Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKA la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), limejitokeza
katika sekta nyeti ya michezo kwa kushirikiana na Klabu ya Real Madrid
kuanzisha kituo cha michezo nchini Tanzania.
Ujenzi huo utajumuisha viwanja vitano vya mpira wa miguu, mabweni ya
wachezaji na wageni, maduka na huduma nyingine muhimu, ambapo pia watajenga
uwanja wa gofu wenye mashimo 18 utakaoambatana na ujenzi wa nyumba za kisasa
katika eneo la ekari 400 lililopo katika mji uliopangwa kuwa wa kisasa wa
Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Hongera sana NSSF, ila wengine wapo wapi? Shirika hilo limefanya kitu
ambacho kitakuwa na mguso na uwezo wa kuibua vipaji vya vijana wetu. Hii ni kwa
sababu kwa miaka mingi Tanzania imeshindwa kufanya vizuri katika michezo,
hususan mpira wa miguu.
Kushindwa huko kunatokana na kukosa mipango yenye tija. Tunakuwa na
wachezaji ambao umri wao ni mkubwa. Nguvu zao nyingi zinaishia kwenye ligi za
mchangani na wanapoingia Ligi Kuu wamechuja.
Na ndio maana mara kadhaa wamekuwa na
ndoto ya kuona kunakuwa na vituo vingi vya michezo, bila kusahau ligi za vijana
nchini kote. Kila mmoja kwa nafasi yake akitimiza wajibu wake vizuri, maendeleo
yatapatikana.
Na hilo la wadau kushindwa kubuni na kusimamia miradi mikubwa na midogo inayohusisha
soka la michezo ya kuanzia umri mdogo ndio unaonifanya nishindwe kuvumilia.
Hakika siwezi kuvumilia. Angalau sasa tunaweza kupata cha kujivunia, tukiamini
kuwa mambo mengi yanayoanzishwa na NSSF Tanzania huwa na uhakika.
Ni jukumu la wadau wa michezo sasa kuona namna ya kuwaunga mkono NSSF juu ya
program yao hiyo, huku mchakato wa upatikanaji wa watoto ukianza rasmi mwishoni
mwa wiki iliyopita, katika viwanja vya Karume, jijini Dar es Salaam.
Ni vyema sasa tukaweka mipango na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunavuna
watoto wengi wanaoweza kufaidika kutokana na vipaji vyao vya michezo kwa
kuwanoa kuanzia chini hadi juu, maana ndio njia nzuri ya kuwakwamua.
Kinyume cha hapo tutaendelea kuwa mashabiki wa wachezaji wa Kimataifa
wanaowika duniani kote, hali ya kuwa tunao uwezo wa kuzalisha idadi kubwa ya
vijana kutoka nchini Tanzania, kama tutakuwa na mipango kama waliyokuwa nayo
NSSF.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment