyewe imevunja mkataba, maana shamba ni la mkonge na wao eti wanataka walime mitiki. Kwa jinsi shamba lilivyokuwa kubwa, kampuni haitaweza kulilima lote hadi walipokuwa wananchi hao. Mwekezaji anaamuru wananchi wahame ndani ya siku 90 kwa madai wanataka kulima mitiki, wakiogopa kauli ya serikali ya kutaifisha mashamba yasiyolimwa na wawekezaji uchwara. Siku 90 zinaisha, wanatumwa vijana kuanza kuvunja nyumba za walalahoi hawa, masikini wanaoishi kwa kutumia jembe la mkono. 

Nimekuja hapa, nimeumia, haswa baada ya kusikia kwamba viongozi wa wilaya ya Handeni wamewataka wananchi hao wahame kama walivyohamia hapo. Huu ni ujinga wa karne. Ningekuwa mimi ni Mkuu wa wilaya ya Handeni, ningezungumza na mwekezaji huyo badala ya kuhamisha wakulima hao, wangewamilikisha heka japo mbili au tatu ili waendelee kulima na kujenga Taifa lao. Kitendo cha kuwataka wahame, wakiwa na mazao yao, mihogo au msimu huu wa kilimo ni kuwasumbua na kuwadhalilisha wananchi hawa. 

Mkuu wa wilaya, Mkurugenzi, Diwani na viongozi wengine wa chama na serikali wanashindwa kuwa upande wa wananchi badala yao wapo upande wa mwekezaji aliyeshindwa kuilima ardhi yetu. Hii si haki. Serikali iliangalie upya suala hili. Wananchi hawa wapewe japo mwaka mmoja au miwili ili wajiandae kuhama sanjari na kuhamisha rasilimali zao. Wana watoto wanasomesha. Wameshiriki mengi ya kimaendeleo kama michango ya zahanati, shule, maabara za sekondari wakitambuliwa kama wananchi halali katika eneo hilo hilo moja. Je, serikali haikujua udhaifu huo?
Hivi msimu huu wa kilimo, hata kama wananchi hao wakihama, watakwenda wapi? Watalima wapi? Na je mwekezaji anaweza kuwafikia mwaka huu au anataka kulima vibarabara ili waonekane wanalilima shamba lote? Wahanga wananiuliza. Je, ungekuwa ni mwaka wa uchaguzi wangenyanyaswa? Nimewaambia nitawajibu siku nyingine.
By Kambi Mbwana, Mwananchi wa kawaida
0712 053949
kambimbwana@yahoo.com
Mungu ibariki Tanzania.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...