NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM
IFIKIE wakati kama Taifa tuone haya pale tunaposhuhudia wingi
wa wachezaji ambao mwisho wa siku ni masikini. Mchezaji anawika kwa nyakati
kadhaa, lakini ukimuangalia mfumo wake wa maisha utagundua hakuna kitu chochote
anachoweza kujivunia.
Mimi si wa kwanza katika kilio hiki. Watu mbalimbali
wameshawahi kuonyesha malalamiko yao, wakiwamo wanamichezo wenyewe. Kabla ya
kuhukumiwa kifungo cha miaka 3 jela, bondia tishio, Francis Cheka, mara kadhaa
Amelia juu ya maisha yake kuwa magumu, licha ya umaarufu aliokuwa nao.
Ukiacha Cheka, wapo wengine ambao majina yao hayalingani
kabisa na kipato chao, hususan hawa wanaocheza michezo tofuati na mpira wa
miguu wenye unafuu katika jamii yetu.
Wachezaji kama vile Mbwana Matumla, Rashid Matumla, Francis
Miyeyusho, Japhet Kaseba, unaweza kulia utakapogundua majina yao makubwa si
sawa na kipato chao na maisha yao kwa ujumla.
Na hili ndio sababu kuu ya kuwaathiri wanamichezo hao kisaikolojia.
Na suala hilo litazidi kuwazorotesha wao kimichezo. Kamwe siwezi kuvumilia. Ni
wakati sasa wa wanajamii kuweka mipango yenye tija na mbolea.
Tuelezane ukweli na kuamua kwa dhati kufanya mambo yenye
kusababisha maendeleo na mafanikio. Mabondia wetu na wanamichezo wote kwa
ujumla wawekewe mazingira bora na rafiki.
Kwa bahati mbaya, matatizo yote hayo yanaanzia chini ya
serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni ambako hakuna sera
au zipo lakini zina matege.
Na ndio maana tumekuwa na wanamichezo wengi wenye majina,
lakini ni masikini wa kutupwa. Hii si sawa. Tuweke mifumo mizuri si tu kwa
ajili ya kuendeleza michezo, bali pia kuwapatia maisha bora wanamichezo hao ili
waishi vizuri kulingana na majina yao.
Kuanzishwe mashindano, mapambano makubwa kwa mabondia wa
Tanzania, sambamba na kuwekewa mifumo ya kutoka nje na kushiriki kwenye matukio
makubwa yenye kuingiza fedha nyingi.
Kinyume cha hapo michezo na wanamichezo wetu wa Tanzania
wataendelea kuwa hohe hahe. Tatizo hili si rafiki kwa wanamichezo wetu. Na pia
ni sehemu inayoifanya michezo ishindwe kupiga hatua.
Ukiacha mpira wa miguu tena ule wa wanaume, michezo mingine
kwa Tanzania inatoa ajira kwa wanamichezo wetu au inawapotezea muda tu, maana
muda mwingi mazoezini, lakini hakuna wanachoambulia zaidi ya kufanikisha majina
makubwa, lakini mfukoni sifuri.
Hii ni hatari na haiwezi kuvumilika. Nani anafurahia tatizo
hili kwa wanamichezo wengi wa Tanzania? Je, wadau wa michezo na viongozi
wanaliangalia suala hili kwa kirefu?
Serikali inachoweza wao ni kutoa pongezi tu au kutoa pole
panapokuwa na msiba, lakini si kubuni au kusimamia sera zenye mashiko kwa ajili
ya kuendeleza michezo na kuwapatia maisha bora wanamichezo na Watanzania kwa
ujumla.
Tunapaswa kubadilika, kinyume cha hapo siwezi kuvumilia kuona
wanamichezo wetu wanaendelea kuogelea kwenye wimbi la umasikini, hali ya kuwa
wana vipaji kama vile vinavyowapatia utajiri nyota duniani kote.
Tuonane wiki ijayo
+255712053949
No comments:
Post a Comment